Kwanini Israel inataka udhibiti wa eneo la mpaka wa Gaza na Misri?

    • Author, Alaa Rajai
    • Nafasi, BBC

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema eneo la mpakani kati ya Gaza na Misri linapaswa kuwa chini ya udhibiti wa Israel. Akielezea vita vya Israel huko Gaza vitaendelea kwa miezi mingi.

Wakati wa mkutano na waandishi wa habari, alisema, "eneo la mpakani (kati ya Gaza na Misri), lazima liwe chini ya udhibiti wetu. Ni lazima tulifunge eneo hilo. Na mpango mwingine wowote mbali na huo hautatoa uhakika wa kuikongoa Hamas, kama tunavyotaka."

Wachambuzi wa Misri wanahofia juu ya mvutano kati ya Misri na Israel ikiwa kutakuwa na mashambulio yanayolenga mpaka unaotenganisha Misri na Gaza, katika eneo ambalo linachukuliwa kuwa eneo maalumu la usalama.

Mvutano wa Misri na Israel

Israel inaamini mpaka wa Gaza na Misri ndio lango kuu la Hamas kupata silaha za magendo kupitia mahandaki ya chini ya ardhi, lakini Misri inaamini mpaka wa eneo hilo umedhibitiwa, na hakuna mahandaki au magendo kupita ardhi yake.

Mzozo huu kati ya majirani wawili waliotia saini makubaliano ya amani ulianza kwa siri, lakini Israel imetoa tamko hadharani la ulazima wa kulidhibiti eneo hilo.

Rais wa Misri, Abdel Fattah El-Sisi alikataa kupokea simu kutoka kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Israel.

Saa chache baada ya hatua hiyo, Hamas ilijitokeza kushukuru msimamo wa Misri wa kukataa uwepo wa jeshi la Israel katika mpaka wake, na kusisitiza umuhimu wa msimamo wa Misri katika kuwaunga mkono wananchi wa Palestina.

Misri imekataa mipango ya kijeshi ya Israel kupitia taarifa kali, iliyokanusha madai ya kuwepo operesheni za magendo ya silaha kuingia Ukanda wa Gaza kutokea eneo la Misri kupitia mahandaki.

Taarifa hiyo ilirejelea juhudi za Misri za kuondoa mahandaki 1,500 ambayo yalitumiwa kusafirisha wapiganaji na silaha kutekeleza operesheni za kigaidi huko Sinai, baada ya kupinduliwa utawala wa Muslim Brotherhood mwaka 2013.

Taarifa hiyo pia inaeleza kuwa, Israel imeanzisha tuhuma hizo ili kujipatia uhalali wa kuukalia kwa mabavu Ukanda huo wa Salah al-Din, unaojulikana kama Ukanda wa Philadelphia.

Kadhalika taarifa hiyo imesisitiza kuwa Misri ina uwezo wa "kutetea maslahi yake" ikiwa Israel itachukua hatua yoyote katika mwelekeo huo.

Ukanda wa Philadelphi ni upi?

Eneo hilo la mpakani liko kati ya Misri na Ukanda wa Gaza, lina urefu wa kilomita 14 kutoka Bahari ya Mediterania kaskazini hadi katika kivuko cha Kerem Shalom kusini.

Chini ya mkataba wa amani wa Misri na Israel wa 1979, eneo la hili ambalo lilikuwa chini ya udhibiti na ulinzi wa Israel kabla ya kujiondoa Ukanda wa Gaza mwaka 2005, Israel ilitia saini itifaki na Misri inayoitwa "Itifaki ya Philadelphia."

Itifaki hiyo inaweka mipaka ya uwepo wa shughuli za kijeshi kwa pande zote mbili katika eneo hilo, na itifaki hiyo inairuhusu Misri kupeleka wanajeshi la polisi 750 katika mpaka na Gaza, ili kupambana na ugaidi na upenyezaji wa silaha.

Miaka miwili baadaye, vuguvugu la Hamas lilichukua udhibiti wa eneo hili kwa upande wa Gaza, baada ya kuchukua udhibiti wa eneo lote la Ukanda wa Gaza.

Tangu wakati huo, Misri imeimarisha ulinzi wake kwenye ukanda huu wa mpaka.

Kwa nini Israel inataka kudhibiti eneo hilpo?

Kwa miaka mingi, mamia ya mahandaki yalichimbwa chini ya ukanda huu wa mpaka, ambao umezungukwa na Bahari kaskazini, Israel mashariki na kusini, na Misri upande wa magharibi.

Uwezo wa kijeshi wa vuguvugu la Hamas wakati wa vita vinavyoendelea - umeifanya Israel kuamini bado kuna mahandaki chini ya ukanda huu.

Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, Misri ilianzisha operesheni ya kijeshi dhidi ya waasi wenye silaha katika Rasi ya Sinai kwenye mpaka wa kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo.

Operesheni hiyo ilijumuisha uharibifu wa mahandaki yanayounganisha Ukanda huo na Misri, kwa lengo la kuzuia kupenya wanamgambo na watu wenye itikadi kali katika eneo lake.

Misri imekuwa ikiishutumu mara kwa mara Hamas kuunga mkono makundi yenye itikadi kali ambayo yanashambulia vikosi vya Misri, kufuatia kupinduliwa Rais wa zamani wa nchi hiyo Mohamed Morsi, mfuasi wa Muslim Brotherhood, iliyokuwa na uhusiano mzuri na Hamas.

Kivuko cha Rafah

Kuna lango moja kuu katika ukanda huu wa mpaka kati ya Palestina na Misri, ambalo ni kivuko cha ardhi cha Rafah; njia kuu na pekee iliyobaki ya Wagaza kuelekea ulimwengu wa nje, baada ya Israel kufunga vivuko vyote sita kati ya Gaza.

Upande wa Palestina wa kivuko cha Rafah ulikumbwa na mashambulizi ya Israel mara 4, kwa mujibu wa maafisa wa Misri.

Utawala wa Misri mara kwa mara ulitoa onyo kali kwa Israel dhidi ya operesheni zozote za kijeshi katika eneo hilo, hasa baada ya Israel kuwashambulia kimakosa askari wa Misri karibu na kivuko cha Kerem Shalom, katika tukio ambalo Israel iliomba radhi baadaye.

“Kurejea Israel katika udhibiti wa upande wa Wapalestina wa koridoo ya Philadelphia, ikiwa itashinda vita vinavyoendelea, kutahitaji ushirikiano wa usalama na Misri,” anasema Samir Ghattas, mkuu wa Jukwaa la Mashariki ya Kati la Strategic Studies.

Waangalizi wa mambo wanaamini udhibiti wa Israel wa Philadelphia utahitaji makubaliano, sawa na yale yaliyoidhinishwa 2005 baada ya Israel kujiondoa kutoka Ukanda wa Gaza.

Mkurugenzi wa Kituo cha Misri cha Thought and Strategic Studies anaeleza, "ikiwa Israel itadhibiti eneo hilo kwa upande wa Gaza, itakuwa na maana Israel itadhibiti kituo cha Rafah, ambacho kwa sasa ndio njia pekee ya kuelekea Ukanda huo ilio nje ya udhibiti wa Israel."

“Misri inahofia udhibiti wa Israel wa Philadelphia "utalifanya eneo hilo kuwa gereza la wazi, jambo ambalo litawasukuma wakaazi wa Ukanda huo kuhama kwa hiari,” anasema Samir Ghattas.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah