Uharibifu wa maeneo ya kidini huko Gaza

    • Author, Na Reha Kansara & Ahmed Nour
    • Nafasi, Ripota wa masuala ya dini wa WS Global na BBC Monitoring

Gaza ni nyumbani kwa baadhi ya makanisa na misikiti mikongwe zaidi duniani lakini mingi haijaepuka uharibifu mkubwa wa mashambulizi ya kijeshi ya Israel.

BBC World Service imekuwa ikithibitisha idadi ya maeneo ya kidini yaliyoharibiwa kabisa tangu vita hivyo vilipoanza Oktoba mwaka jana. Kwa kutumia ripoti za ndani, miongozo kutoka kwa mitandao ya kijamii na picha za satelaiti, tumehesabu sehemu 117 ambazo zimeripotiwa kuharibiwa kati ya tarehe 7 Oktoba na 31 Desemba.

Kutoka kwa hizo, tumethibitisha uharibifu wa sehemu ya misikiti 72 na makanisa mawili, ingawa takwimu kutoka Hamas zinaonyesha kuwa ni kubwa zaidi.

Kuthibitisha uharibifu wa sehemu zote ambazo tumehesabu kuna vikwazo. Picha za setilaiti huonyesha tu uharibifu kamili wa majengo ya kidini badala ya uharibifu kiasi, na katika baadhi ya matukio, ukosefu wa ushahidi umeacha matokeo yetu kuwa ya kutoeleweka.

Katika taarifa Hamas inasema misikiti 378 na makanisa matatu yameathiriwa tangu vita vilipozuka: "Hii si mara ya kwanza kwa utawala wa Israel kulenga misikiti kwa mashambulizi ya mabomu na uharibifu" lakini wakaongeza "ndio ukatili zaidi".

Vikosi vya Ulinzi vya Israel (IDF) vinahoji kuwa wanamgambo wa Hamas wanatumia sehemu za ibada kama sehemu ya kujificha na mahali pa kufanyia mashambulizi.

'Ilikuwa kifo cha papo hapo'

Inaaminika kuwa mojawapo ya makanisa kongwe zaidi duniani, St Porphyrius ni mojawapo ya makanisa machache yanayozunguka Ukanda wa Gaza. Wengi wa Wakristo wachache wa Gaza, wanaokadiriwa kuwa 1,000 kabla ya vita, wana uhusiano mkubwa na ardhi karibu na kanisa, iliyopewa jina la askofu wa karne ya tano, ambaye kaburi lake liko chini.

Kama Wakristo wengi wa Kipalestina, Marian Saba na familia yake walitafuta hifadhi ndani ya uwanja wa kanisa wakati wa vita, wakiamini wangekuwa salama. Lakini tarehe 19 Oktoba, usiku ulipofika, kombora la Israel liligonga moja ya majengo ya kanisa hilo, na kuua watu 18 na wengine wengi kujeruhiwa.

Marian alisema shemeji yake Soliman mwenye umri wa miaka 34 aliuawa alipokuwa akimkinga mwanawe kutokana na ukuta kuporomoka. "Lilikuwa tukio la kuogofya. Sijawahi kuona maiti. Sikujua la kusema," anasema. "Ilikuwa kifo cha papo hapo."

Rami Tarazi, ambaye alikuwa katika moja ya kumbi za kanisa hilo wakati wa mlipuko huo alisema: "Lilikuwa ni kombora la roketi ambalo lilikuwa kubwa hata watu waliokuwa kwenye ukumbi mwingine walitoka nje wakiwa na vumbi jeupe."

"Tulitoa watu 16 wakiwa vipande vipande na maiti mbili kamili," anakumbuka waziwazi. Mmoja wa watu waliouawa alikuwa binamu wa Rami mwenye umri wa miaka 36 Suliman, ambaye, saa moja kabla, Rami anasema alikuwa "akizungumza na kucheka" naye.

Wanajeshi wa Israel wamethibitisha kuwa sehemu ya kanisa hilo iliharibiwa katika shambulio ambalo walisema lilitekeleza katika kituo cha karibu cha jeshi la Hamas.

Kulingana na sheria ya kimataifa ya kibinadamu, kulenga majengo ya kidini kimakusudi wakati wa vita ni uhalifu wa kivita. Kuna hali hata hivyo ikiwa sehemu kama hizo zinatumiwa kwa madhumuni ya kijeshi ambapo zitalengwa kihalali .

Video zilizopakiwa na IDF kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha jeshi likiingia kwenye majengo ya kidini ambayo wameyalenga na kuonyesha njia za chini kwa chini ambazo inasema zinatumiwa na Hamas.

