Mashambulizi ya Kharkiv: Wanajeshi wa Ukraine waelekea mashariki

Chanzo cha picha, Getty Images
Maafisa wa Ukraine wanasema wanalenga miji ya eneo la Donbas mashariki baada ya kupata msururu wa mafanikio kwa kuyakomboa maeneo yao yaliyokuwa yametekwa katika mashambulizi ya haraka.
Katika siku za hivi karibuni jeshi la Ukraine lilirejesha sehemu kubwa ya eneo lililotekwa, na kuwalazimu wanajeshi wa Urusi kurudi nyuma.
Rais Volodymyr Zelensky alisema vikosi vyake vinaimarisha eneo lao zaidi ya kilomita za mraba 8,000 (maili za mraba 3,088) za eneo lililochukuliwa tena katika mkoa wa Kharkiv.
Rais wa Marekani Joe Biden alisema Ukraine imepata ‘’mafanikio makubwa’’.
Bw Biden alisema ni ‘’wazi’’ kwamba mashambulizi ya Ukraine yamekuwa na mafanikio makubwa, lakini alionya kwamba huenda yakawa ya ‘’muda mrefu’’.
Wakati Urusi bado inadhibiti karibu moja ya tano ya ardhi ya Ukraine, miji ya Donbas iliyoanguka mapema katika vita, sasa iko chini ya tishio kutoka kwa vikosi vya Kyiv vinavyoendelea kusonga mbele.
Baada ya kushindwa kuteka miji kote nchini, ukiwemo mji mkuu wa Kyiv, Urusi imekuwa ikielekeza nguvu zake katika maeneo ya Donbas, ambayo sehemu zake tayari zilikuwa chini ya udhibiti wa waasi wanaoungwa mkono na Urusi kabla ya Urusi kuanzisha uvamizi wake mwaka huu.
Andrey Marochko, kamanda wa kijeshi wa Jamhuri ya Watu wa Luhansk iliyojitangaza kujitawala - moja ya majimbo mawili yanayounda Donbas - aliambia vyombo vya habari vya serikali ya Urusi kwamba mapigano yamefika kwenye mipaka ya eneo hilo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Naye Serhiy Hayday, mkuu wa Ukraine aliye uhamishoni wa eneo la Luhansk, alisema vikosi vya Ukraine vinawakabili wanajeshi wa Urusi kwenye viunga vya Lyman.
‘’Kuna vita vikali huko Lyman kwa sasa, ambavyo nadhani vitadumu kwa siku chache zaidi,’’ Bw Hayday alisema katika mtandao wa Telegram.
Lyman ilitekwa na vikosi vya Urusi baada ya vita vya muda mrefu mwishoni mwa Mei.
Iko umbali wa kilomita 50 tu kutoka mji wa Donetsk, mji mkuu wa Jamhuri ya Watu wa Donetsk inayojitangaza kujitawala.
Kutekwa kwake kulikuwa mapinduzi ya wanajeshi wa Urusi, na kuipa Moscow udhibiti wa barabara kuu ya mashariki-magharibi.
Katika maeneo mengine, vikosi vya Ukraine vinasemekana kufika mpaka wa Urusi, na Bw Hayday alisema kukamata kwao miji miwili - Izyum na Kupiansk - kunaweza kuona njia za usambazaji kwa miji inayoshikiliwa na Urusi ya Severodonetsk na Lysychansk zikiwa hazina mawasiliano.
Kiwango sahihi cha mafanikio ya Ukraine hakijathibitishwa na BBC.
Wakati vikosi vya Kyiv vikihamia katika maeneo yaliyokaliwa kwa mabavu, madai ya uhalifu wa kivita wa Urusi yameanza kuibuka.
Wenyeji katika mji wa Balakliya waliambia BBC kwamba wanajeshi wa Urusi waliwatesa raia katika kituo cha polisi cha mji huo wakati wa uvamizi wao, na wengine walisimulia kuteswa kwa njia ya umeme walipokuwa kizuizini.

Ikulu ya Kremlin imekiri kwamba vikosi vyake vimeondoka katika baadhi ya miji ya mashariki, lakini ilikataa kuiita hilo kujisalimisha, badala yake ikasisitiza kuwa vikosi vyake vinajipanga upya.
Siku ya Jumatatu, Moscow ilisisitiza kwamba itaendelea na uvamizi wake ‘’mpaka malengo yote ambayo yaliwekwa hapo awali yafikiwe.’’
Lakini kasi ya kusonga mbele kwa vikosi vya Ukraine inaonekana kushangaza vikosi vya Urusi, na ripoti za baadhi ya vikosi vya Moscow kuacha sare zao na kujichanganya na raia.
Katika baadhi ya maeneo, walimu wa Urusi waliohamia miji na majiji ya Ukraine baada ya Moscow kunyakua udhibiti waliachwa nyuma na wanajeshi wanaorudi nyuma.
Idadi ambayo haijatajwa ya wanajeshi sasa wanazuiliwa na vikosi vya Ukraine na Naibu Waziri Mkuu Iryna Vereshchuk ameonya kwamba watakabiliwa na mashtaka.
Wakati huo huo, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alimtaka Rais wa Urusi Vladimir Putin kuingia tena kwenye meza ya mazungumzo na Ukraine haraka iwezekanavyo wakati wa mazungumzo ya simu ya dakika 90 siku ya Jumanne.
Msomaji wa serikali ya Ujerumani kuhusu wito huo alisema Bw Scholz alimtaka Bw Putin ‘’kutafuta suluhu la kidiplomasia haraka iwezekanavyo, kwa kuzingatia usitishaji mapigano, kuondolewa kabisa kwa wanajeshi wa Urusi na kuheshimu uadilifu wa eneo na uhuru wa Ukraine’’.
End of Pia unaweza kusoma:














