Ni klabu gani bora ya muda wote ya soka nchini Uingereza?

Muda wa kusoma: Dakika 4

Ni klabu yenye vikombe vingi zaidi? Au ile yenye mapato makubwa zaidi? Au yenye wafuasi wengi zaidi katika mitandao ya kijamii? Ama klabu yenye uwanja mkubwa zaidi wa soka?

Katika mjadala huu hakuna mtu anayeweza kushinda. Lakini BBC Sport hivi karibuni iliwauliza takribani wafanyakazi wake 250 kote Uingereza kujibu swali hilo lisiloweza kujibiwa.

Kulikuwa na mabishano mengi. Lakini mwisho tulipata orodha ya klabu zilizotajwa sana katika 10 bora na vigezo vilivyotumika. Je, wewe utakubaliana na orodha hii? Pengine hapana.

Pia unaweza kusoma

Vilabu 10 bora Uingereza

Orodha hii ni kwa mujibu wa BBC Sport

  • Manchester United
  • Liverpool
  • Arsenal
  • Manchester City
  • Celtic
  • Chelsea
  • Tottenham Hotspur
  • Rangers
  • Aston Villa
  • Newcastle United

Ili kujaribu kutoa sababu kwa nini orodha ya BBC ni hii, tumeangalia mambo fulani ili kuona ni vilabu gani vinaongoza.

Iliyoshinda mataji mengi zaidi

Vilabu 10 vilivyoshinda mataji mengi Uingereza. Rangi ya njano ni mataji ya English First Division na Primia Ligi hadi kufikia Machi 2025. Rangi nyeusi ni mataji ya ligi za ndani. Rangi kijani ni mataji ya kimataifa au Ulaya.

Kikawaida vilabu huhesabiwa ni bora ikiwa vitashinda makombe. Linapokuja suala la mataji makubwa, wababe wa jiji la Glasgow, Celtic na Rangers wanaongoza kwa kuwa na makombe mengi zaidi kuliko timu yoyote nchini Uingereza.

Liverpool ndio klabu yenye mafanikio zaidi England, huku Manchester United ikifuata ya pili - na Liverpool wanaonekana kuwa na uwezekano wa kuifikia rekodi ya United ya mataji 20 ya ligi kuu msimu huu.

Pia wana mataji mengi ya Ulaya kuliko timu nyingine yoyote ya Uingereza, huku Arsenal wakiwa wanaongoza kwa mataji ya FA.

Ubabe wa hivi karibuni wa Manchester City umewapandisha kwenye viwango vya ubora, na kushinda mataji sita kati ya saba ya Ligi ya Kuu ya England na kufanikiwa kutwaa mataji matatu ya kihistoria katika msimu mmoja wa 2022-23.

Yenye wafuasi wengi zaidi

Vilabu 10 vyenye wafuasi wengi katika mitandao mikubwa minne ya kijamii hadi kufikia Machi 2025. Idadi hii iko kwenye mamilioni.

Baadhi ya watu wanaweza kupuuza wafuasi wa vilabu katika mitandao ya kijamii kuwa si jambo la muhimu. Lakini wafuasi hao wanatupa dalili ya jinsi vilabu vilivyo na mashabiki wengi sio tu Uingereza lakini ulimwenguni.

Manchester United wana wafuasi wengi zaidi katika mitandao ya kijamii ukijumuisha wafuasi wote katika majukwaa makubwa manne, huku vilabu vingine vikifanya vyema kwenye jukwaa moja moja.

Manchester City wana ufuasi wachache kwa idadi ukijumlisha wafuasi wao wote kwenye mitandao ya kijamii kuliko wapinzani wao wa jiji United, lakini wana wafuasi wengi zaidi kwenye Tik Tok, huku Tottenham wakiwa katika nafasi ya sita kwa idadi jumla ya wafuasi lakini wana wafuasi wengi Tik Tok kuliko klabu yoyote.

Mapato mengi na uwanja mkubwa

Vilabu 10 vyenye mapato makubwa Uingereza, mapato hayo yako kwenye mamilioni. Chanzo cha orodha hii ni Deloitte.

Manchester City ndio wanaongoza kwa kuzalisha mapato mengi. Kulingana na utafiti wa Deloitte Money League, City ilipata mapato mengi zaidi ya pauni milioni 708 msimu wa 2023-24 kuliko klabu yoyote ya Uingereza.

Ikiwa ubora wa klabu ni kuwa na uwanja mkubwa, basi mashetani wekundu, Manchester United ndio wanashika nafasi ya kwanza.

Wembley uwanja wa nyumbani wa timu ya taifa ya England, ndio uwanja mkubwa zaidi kwa sasa, una uwezo wa kuchukua watu 90,000.

Lakini Old Trafford wa United, ndio uwanja mkubwa zaidi kwa vilabu na United pia wana mipango ya kujenga uwanja mkubwa zaidi ya Wembley - kwa pauni bilioni 2, utakao kuwa na uwezo wa kuchukua watu 100,000.