Je, Wahouthi wana uwezo wa kuhujumu nyaya za mawasiliano chini ya bahari?

    • Author, Frank Gardner
    • Nafasi, BBC

Kulipiza kisasi kuko kwa aina nyingi. Waasi wa Houthi nchini Yemen hawajaficha azma yao ya kulipiza kisasi dhidi ya nchi za Magharibi kutokana na mashambulizi ya anga yanayoongozwa na Marekani ambayo yamekuwa yakilenga maeneo yao ya kurushia makombora na ndege zisizo na rubani.

Kuna mashambulizi ya Wahouthi zaidi ya 30 dhidi ya meli za kimataifa katika Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden, ambayo wanasema ni ya kuwaunga mkono Wapalestina huko Gaza.

Serikali halali ya Yemen, inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa mjini Aden imeonya kwamba Wahouthi, ambao waliteka sehemu kubwa ya Yemen mwaka 2014, wanatishia kuhujumu nyaya muhimu za mawasiliano chini ya bahari, zikiwemo za intaneti, zinazopita chini ya Bahari ya Shamu - zinazounganisha Asia na Ulaya.

Onyo hilo lilikuja baada ya chaneli inayohusishwa na Wahouthi kwenye mtandao wa Telegram kuchapisha ramani inayoonyesha njia za kebo za chini ya bahari katika Bahari ya Shamu.

Pia unaweza kusoma

Wana uwezo wa kufanya hivyo?

Waya hizi ambazo hubeba 17% mtandao wa intaneti duniani, mara nyingi ziko mamia ya mita kutoka juu ya bahari - na haziwezi kufikiwa na wapiga mbizi.

Marekani na Urusi zinadhaniwa kuwa na uwezo wa kukata nyaya hizo. Kwa kupeleka nayambizi ndogo kutoka nyambizi kubwa. Kisha kutumia mkasi mkubwa kukata nyaya kwenye sakafu ya bahari.

Lakini itakuwa vigumu sana kwa Wahouthi kufanya hivyo.

"Ni majigambo tu," ansema kamanda wa zamani wa jeshi la wanamaji la Uingereza, Adm John Gower kuhusu madai kuwa kundi hilo linatishia kuharibu waya.

"Itahitaji mshirika aliye na uwezo, mwenye nyambizi na uwezo wa kuziona waya hizo."

Wahouthi wana mshirika wao - Iran. Kwa msaada kutoka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran na Hezbollah ya Lebanon, Wahouthi wameunda makombora mengi na ndege zisizo na rubani.

Iran inaweza kuwawezesha Wahouthi?

"Sidhani kama Iran inataka kuzigusa waya hizi. Hasa kwa kutumia nyambizi zao," anasema kamanda wa zamani wa Jeshi la Wanamaji la Uingereza, Tom Sharpe.

Kwa Iran kuwezesha mshirika wake kuhujumu waya za intaneti zilizo chini ya bahari, itakuwa ni hatua ya hatari kwa upande wa Tehran.

Si Iran wala Marekani wanaotaka kuingia katika vita kamili kati yao na wameliweka hilo wazi.

Mzozo wa sasa kati ya Marekani na washirika wa Iran Mashariki ya Kati umeongezeka. Marekani ilitoa onyo siku kadhaa kabla ya kushambulia kambi za wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran nchini Iraq na Syria, na kuwaruhusu maafisa muhimu kuondoka.

Kukata nyaya za mawasiliano kutaongezeko mvutano ambao unaweza kusababisha mashambulizi ya kulipiza kisasi kwa Iran yenyewe.

"Iran itakuwa na hofu kupanua kampeni yao ya kimataifa ya mshambulizi," anasema Edmund Fitton-Brown, balozi wa Uingereza nchini Yemen kutoka 2015-2017.

Tishio lililotolewa hivi karibuni na Wahouthi kwenye chaneli yao ya Telegraph litakuwa gumu kutekelezeka. Kuna changamoto za kiufundi na hatari ya kisiasa kwa Iran.

Lakini Wahouthi wamewashangaza wapinzani wao hapo awali - wakirusha makombora kwenye ghala la mafuta la Saudia huko Jeddah 2022.

Pia wamenusurika kwa takribani miaka minane ya mashambulizi makali ya anga yaliyofanywa na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia ambao umeshindwa kuwatokomeza.

Na leo, licha ya mashambulizi ya mara kwa mara ya anga yanayoongozwa na Marekani kwenye vituo vyao vya makombora na ndege zisizo na rubani, hawaonyeshi dalili za kupunguza mvutano wao na Magharibi.

Wahouthi, ambao wanaogopwa na Wayemen wengi wanaoishi katika maeneo wasiyo yadhibiti, wamekuwa na nguvu na ushawishi.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na radhid Abdalla