“Kodi ya watu Weusi” – Sababu ya vijana wa Kiafrika ughaibuni kutaka kuacha kutuma pesa nyumbani

.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Elsa Majimbo
Muda wa kusoma: Dakika 4

"Kutuma pesa nyumbani au kwa jamaa zako ni mazoea ya kawaida ya Kiafrika ambayo nayachukia kabisa," alisema mtu mwenye ushawishi mitandaoni kutoka Kenya Elsa Majimbo, mapema mwezi wa nane mwaka 2024, katika mdahalo uliofutwa wa TikTok ambao ulizua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 23, ambaye alijipatia umaarufu mkubwa wakati wa janga la corona kupitia video zake za vichekesho, aliibua hisia mseto ilipofika wakati wa kujadiliana na wafuasi wake milioni 1.8 kile kinachojulikana kama "kodi ya watu weusi" maarufu kama “Black Tax”.

"kodi ya watu weusi" ama “Black Tax” ni pale Waafrika wanaopata mafanikio kidogo, iwe nyumbani au nje ya nchi, wanapolazimika kutegemewa na wanafamilia isio na uwezo.

Kusaidiana kunaonekana kama sehemu ya ndani ya falsafa ya Kiafrika ya ubuntu, ambayo inasisitiza umuhimu wa familia na jamii, badala ya mtu binafsi mwenyewe.

Swali kwa wengi ni je huu ni mzigo usio wa lazima na usiokubalika au ni sehemu ya wajibu wa jamii kusaidia kuwavuta wengine.

Lakini Bi Majimbo, ambaye sasa anaishi Marekani, hakubaliani na tabia hiyo.

Katika video hiyo alisema baba yake alikuwa amewasaidia watu wa familia yao wengi kwa miaka mingi na sasa walikuwa wanamtafuta yeye kumuomba msaada. Alilalamika sana kuhusu ndugu yake mmoja ambaye hakumtaja jina.

"Umekuwa ukimuomba baba yangu fedha kabla hata sijazaliwa. Nilizaliwa, nililelewa, nilikua, sasa unaniomba fedha – wewe ni mvivu. Siwezi kuendekeza tabia zako ."

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakati wengine wakimuunga mkono, wengine wamepinga msimamo wake. Haijabainika kwa nini video hiyo iliondolewa kwenye mtandao wa TikTok, na timu ya usimamizi ya Bi Majimbo haikujibu ombi la BBC la kutoa maoni yoyote.

Lakini kwa wengi, bila kujali kile wanachoamini binafsi, ni ngumu kukataa kusaidia jamaa zako kwa sababu misingi ya jamii ambayo walilelewa.

Kunaweza kuwa na hali ya kujivunia kusaidia na kutunza familia yako, ingawa inaweza pia kuwa mzigo mkubwa.

Aliyekuwa mwalimu nchini Zimbabwe, mwenye umri wa miaka 50, ambaye aliomba kutotajwa jina, aliiambia BBC kuwa miaka 30 iliyopita karibu mshahara wake wote wa kwanza wa takriban dola 380 za Zimbabwe ulienda moja kwa moja kusaidia ndugu zake tisa.

"Baada ya kumaliza kununua sare za shule, nguo na mboga, nilikuwa nimebakiwa na dola 20," aliiambia BBC kwa sauti iliyoonyesha vyote heshima na kuudhika.

Ingawa hii ilimaanisha kwamba alilazimika kununua chakula kwa mkopo, alisema kuwa kama mtoto mkubwa ilitarajiwa kuwa angekabidhi pesa taslimu pale atakapo anza kupata mshahara.

Mshahara wake haukuwa wake peke yake bali wa familia yake pia.

Alipoolewa, majukumu yake yaliongezeka hata zaidi. Wakati fulani, ilimbidi achukue mkopo ili kumlipia shemeji yake ada ya shule baada ya kuibiwa wakati akienda kuweka hundi kwenye benki. Ilimchukua miaka miwili kulipa.

Sandra Ajalo, mfanyabiashara na mbunifu wa mitindo ya nywele mwenye umri wa miaka 28, nchini Uganda, anashukuru kwa msaada ambao ndugu zake walitoa kwa familia yake wakati anakua.

Kwa Waafrika walio ughaibuni shida inaweza kuwa kubwa zaidi kwani watu wana matarajio makubwa zaidi kutoka kwao kutokana na imani kwamba walio kwenye mataifa ya nje wanapata fedha nyingi.

Gabe Mutseyekwa, mwenye umri wa miaka 35, ni mwanaume mwenye asili ya Zimbabwe ambaye ameishi Ujerumani kwa zaidi ya miaka mitano. Alisimama kidete na kuiambia familia yake kuwa ataacha kutuma malipo ya kila mwezi kwa sababu alikuwa anashindwa kuweka akiba kwa ajili ya maisha yake ya baadaye.

Familia yake hawakulipokea hili vizuri - lakini hatimaye walikubali.

"Waligundua kuwa nilikuwa peke yangu na nilihitaji kutengeneza maisha yangu mwenyewe," alisema.

Kuna wakati alituma nyumbani kama €2,000 ($2,200; £1,700) kwaajili ya dharura ya kifamilia wakati alipokuwa mwanafunzi na akifanya kazi kwa masaa machache.

"Kuna haja ya kuwa na usawa kati ya kubeba jukumu hili la kifedha na hali yako binafsi ya kifedha," aliiambia BBC.

Watu wengi wamegundua kuwa wanafamilia wanaweza kuhisi kuwa wana haki ya kupata fedha zako hususan pale muhusika anapokuwa tajiri.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, John Obi Mikel

Hili lilimkasirisha sana mchezaji mpira wa zamani wa Nigeria Mikel John Obi. Mwaka jana, alizungumza kuhusu "kodi ya watu weusi" pale alipohudhuria kipindi cha radio kinachojulikana kama Rio Ferdinand Presents.

"Unapotoka Afrika, unapopata fedha, hizo sio fedha zako. Sio fedha zako tu. Una watu wote hawa , iwe ndugu, jamaa, binamu, vyovyote vile utakavyowaita,” alisema.

Aliongeza kuwa ndugu zake waliendelea kuwa na watoto wengi, wakitarajia yeye awatunze.

Ingawa sio kila mtu alikubaliana na maneno ya Elsa Majimbo, lakini inaonekana kuwa yamegusa hisia za watu wengi, haswa miongoni mwa kizazi kipya.

Lakini Dk Dendere anasema kuwa “kodi ya watu weusi itaendelea kuwepo milele, hadi pale Afrika itakapoweza kujiendeleza yenyewe.”

Imetafsiriwa na Elizabeth Kazibure na kuhaririwa na Seif Abdalla