Vita vya Ukraine: Ushuhuda wa mateso ya Warusi wajitokeza katika maeneo yaliyokombolewa

K
Maelezo ya picha, Artem anasema alishikiliwa seli na Warusi kwa zaidi ya siku 4, na alipigwa kwa umeme.

 Kaskazini- Mashariki mwa Ukraine, kumeshuhudiwa mashambulio ya ulipizaji kisasi ya vikosi yaliyowezesha kutekwa upya eneo lenye ardhi tambarare, na kuviondoa nje ya eneo hilo vikosi vya Urusi.

Lakini katika maeneo mapya yaliyokombolewa,afueni na huzuni vimekuwa vikishuhudiwa - huku ushuhuda ukijitokeza wa mateso na mauaji wakati wa miezi ya uvamizi wa Warusi.

Artem,ambaye anaishi katika mji wa Balakliya katika jimbo la Kharkiv aliiambia BBC kuwa alishikiliwa na Warusi kwa zaidi ya siku 40, na aliteswa kwa kupigwa na umeme.

Balakliya ilikombolewa tarehe 8 Septemba baada ya kutwaliwa kwa zaidi ya miezi sita. Kitovu cha ukatili kilikuwa ni kituo cha polisi cha mji huo, ambacho Warusi walikitumia kama makao yake makuu.

Artem alisema kuwa aliweza kusikia mayowe ya maumivu na vitisho kutoka katika seli nyingine

 Wavamizi walihakikisha kuwa vilio vinaweza kusikika, alisema, kwa kuzima mifumo ya viyoyozi yenye kelele.

 "Waliizima ili kila mmoja aweze kusikia jinsi watu walivyokuwa wakipiga kelele wakati walipokuwa wakipigwa kwa umeme," alituambia. "Walifanya hili kwa baadhi ya wafungwa kila siku... Walifanya hivyo hata kwa wanawake".

 Na walifanya hivyo kwa Artem,ingawa yeye alifanyiwa hivyo mara moja tu.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Walinishikisha nyaya mbili za umeme " alisema.

"Tulikuwa na jenereta ya umeme. Kadri ilivyokwenda haraka, waliongeza kiwango cha umeme. Walisema, ukiiachilia, umeisha . Halafu walianza kuniuliza maswali. Walisema nilikuwa muongo, na wakaanza kuizungusha zaidi na hata zaidi na kiwango cha umeme kikaongezeka."

 Artem

alituambia kuwa alifungwa kwasababu Warusi walipata picha ya kaka yake, mwanajeshi, aliyekuwa amevalia sare.

 Mwanaume mwingine kutoka Balakliya alishikiliwa kwa siku 25 kwasababu alikuwa na bendera ya Ukraine, alisema Artem.

 Mkuu wa shule aliyeitwa Tatiana alituambia kuwa alishikiliwa katika kituo cha polisi kwa siku tatu na pia alisikia mayowe kutoka katika seli nyingine.

 Tulitembelea kituo cha polisi, na kuona sala za maombi kwa Mungu ambazo zilikuwa zimeandikwa kwenye ukuta mmoja wa seli pamoja na alama zinaozoonyesha ni jinsi gani siku zilikuwa zimepita.

 Maafisa wa polisi wa Ukraine wanasema wanaume wanane walishikiliwa katika seli yenye uwezo wa kuwahifadhi watu wawili.

Wanasema wakazi wa eneo hilo waliogopa hata kupita kwenye kituo hicho wakati Warusi walipokuwa wamekishikilia, walihofiwa kuchukuliwa na wanajeshi wa Urusi.

Getty

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Magari ya kijeshi yaliyoharibiwa yakiwa yameachwa na vikosi vya Urusi katika barabara ya Balakliya

 Katikati mwa jiji la Balakliya, kulikuwa na bendera ya Ukraine ikipepea tena, umati ulikusanyika karibu ya lori dogo lililokuwa limebeba chakula.

 Wengi katika foleni walikuwa ni wazee na walionekana wachovu, lakini walikuwa wenye furaha kuungana tena na marafiki zao huku wakikumbatiana kwa mara ya kwanza tangu walipofurushwa na Warusi.

 Mwendo mfupi tu kutoka mbali na eneo la upweke, baadhi ya wahanga wamelala watu waliozikwa na majirani zao. Msalaba uliotengenezwa kwa ubao ni ishara ya kaburi la dereva wa teksi aliyeitwa Petro Shepel. Abiria wake - ambaye utambulisho wake haujulikani – amezikwa kando yake.

Uvundo wa kifo ulijaa hewani wakati polisi walipokuwa wakifufua miili ya watu, na kuifunga ndani ya mifuko ya plastiki.

Maafisa wanasema wanaume hao wawili walipigwa risasi karibu na kituo cha ukaguzi cha Urusi katika siku ya mwisho ya uvamizi.

 Mama yake Petro, Valentyna, alitazama wakati miili yao ilipokuwa ikifufuliwa, na aliwalaumu Warusi waliomuua kijana wake.

"Ninataka kumuuliza Putin, ni kwanini alimpiga risasi na kumuua mwanangu" alilia. "Kwanini? Ni nani alimuomba aje hapa na silaha za aina hiyo za kutisha? Hakuwauwa watoto wetu tu, bali alituua sisi, mama zao.

"Siku hizi mimi ni mwanamke aliyekufa. Na ninataka kuwaambia akina mama wote duniani: fanyeni uasi dhidi ya muuaji."

 Njiani kuelekea Balakliya, tuliyaona magari ya kijeshi yenye alama ya vita "Z" – ambayo yalikuwa yameachwa na Warusi walipokuwa wakitoroka. 

Katika kijiji kilichopo karibu, tulionyeshwa uharibifu mkubwa kwa shule. Maafisa wa eneo hilo walisema hiki kilikuwa ni mojawapo ya vitendo vya mwisho vya uharibifu kabla ya Warusi kutimuliwa.

Akiwa amesimama katika eneo lililoharibiwa, mkuu wa jimbo la Kharkiv, Oleh Syniehubov, alisema kuwa kazi ngumu ilikuwa ni kurejesha usambazaji wa maji na umeme, lakini kuna hofu kuwa mifumo ya umeme huenda iliharibiwa.

Alipoulizwa na BBC iwapo anafikiri Warusi wanaweza kurejea alijibu: "Tuko katika vita, kuna hatari kila mara".

Getty