Mzozo wa Ukraine: Jinsi wanajeshi wa Ukraine walivyowazidi nguvu wale wa Urusi katika mashambulizi

Chanzo cha picha, Getty Images
Vikosi vya Ukraine viliwazidi wanajeshi wa Urusi kwa idadi ya nane kwa moja katika mashambulizi ya wiki iliyopita katika eneo la Kharkiv, afisa mkuu wa eneo linalokaliwa na Urusi anasema.
Vitaly Ganchev aliambia runinga ya Urusi kwamba jeshi la Ukraine limevikomboa vijiji vya kaskazini na kuingia katika mpaka wa Urusi.
Ukraine inasema imepata tena udhibiti wa kilomita za mraba 3,000 za (maili za mraba 1,158) za eneo katika vita hivyo vya miezi sita.
BBC haiwezi kuthibitisha takwimu hizi.
Jeshi la Ukraine linasema kuwa lilikomboa vijiji 20 katika muda wa saa 24 pekee, katika mashambulizi yake kaskazini-mashariki mwa nchi.
Maafisa wa ulinzi wa Uingereza wanasema mafanikio ya jeshi la Ukraine yatakuwa na "madhara makubwa" kwa muundo wa jumla wa uendeshaji wa Urusi.
Msemaji wa Kremlin hata hivyo hakukatishwa tamaa, akisema shughuli nchini Ukraine zitaendelea "hadi kazi zote zilizoahidiwa awali" zikamilike.
Urusi ilisema kuwa vikosi vyake vinafanya mashambulizi katika maeneo hayo ambayo Ukraine imechukua udhibiti wake.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hii ni pamoja na maeneo ya Izyum na Kupiansk ambayo yalichukuliwa na Ukraine siku ya Jumamosi. Urusi ilithibitisha kuondoka kwa vikosi vyake kutoka miji yote miwili, ambayo ilisema itawaruhusu "kujipanga upya".
Urusi imeshutumiwa kwa kulenga miundombinu ya kiraia ili kulipiza kisasi kwa kushindwa kwenye uwanja wa vita.
Moscow ilijibu siku ya Jumapili kwa wimbi la mashambulizi katika eneo lote la Ukraine, na kusababisha kukatika kwa umeme.
Kukatika kwa umeme kunaripotiwa kuathiri mamilioni ya watu katika mikoa ya Kharkiv na Donetsk. Meya wa jiji la Kharkiv anasema nguvu za umeme sasa imerejeshwa.
Ihor Terekhov aliliita jaribio baya na la kijinga la kulipiza kisasi kufuatia mafanikio ya hivi majuzi ya jeshi la Ukraine.
Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Oleksii Reznikov, alisema kipaumbele sasa ni kupata kudhibiti mafanikio ya kimaeneo yaliyopatikana katika eneo la Kharkiv.
Jeshi la Urusi linaonekana kuacha vifaa na risasi nyingi huku likijiondoa katika maeneo ambayo lilikuwa limeshikilia tangu wiki za kwanza za vita.
Mtengenezaji wa vifaru vya Urusi amebadilisha hadi muda wa uzalishaji wa vifaru hiyo kufuatia mafanikio hayo yalioafikiwa na jeshi la Urusi.
Wafanyikazi wa Uralvagonzavod huko Nizhny Tagil, kampuni kubwa zaidi ya kutengeneza magari ya kivita nchini Urusi, wameripotiwa kutoruhusiwa kwenda likizo kutokana na "lazima ya uzalishaji".













