Zaporizhzhia: Dunia ilinusurika ajali ya mionzi ya kinyuklia - Zelensky

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Kinu cha kinyuklia cha Zaporizhzhia ndio kikubwa zaidi Ulaya

Ulaya nusra ikabiliwe na maafa ya mionzi siku ya Alhamisi wakati kinu cha nyuklia kinachokaliwa na Urusi kilipokatwa kutoka kwa gridi ya umeme ya Ukraine, Rais Volodomyr Zelensky amesema.

Ni umeme wa ziada uliosaidia mtambo huo wa Zaporizhzhia kuendelea kufanya kazi kwa usalama, aliongeza.

Moto ulikuwa umeharibu nyaya za umeme hapo awali, na kuuzima mtambo huo.

Kuna wasiwasi wa ongezeka la mapigano karibu na kinu hicho ambacho ndio kikubwa zaidi barani Ulaya.

''Iwapo majenereta hayangejiwasha yenyewe, ikiwa mitambo ya otomatiki na wafanyikazi wetu wa mtambo hawangechukua hatua baada ya kukatika kwa umeme, basi tungelazimika kukabiliana na matokeo ya ajali ya mionzi," Rais Zelensky alionya Alhamisi usiku.

Uharibifu huo ulisababishwa na moto ambao shirika la nyuklia la Ukraine lilisema kuwa uliingilia njia za umeme zinazounganisha mtambo huo siku ya Alhamisi, na hivyo kukatiza kwa muda Zaporizhzhia kutoka kwa gridi ya taifa kwa mara ya kwanza katika historia yake.

"Matokeo yake, ni kwamba vitengo viwili vya kufanya kazi vya kituo vilikatwa kutoka kwa umeme," maafisa wa Kyiv walisema.

Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) lilionya kwamba na "usambazaji wa nishati salama nje ya tovuti kutoka kwa gridi ya taifa ni muhimu kwa kuhakikisha usalama wa nyuklia".

.
Maelezo ya picha, Moto ukiwaka katika kinu cha kinyuklia cha Zaporizhzhia Ukraine
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alilaumu uharibifu huo kutokana na mashambulizi ya makombora ya Urusi, na katika hotuba yake ya usiku aliishutumu Moscow kwa kuiweka Ukraine na Ulaya "hatua moja mbali" na maafa.

Lakini gavana wa eneo hilo aliyeteuliwa na Urusi Yevgeny Balitsky alilaumu jeshi la Ukraine kwa mashambulizi hayo, akiwashutumu kusababisha kukatika kwa umeme katika eneo hilo.

BBC haikuweza kuthibitisha kwa kujitegemea ni nani aliyehusika.

Viwango vya mionzi karibu vilibaki kuwa vya kawaida licha yam tambo wa nyuklia la Zaporizhzhia kupoteza usambazaji wake mkuu wa umeme siku ya Alhamisi, maafisa wa eneo hilo waliripoti.

Kiwanda hicho "kimesalia kuunganishwa kwenye njia ya 330kV kutoka kituo cha karibu cha nishati ya joto ambacho kinaweza kutoa umeme wa ziada ikiwa inahitajika," IAEA ilisema katika taarifa, ikitoa mfano wa wakala wa nyuklia wa serikali ya Ukraine.

Iliongeza kuwa vitengo vyote sita vya vinu vya nyuklia vilisalia bila kuunganishwa kutoka kwa gridi ya umeme licha ya kurejeshwa kwa njia hiyo baadaye siku ya Alhamisi.

Kwa kawaida mtambo wa nyuklia hutoa moja ya tano ya jumla ya umeme wa Ukraine - hivyo kuendelea kukatwa kwake kutoka kwa gridi ya taifa kungeleta changamoto kubwa kwa Ukraine.

Eneo hilo la kiwanda hicho cha nyuklia limekaliwa na vikosi vya jeshi la Urusi tangu mapema Machi lakini linaendelea kuendeshwa na mafundi wa nyuklia wa Ukraine.

Kremlin imeashiria kuwa itawaruhusu wakaguzi wa kimataifa kuzuru jengo hilo - lakini hadi hilo kutendeka ni vigumu kuthibitisha kile kinachotokea .

"Karibu kila siku kuna tukio jipya katika au karibu na kinu hicho cha nyuklia cha Zaporizhzhia. Hatuwezi kupoteza muda zaidi," mkurugenzi mkuu wa IAEA Rafael Grossi alisema katika taarifa yake, akirudia wito wake wa kuongoza ujumbe wa kimataifa kwenda katika kinu hicho siku chache zijazo.

Wataalam wa nishati wana hofu kwamba baadhi ya mifumo ya usalama wa kinu hicho huenda ikafeli iwapo kitapoteza umeme wote.

Hatua hiyo inajiri kufuatia madai kutoka Kyiv kwamba Moscow huenda inajaribu kuondoa umeme kutoka kwa kinu hicho na Kuunganisha umeme huo kwa gridi ya Urusi.

Pia kulikuwa na ripoti za vyombo vya habari siku ya Alhamisi kuhusu ukosefu wa umeme katika miji na vijiji katika maeneo ya Ukraine yanayokaliwa na Urusi.

Meya wa mji wa Enerhodar, ambao upo Jirani na kinu hicho alisema siku ya alhamisi kwamba mji huo hauna umeme au maji kabisa na pia kulikuwa na ripoti za ukosefu wa umeme katika miji ya Ukraine inyokaliwa na Urusi ya Melitopol na Kherson.

Maafisa wa Washington walishtumu mpango wowote wa Moscow kupeleka umeme huo unaotolewa na kituo hicho cha Zaporizhzhia kutoka kwa gridi ya kitaifa la Ukraine.

Umeme unaozalishwa na kinu hicho cha kinyuklia ni wa raia wa Ukraine’’, Msemaji wa wizara ya masuala ya kigeni wa marekani Vedant Patel alisema siku ya Alhamisi jioni , akiongezea kwamba , hakuna taifa linalopaswa kubadilisha kinu cha kinyuklia kuwa eneo la vita.