Kwanini Wamarekani weusi wameamua kurejea Afrika?

Chanzo cha picha, ASPT SENEGAL
Kuna idadi kubwa ya Wamarekani wenye asili ya Afrika, wakiwa katika harakati za kutafuta historia zao na asili zao, wanaoamua kufanya uamuzi wa kudumu wa kuondoka Marekani na kuhamia Afrika, kwenye ardhi ya mababu zao na kuchangia katika maendeleo ya nchi zao asili.
Kwa wengine, kuhamia Afrika ni kuonyesha hitaji lao kurejea kwenye chimbuko na asili zao.Na hii mara nyingi huanza na vipimo vya kijenetiki.
Kwa kutumia wito wa Rais wa zamani wa Ghana, Nana Akufo-Addo, akiwasihi Waafrika waishio nje ya Afrika kutembelea nchi hiyo, AdaEze Naja Njoku, afisa wa zamani wa jeshi la Marekani alichangamkia fursa adhimu kwake.
"Nilitaka kujua ni wapi nilipotoka. Nilipokea majibu yangu (ya vipimo vya DNA), mara moja nikaamua kurejea Afrika.
Nilifanya utafiti mwingi kabla ya kuondoka kuelekea Cameroon. Nilianza safari yangu mwaka 2010," asema Naja.
Kwa Naja, ilikuwa ni kurejea "nyumbani" na alikuwa na uhakika kwamba mtoto wake wa wiki 6, ambaye alisafiri naye kwenda Cameroon, angeanza maisha yake kwa usahihi.
"Nilipokea mapokezi ya kipekee kule. Familia yangu mpya ilinijulisha jukumu la kutafuta wanandugu wengine wa familia yetu na kuwaleta nyumbani," anafafanua.
Naja alifanya safari ya kwenda Cameroon kwa ushirikiano na shirika la Roots to Glory, shirika lililoanzishwa Maryland, Marekani, linalosaidia Wamarekani wenye asili ya Afrika, hasa waathirika wa utumwa nchini Marekani, kuungana na chimbuko na asili zao.
"Ilinichukua miaka 7 kupata binamu yangu lakini leo nina 30. Waliniambia simulizi za familia zao. Asili yangu ni Ibo, Peul na Yoruba.
Sasa nimepata kujua taarifa iliyokosekana katika historia yangu na maisha yangu. Wazazi wangu wapya wananiita kila wiki kuniangalia. Wananipa hisia halisi za kuwa na familia," anasema.

Chanzo cha picha, Ada Anagho Brown
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Dkt Obadele Kambon alihamia Ghana mwaka wa 2008 na hajawahi kurudi.
Mmarekani huyu mwenye asili ya kiafrika aliondoka Marekani baada ya kuwa mhanga wa tukio la kibaguzi lililohusisha maafisa wa polisi.
Dk Kambon alikamatwa na kuhukumiwa huko Chicago - alikokuwa akiishi - baada ya kushutumiwa na polisi kwa kumiliki bunduki iliyowekwa chini ya kiti cha gari lake na kukusudia kufyatua risasi alipokuwa akiendesha gari.
Ni kweli, alikuwa na bunduki isiyo na leseni kwenye gari lake, iliyotumiwa hapo awali kulinda eneo la kambi.
Baada ya kuachiliwa huru na mahakama, Dk. Kambon na familia yake walihamia Accra, Ghana, ili kuepuka ukatili wa polisi na aina nyingine za ubaguzi wa rangi nchini Marekani.
Dkt Kambon, aliyeshtushwa na shutuma hizo wakati huo, anakumbuka akiapa kuondoka Marekani alikozaliwa: "Sitawahi tena kurudi katika eneo la mamlaka ambapo maafisa wa polisi weupe na jaji wakora watakandamiza familia yangu, mke wangu na watoto wangu kwa kukurupuka.
Bw Kambon, ambaye sasa amejijengea maisha mazuri, anatazamia kuishi kwa uhuru, jambo analosema alinyimwa nchini Marekani.

Chanzo cha picha, Obadele Kambon
Tangu kuanzishwa kwake mwaka wa 2012, shirika lisilo la kiserikali la Roots to Glory lenye makao yake huko Maryland, Marekani, limekaribisha mamia ya wasafiri kwa safari maalum za kutembelea nchi za Afrika Magharibi na Kati.
Muungano huu huwasaidia Wamarekani wenye asili ya Afrika, hasa wazao wa watumwa nchini Marekani, kuungana na nchi za mababu zao na watu wao.
"Nilianzia Roots to Glory kwa sababu nilijua wangetaka kujua walikotokea baada ya kuchukua vipimo vya DNA," muasisi wa kampuni Ada Anagho Brown aliambia BBC Africa.