Baadhi ya video na picha zinazoshirikiwa mtandaoni pia zinaashiria kuwaonyesha wanajeshi wa Israel wakidharau utakatifu wa maeneo ya kidini na kutukuza uharibifu. Picha moja inayoonekana kwenye X, ambayo zamani ilijulikana kama Twitter, inamuonyesha mwanajeshi wa Israel akiwa amesimama mbele ya mnara ulioanguka ambao umechorwa kwa Kiebrania, na maneno haya: "hekalu litajengwa vizuri". BBC iliuliza IDF kuhusu picha hii lakini haikutoa maoni.

Profesa Georgia Andreou kutoka Taasisi ya Akiolojia katika Chuo Kikuu cha London amekuwa akiangalia uharibifu wa maeneo ya urithi katika Ukanda wa Gaza. Anasema maeneo mengi matakatifu yana umuhimu mkubwa wa kihistoria. "Inapaswa kutazamwa kama sehemu ya jaribio pana la kuondoa uhusiano ambao watu wameanzisha na sehemu hizi," anasema, na kuongeza, uharibifu wa maeneo matakatifu na ya urithi huko Gaza "ni mbaya zaidi kuwahi kuona. ".

'Nakosa sauti ya maombi'

Misikiti mingi imeharibiwa huko Gaza, na tofauti na wale wanaojificha makanisani, Waislamu wa Palestina wanachagua kutafuta kimbilio mbali na mahali pao pa ibada.

Huko Khan Younis, tulithibitisha kuharibiwa kwa msikiti wa Khalil Al-Rahman, ambao uliripotiwa kuharibiwa katika shambulio la anga katika eneo hilo.

Kama Muislamu mcha Mungu, Renad Alaa al-Bataa mara nyingi alitembelea msikiti huu, ambapo alijifunza kuhifadhi Quran. Lakini tangu vita kuanza hajarudi tena.

"Hapo awali, IDF ilikuwa nadra kulenga misikiti isipokuwa kama kuna watu wanaodaiwa kuwalenga wanamgambo. Lakini wakati huu, wameharibu misikiti kadhaa mizuri ambayo ilitulea na kutufundisha kuhusu dini yetu," anasema.

Wakati wa mapatano ya wiki nzima yaliyofanyika mwezi wa Novemba, anasema muadhini alibuni mnara wa muda na kuanza kuitisha sala mara tano kwa siku kutoka juu ya mabaki ya msikiti wa Khalil Al-Rahman. Anasema ilimletea hali ya usalama ambayo iliisha wakati Israeli ilipoanza tena mapigano dhidi ya Hamas.

Mojawapo ya picha kali za uharibifu zitakazojitokeza kutoka kwa Khan Younis ni video inayoonyesha kutandazwa kwa haraka na ghafla kwa msikiti wa Khalid bin Al-Walid. Imetazamwa karibu mara milioni 15 kwenye X.

Kulingana na Chris Partridge, mchambuzi wa silaha wa BBC, video hiyo inaonyesha bomu lililoelekezwa kwa usahihi ambalo limerushwa kutoka kwa ndege ikigonga msikiti huo kabla ya kulipuka na kuwaka wingu la moto na moshi. Kidokezo katika silaha iliyotumiwa , anasema, ni usahihi wake.

Haijulikani ni sehemu ngapi za kidini ambazo tumethibitisha zimeharibiwa na IDF au ni ngapi zimetumiwa na Hamas, hata hivyo IDF inasema wanafanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria za kimataifa kuvunja uwezo wa kijeshi na kiutawala wa Hamas na kuchukua tahadhari ili kupunguza madhara kwa raia.

Kuhusu kuharibiwa kwa msikiti wa Khalid Bin Al-Waleed na Msikiti wa Khalil Al-Rahman, IDF haikutoa maoni yoyote.

Huku kukiwa na uharibifu wa sehemu nyingi za ibada za Gaza, imani imezidi kuwa jambo lenye usalama wa kiroho kwa Wapalestina wengi wanaokimbia kifo.

Marian Saba na familia yake wanaendelea kujihifadhi katika Kanisa la Saint Porphyrius na takriban wengine 300, wakihudhuria Misa ya Jumapili kila wiki.

Siku tisa baada ya kuharibiwa, binti yake alibatizwa. Anaielezea kama wakati mchungu. Jambo ambalo linapaswa kuwa la furaha, lilisukumwa mbele kwa wasiwasi na hofu kwamba mtoto wake anaweza kuuawa .

Katika kambi ya Wapalestina waliokimbia makazi yao huko Rafah, Renad Alaa al-Bataa yuko mbali na nyumbani kwake na msikiti huko Khan Younis. Instagram sasa ni shajara yake, na kumbukumbu mara nyingi huchukua nafasi, anapochapisha picha za maisha yake ya zamani, pamoja na wakati wake kama mwanafunzi wa daktari wa meno,

Lakini anasema Quran, ambayo anaisoma kila siku, ni mahali pake pa kujifariji: "Inapunguza uzito wa usiku. Laiti ungejua jinsi usiku wa Gaza ulivyo mgumu."

Taarifa ya ziada: Mehdi Musawi

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah