Vita vya Ukraine: Putin asema vikwazo vya Magharibi ni pigo kwa maisha ya raia wa Ulaya

Chanzo cha picha, TASS VIA REUTERS
Vladimir Putin amelaani vikwazo vya Magharibi vilivyowekwa kwa sababu ya vita vya Urusi nchini Ukraine akivitaja kuwa homa inayoleta tishio kwa ulimwengu mzima.
Katika hotuba yake kwenye kongamano la kiuchumi mjini Vladivostok, alisema Urusi inakabiliana na ‘’uchokozi’’ wa kiuchumi wa nchi za Magharibi.
Lakini rais wa Urusi alionya ubora wa maisha kwa Wazungu ulikuwa umepata pigo kutokana na vikwazo huku nchi maskini zikikosa kupata chakula.
Pia alishutumu Ulaya kwa kudanganya nchi kuhusu nafaka ya Ukraine.
Kwa miezi kadhaa bandari za baharini za Ukraine zilizingirwa na vikosi vya Urusi, lakini tangu mauzo ya nje ya nchi hiyo kuanza tena mwanzoni mwa Agosti kiongozi wa Urusi alidai kuwa ni meli mbili tu za nafaka zilizokwenda Afrika - jambo ambalo si kweli.
Urusi ilizindua uvamizi wake tarehe 24 Februari na sasa imekalia karibu maeneo matano ya eneo la Ukraine.
Miezi sita baadaye, imerudishwa nyuma kutoka maeneo karibu na Kyiv na kaskazini na sasa inakabiliwa na shambulio la Ukraine kusini na mashariki.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mataifa ya Magharibi yalijibu vita kwa kuweka vikwazo kwa idadi kubwa ya watu wa Urusi, wafanyabiashara na mashirika ya serikali.
Umoja wa Ulaya umetaka kupunguza utegemezi wake kwa gesi na mafuta ya Urusi na Moscow imefunga bomba lake kuu la gesi la Nord Stream 1 hadi Ujerumani, ikiilaumu kwa maswala ya kiufundi.
Bei ya nishati imepanda na mawaziri wa EU wanakutana siku ya Ijumaa kujibu mzozo huo, na kiongozi wa Urusi alilaani pendekezo moja la kuwekwa kwa ukomo wa bei ya gesi ya Urusi kuwa hatua ya ‘kijinga’.
Bw Putin aliwaambia wasikilizaji wake kwamba nchi za Magharibi zinajaribu kulazimisha tabia yake kwa nchi nyingine.
Kampuni nyingi zilikimbilia kuondoka Urusi, alisema, lakini ‘’sasa tunaona jinsi uzalishaji na ajira barani Ulaya zinavyofungwa moja baada ya nyingine’’.
Hata hivyo, Urusi pia inakabiliana na hatua hiyo iliyosababisha mvutano kati yake na nchi za Magharibi, huku mfumuko wa bei ukiongezeka na makampuni yakitatizika kuagiza vipuri kutoka sehemu zingine za nje ya nchi.
Katika hotuba ambayo ilionekana kuwalenga waangalizi wa Magharibi kama vile hadhira ya ndani, alisema imani iliyopo kwa sarafu za dola, euro na pauni inapotea mbele ya macho ya watu.
Urusi, wakati huo huo, ilikuwa ikitoka kwenye vita na uhuru wake kuimarishwa: ‘’Nina hakika kwamba hatujapoteza chochote na hatutapoteza chochote.’’
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba alisema Urusi ilikuwa ikitaka kuchafua Ulaya na rasilimali zake za nishati: ‘’Putin anataka kuharibu utulivu na ustawi wa kila kaya barani Ulaya.’’
Mbunge wa ngazi ya juu wa China Li Zhanshu alikuwa akihudhuria kongamano hilo na rais wa Urusi alisema kuwa ‘’haijalishi ni kiasi gani mtu angependa kuitenga Urusi, haiwezekani kufanya hivyo’’.
Mashirika ya habari ya Urusi yalisema Rais Putin atakutana na mwenzake wa China Xi Jinping nchini Uzbekistan wiki ijayo.
Hadi makubaliano yaliyofadhiliwa na Umoja wa Mataifa yenye lengo la kuondoa vikwazo vya Urusi katika bandari tatu za Bahari Nyeusi ya Ukraine, mauzo ya nafaka yalikuwa yamepunguzwa hadi kiwango cha chini.
Usafirishaji umeanza taratibu na meli iliyokodishwa na Umoja wa Mataifa iliwasili Djibouti wiki iliyopita ikiwa imebeba nafaka kuelekea maeneo ya Ethiopia yaliyokumbwa na ukame huku meli nyingine ikiondoka kuelekea Yemen.
Meli kadhaa zimekwenda Misri pia.
Chini ya makubaliano hayo mizigo yote imeidhinishwa na kituo cha pamoja nchini Uturuki.
Kituo hicho kinasema tani 2m zimeidhinishwa kufikia sasa, ikiwa ni pamoja na Uturuki na Mashariki ya Kati pamoja na bandari katika EU.
Lakini Rais Putin alishutumu nchi nyingi za Ulaya kwa kuendelea kufanya kama wakoloni na akasema angependekeza kuwekewa vikwazo kwa mauzo ya bidhaa za Ukraine kwa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.
‘’Bila kuhesabu Uturuki kama nchi mpatanishi, karibu nafaka zote zinazochukuliwa kutoka Ukraine hazikusudiwa kwa nchi maskini zaidi na zinazoendelea, lakini kwa nchi za Umoja wa Ulaya,’’ kiongozi wa Urusi alisema.















