'Nilikuwa muamuzi wa Primia Ligi lakini sasa najifunza kutembea tena'

Muda wa kusoma: Dakika 4

Uriah Rennie alifahamika na mamilioni ya mashabiki wa soka baada ya kuwa muamuzi wa kwanza mweusi wa Ligi Kuu ya Uingereza.

Mara baada ya kutajwa kuwa afisa wa mechi "aliye fiti zaidi" katika soka la kimataifa na mtaalam wa sanaa ya karate, sasa anajifunza kutembea tena baada ya hali adimu ya kiafya iliyomfanya kupooza kuanzia kiunoni kwenda chini.

Baada ya kukaa kwa miezi mitano hospitalini, mzee huyo mwenye umri wa miaka 65 amezungumza na BBC News kuhusu ukarabati, ari yake ya kukabiliana na hali yake na jukumu jipya kabisa.

Rennie, ambaye alisimamia zaidi ya mechi 300 za ligi kuu kati ya 1997 na 2008, alikuwa katika safari ya kusherehekea siku ya kuzaliwa Uturuki mwaka jana alipokumbwa na maumivu ya ghafla kwenye mgongo wake.

"Nilidhani nilikuwa nimelala tu kwenye chumba cha kupumzika cha jua, nilitarajia kwenda upanda mwavuli angani lakini kwasababu ya maumivu ya mgongo sikuweza kwenda," anasema.

"Mwisho wa likizo sikuweza kulala , nilikaa macho kutokana na maumivu, na nilipofika nyumbani nilitembea kwa shida."

Rennie aliweka historia mwaka wa 1997 aliposimamia mechi kati ya Derby County na Wimbledon, na kuwa mwamuzi wa kwanza mweusi wa daraja la juu.

Mwanaume huyu ambaye ni mrefu kwa kimo na mtaalam wa ndondi za mateke na aikido, wachezaji waliokuwa wakipinga waligundua kwa haraka kwamba alikuwa amejiweka sawa wakati wa makabiliano

Akiwa mwamuzi huko Sheffield tangu 1996, amefanya kampeni katika masuala kama vile kuboresha usawa na ushirikishwaji katika michezo, kusaidia afya ya akili na kukabiliana na kunyimwa.

Rennie alikuwa kwenye harakati za kuanza kazi mpya kama Chansela wa Chuo Kikuu cha Sheffield Hallam alipolazwa katika Hospitali Kuu ya Kaskazini mnamo Oktoba.

"Nililala kwa mwezi mmoja chali na miezi minne mingine huku nikiwa nimekaa kitandani," anasema.

"Waliniweka hospitalini hadi Februari, walikuta kinundu kikinisukuma kwenye uti wa mgongo na ilikuwa ni hali ya nadra ya mishipa ya fahamu hivyo si kitu ambacho wanaweza kukifanyia upasuaji.

"Imebidi nijifunze kutembea tena, ninarekebisha miguu yangu."

"Ilikuwa ya kushangaza ...Sikuwa na matatizo yoyote ya nyuma ya awali lakini ghafla sikuweza kutembea nilikuwa katika kitengo cha wagonjwa wa mgongo."

Akizungumzia harakati zake za sasa, anasema: "Ninaweza kusongesha miguu yangu na ninaweza kusimama na mikongojo iliyounganishwa kwenye kiti changu cha magurudumu ."

Kwa mzaha anaonyesha kiti cha magurudumu kwenye bodi karibu na nyumba yake, na mazoezi ya viungo - physiotherapy, inachukua muda mwingi wa siku yake.

"Ninatikisika kwenye kiti changu nikifanya mazoezi yangu, mimi ni mgonjwa mzuri sana, anayetii," anacheka.

"Hali hii imekuwa ya kufadhaisha lakini familia na marafiki wamekuwa wa maana sana, hospitali ilikuwa nzuri kabisa na chuo kikuu kimekuwa cha kipekee."

Anaanza rasmi kazi kama chansela wa chuo kikuu mwezi Mei, kazi ambayo ameazimia kuichukua licha ya hali yake iliyompata hivi majuzi.

"Nilisisitiza nilitaka kuleta mabadiliko katika Sheffield na kwa jamii za hapa," anasema.

"Niliendelea kufanya kazi na timu za michezo za kijamii nikiwa hospitalini, nikiwaelekeza kutoka kitandani mwangu."

Alisomea MBA katika chuo kikuu wakati wa taaluma yake ya uamuzi na akapokea shahada ya udaktari wa heshima mnamo 2023 kwa kazi yake ya michezo na jamii za mitaa.

"Ninalenga kuwa bora zaidi niwezavyo kimwili," anasema.

"Hakuna mtu aliyeniambia sitatembea tena, lakini hata kama mtu alisema kwamba nataka kusema nilifanya kila niwezalo kujaribu."

Rennie, ambaye alihamia Uingerza kutoka Jamaica akiwa mtoto mdogo na kukulia katika eneo la Wybourn mjini humo, anasema kuwa muamuzi wa kwanza mweusi ilikuwa ni "kuunda urithi wa kuwawezesha watu wengine kusimama kwenye mabega yako".

Akizungumzia changamoto yake ya hivi punde, anasema matatizo ya uti wa mgongo yamempa mtazamo mpya wa maisha.

"Watu wengi wako kwenye viti vya magurudumu, lakini haviwazuwii kutimiza ndoto zao," anasema.

"Imenifanya niwe mvumilivu na mwenye nguvu na sitakata tamaa kamwe - siko peke yangu, kuna kijiji kinanisaidia."

Anamalizia hivi: "Ninatambua jinsi mambo yalivyo magumu maishani sasa.

"Sijui kama nitatembea kikamilifu, lakini najua ninachohitaji kufanya ili kujaribu na kamwe usikate tamaa."