Chanzo cha picha, Ada Anagho Brown
"Mimi ni mzaliwa wa Cameroon na nilikulia Marekani tangu utoto. Daima nilikuwa na shauku kuhusu utamaduni wangu, hasa utamaduni wa Kiafrika. Najihisi nipo katikati ya tamaduni za Marekani na Afrika, na naelewa dunia zote mbili.
"Hivyo ilikuwa shauku yangu kusaidia wale wanaotafuta asili zao na historia yao, kuwaunganisha tena na urithi wao kupitia kazi tunayoifanya leo.
Tunaongoza shughuli Afrika na tunafanya mipango mbalimbali Marekani, kama vile matukio na sherehe za kubatiza kwa kupatiana majina. Kila kitu tunachofanya kinalenga kuwasaidia watu kuelewa vyema ni wao ni nani."
"Ninaona kazi inayofanywa na Roots to Glory kama aina ya kurejesha fadhila. Tunajaribu kurekebisha kile kilichovunjika miaka mingi iliyopita. Tunasaidia watu kupata asili zao, na hiyo pia ni sehemu ya fidia. Tunawawezesha watu kurudisha majina yao, yale yaliyochukuliwa kutoka kwao wakati mababu zao walipopoteza asili zao. Hiyo pia ni fidia. Tunawasaidia kujifunza kuhusu viungo na desturi za kupika za mababu zao. Ni muhimu kwamba watu wetu wa ughaibuni waweze kuelewa bara la Afrika kupitia mtazamo wa watu wake, chakula chake, utamaduni wake na desturi zake."

Chanzo cha picha, Ada Anagho Brown
"Watu wengi walioko ughaibuni wanafanya mipango ya ziada, ya kurejea kwenye asili. Ndio maana makundi mengi sasa yananunua ardhi kwenye bara la Afrika.
Kwa nini? Kwanza, kwa sababu wanaona haja ya kuwa kwenye ardhi ya mababu zao.
Pili, wanataka kupata jamii inayoshirikiana, inayojua na kuelewana bila ubaguzi, bila uonevu, bali kwa upendo na wema.
Nina imani kuwa waishio ugenini watakaporejea barani, sisi kama watu wa Afrika tutakuwa na nguvu zaidi. Pamoja, tutafanya kazi, tutakua na tutainua bara hili hadi kiwango kipya."
Zaidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika 8,000 wamegundua asili yao Afrika (Ghana, Benin, Nigeria, Liberia, Sierra Leone, Cameroon) kupitia vipimo vya DNA.
Wengi wanaelezea uzoefu huu kama sherehe ya kurudi nyumbani, kufahamu kwa kina utamaduni na kuhuisha asili ya kiroho, vyote kwa pamoja.
Kuongezeka kwa idadi ya watu wanaofanya vipimo vya DNA kumekuwa na nguvu kubwa hasa kwa watu wa asili ya Kiafrika wanaotaka kuelewa vyema maeneo maalum au makabila ambayo familia zao zinakotokea.
Kwa sababu ya historia yake kama bandari kuu wakati wa biashara ya utumwa, Ghana mara nyingi huwa ni kituo muhimu katika safari za kurejesha wasaka chimbuko lao Afrika.
Kati ya karne ya 16 na 18, maelfu kadhaa ya watu waliotekwa utumwani walipita katika maeneo kama Kasri la Elmina, kabla ya kupelekwa kwenye meli kwenda Amerika ya Kaskazini na Kusini.
Leo, ziara za urithi kama ile ya Kensington ya "Safari ya asili hadi Mlango wa Kurejea Usio na Marejeo" hutoa ziara za maeneo haya ya kihistoria, zikifuatana na mikutano na wataalamu ili kuchunguza simulizi za makabila na vikundi vya asili za wageni, na kujifunza kuhusu uhamiaji wao, desturi na tamaduni zao.
Mwaka 2000, Ghana ikawa taifa la kwanza katika bara hilo kupitisha sheria ya makazi, ikiwaruhusu watu wa asili ya Kiafrika kuomba na kupata makazi ya kudumu katika nchi hiyo.
Angalau Wamarekani wenye asili ya Afrika 3,000 wamehamia Ghana tangu mwaka 2019, kufuatia kampeni ya serikali ya Ghana iliyopewa jina la "Mwaka wa Kurejea."
Kampeni hii pia ilizingatia kumbukumbu za miaka 400 tangu kuwasili kwa Waafrika wa kwanza waliotekwa utumwani katika mji wa Jamestown, Virginia.

Chanzo cha picha, PRESIDENCY OF GHANA
Wamarekani wenye asili ya Afrika milioni 47.2 wanaishi Marekani
Utafiti uliofanywa na Kituo cha Utafiti cha Pew chenye makao yake mjini Washington, Ulichapishwa Februari 2023, uligundua kuwa idadi ya Wamarekani weusi wanaoishi Marekani ilifikia milioni 47.2 mwaka 2021.
Huku majimbo ya Kusini yakiendelea kuona idadi ya watu weusi miongoni mwa wakazi wao ikiongezeka, idadi ya watu weusi pia inaongezeka katika maeneo mengine ya nchi.
Vizazi vipya vya Wamarekani wenye asili ya Afrika wanazidi kufanya ziara zinazowaunganisha na ardhi na tamaduni ambazo babu zao walilazimishwa kuachana nazo.
Kulingana na kikundi cha utafiti cha Wamarekani wenye asili ya Afrika, Hifadhidata ya Biashara ya Watumwa ya Trans-Atlantic, Waafrika 388,000 walifikishwa Amerika Kaskazini wakati wa kipindi cha biashara ya utumwa.
Imetafsiriwa na Martha Saranga












