Kiapo cha utii kwa chama tawala kinachowadhibiti Wanyarwanda ughaibuni

Picha iliyonasa watu wakiwa ubalozi wa Rwanda nchini Uingereza wakila kiapo cha utii kwa chama tawala

Chanzo cha picha, YouTube

Picha zilizovuja za sherehe ya "kiapo" chenye utata katika ubalozi wa Rwanda huko London zimechochea madai ya ukandamizaji ulimwenguni dhidi ya wapinzani unaofanywa na 'serikali ya kimabavu' ya taifa hilo dogo la Afrika Mashariki, inayoitwa "Korea Kaskazini" mpya na wakosoaji wake.

Jamii ya Wanyarwanda waishio ughaibuni wameiambia BBC kuwa sherehe kama hizo zimekuwepo ili kuweka mazingira ya hofu na utii.

Mtu mmoja alisema jamaa zake huko Rwanda walitekwa nyara na labda waliuawa ili kumuadhibu kwa kukataa kutoa ushirikiano. Mamlaka ya Rwanda imepuuzilia mbali madai hayo kuwa ni ya uongo na hayana uthibitisho.

Katika picha ya video, iliyosambaa kwa Whatsapp, zaidi ya watu 30 walikuwa wanaonekana wamesimama kwenye chumba cha mikutano kilichojaa watu kwenye ubalozi wa Rwanda nchini Uingereza, wakiwa wamenyoosha mikono yao na kuapa utii kwa chama tawala , Rwandan Patiotric Front (RPF).

"Ikiwa nitakusaliti au kujitenga na mipango na dhamira ya RPF, nitakuwa nimewasaliti Wanyarwanda wote na lazima niadhibiwe kwa kunyongwa," lilisema kundi hilo kwa lugha ya Kinyarwanda, huku pia wakiahidi kupambana na "maadui wa Rwanda, popote watakapokuwa".

RPF kutumia ubalozi-ambao jijini London ni karibu na kituo cha Marylebone- kwa ajili ya ahadi kubwa ya kisiasa, yenyewe ni jambo muhimu.

'Wana hofu'

Lakini, wakati baadhi ya waliohudhuria sherehe hiyo - inayofahamika kuwa ilifanyika mnamo 2017 - inawezekana walikuwa wafuasi wa kweli wa chama tawala, ambao sasa wanaishi nje ya nchi, wengine wameiambia BBC kwamba wahudhuriaji wengi walikuwa huko kwa kushinikizwa.

David Himbara
BBC
"This is what happens everywhere. It's routine. Either you take [the oath] or you are [the] enemy. It is black and white"
David Himbara
Ex-adviser to President Kagame
1px transparent line

"Nina uhakika watu wengi waliokula kiapo hicho hawakuamini. Tulikuwa tunadanganya kulindana na familia zetu zilizo nchini Rwanda," alisema mtu mmoja ambaye- kwa mujibu wa uchunguzi wetu alikuwepo kwenye sherehe, lakini alitutaka tusiweke wazi jina lake akihofia kuadhibiwa.

"Hiki ndicho kinachotokea kila mahali. Ni kawaida. Ule kiapo au uwe adui. Jambo liko wazi namna hiyo," alisema David Himbara, ambaye aliwahi kuwa mshauri wa juu wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame.

Ni raia wa Canada, mwanataaluma na mwanaharakati ambaye amesema maisha yake yamekuwa yakitishiwa mara kwa mara na maafisa wa usalama wa Rwanda.

" Wengi huenda kwasababu wana hofu. Wanafikiri kuwa ikiwa hawatakwenda, jambo litatokea kwa familia zao (nchini Rwanda),'' alisema Rene Mugenzi, mwanaharakati wa haki za binadamu Uingereza na Rwanda ambaye hivi karibuni alishtakiwa kwa wizi nchini Uingereza na kufungwa

"Unapaswa kuwa na bidii ( ndani ya RPF) ukiwa huoneshi kuegemea upande wowote..wasikuhisi kuwa unaunga mkono makundi ya upinzani," alisema.

Alipoulizwa kuhusu sherehe ya "kiapo", ubalozi wa Rwanda ulijibu, kwa barua pepe, kuwa Wanyarwanda waishio nje walitumia chumba chake cha mkutano kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kitamaduni na kuwa kushiriki katika kiapo cha utii kwa RPF ni jambo halali na " ni uchaguzi wao na hakuna anayelazimishwa kufanya hivyo''.

'Kaka zangu walitekwa'

Lakini BBC imesikia ushahidi mpya kuwa serikali ya Rwanda imekuwa si tu ikiwatishia Wanyarwanda waishio ughaibuni, lakini pia wamekuwa wakitafuta kuwaadhibu watu hao kwa kuwalenga jamaa zao ambao wanaishi nchini Rwanda.

Jean Nsengimana (kushoto) and Antonine Zihabamwe (kulia) ambao wamepotea kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa

Chanzo cha picha, Noel Zihabamwe

"Ili kunitisha, waliwateka kaka zangu wawili. Hawakuwahi kujihusisha na siasa. Walikuwa kwenye ardhi ya Rwanda. Kwanini walipe gharama kwa kutofanya kosa lolote?" aliuliza kwa hisia kali Noel Zihabamwe, akiwa kwenye makazi yake Australia.

Bw. Zihabamwe ni mwanachama wa jumuia ya Wanyarwanda waishio nje huko Sydney, aliyeingia kama mkimbizi mwaka 2006, akitafuta kukimbia kile alichokiona kuwa ongezeko la hali ya ukandamizaji kisiasa.

Amesema kukataa kwake kuunga mkoni serikali ya RPF kulisababisha tishio la kuuawa kutoka kwa mwanadiplomasia wa Rwanda aliyetembelea Australia mwishoni mwa mwaka 2017, tukio ambalo aliliripoti kwa mamlaka za Australia

Noel Zihabamwe
Noel Zihabamwe
They often use this kind of kidnapping or murdering family members. This has to stop. We have had enough"
Noel Zihabamwe
A Rwandan living in Australia
1px transparent line

Hilo lilifuatiwa na kinachodaiwa kuwa kutekwa kwa kaka zake wawili, Jean Nsengimana na Antonine Zihabamwe, ambao waliripotiwa kuchukuliwa na polisi kwenye basi karibu na mji wa Karangazi nchini Rwanda Septemba mwaka 2019 na hawakuonekana tena.

"Mara nyingi hutumia aina hii ya utekaji nyara au kuua wanafamilia. Hii inapaswa kuachwa. Tumevumilia vya kutosha," Bw Zihabamwe alisema.

"Tungependa kuona serikali ya Rwanda inarejesha haki ya kidemokrasia kwa raia wote, kuacha mauaji, utekaji nyara, kukamata kinyume cha sheria na kampeni za kutishia raia wa zamani, kama mimi ambao wanaishi ughaibuni," aliongeza Zihabamwe, ambaye sasa anaamini kaka zake pengine walikufa na ameamua kuzungumza mbele ya hadhara, mbali na kile anachoona hatari kwake na familia yake

"Kwanini hawawezi kuifahamisha familia miili yao ilipo, ili tuandae mazishi rasmi? Kuna Wanyarwanda wengi nje ambao wamewapoteza wapendwa wao.

"Nataka kuzungumza dhidi ya ukosefu wa haki. Tunataka utawala unaoweza kumtetea kila mtu, si baadhi ya watu," aliiambia BBC.

'Shutuma hazina msingi'

Ubalozi wa Rwanda jijini London umetupilia mbali shutuma za Zihabamwe na kuziita kuwa uongo''wa kichovu unaojirudia'' na mpango wanasiasa wa upinzani wanaotaka kuzungumziwa na vyombo vya habari".

Lakini madai kama haya yanachukuliwa kuwa ya kuaminika na watafiti wengi, vikundi vya haki za binadamu na wanadiplomasia wa kigeni, ambao wanasema mamlaka za Rwanda zinaonekana kuwa zimetenda hayo - licha ya kuchochea ukosoaji kutoka kwa serikali za Magharibi - hatua kama hizo, ambazo zimejumuisha mauaji kadhaa nje ya nchi, kamwe hayakuonekana kusababisha athari zozote za muda mrefu za uhusiano wa kimataifa wa Rwanda.

Serikali ya Rwanda imepokea sifa na msaada wa kifedha ulimwenguni, kwa miongo kadhaa, kwa ajenda yake ya maendeleo yenye mafanikio, ambayo imesaidia kupambana na umasikini na kuibadilisha Rwanda kuwa moja ya nchi zenye uchumi wa kuvutia zaidi barani.

"Maoni yao ni - tunaweza kufanya kile tunachopenda, kuua ambao tunapenda," kilisema chanzo kimoja, kikizungumza kwa sharti la kutotajwa jina.

Kesi ya mtu, iliyofahamika kimataifa - hadithi yake iligeuzwa kuwa filamu ya Hollywood Hotel Rwanda - kwa ajili ya kuwalinda watu kutokana na mauaji ya kimbari ya 1994, ilivutia ukosoaji wa ulimwenguni mapema mwaka huu baada ya kuhamasishwa kurudi nchini kukabiliwa na mashtaka ya ugaidi.

Kifo cha mwanzoni mwa mwaka huu, chini ya ulinzi wa polisi, cha mwimbaji maarufu wa injili Kizito Mihigo pia kilichochea hasira kubwa.

Kizito Mihigo

Chanzo cha picha, Kizito Mihigo/Facebook

Kizito, kama alivyojulikana sana, alikuwa amejaribu kuvuka mpaka wa Rwanda kinyume cha sheria, viongozi walisema. Walisema alijiua mwenyewe - tukio ambalo linajadiliwa sana huko ughaibuni na wachambuzi wengi.

"Ikiwa wewe ni Mnyarwanda, ni salama kukaa kimya," alisema Sarah Jackson, naibu mkurugenzi wa Amnesty International Afrika Mashariki.

"Mamlaka ya Rwanda ina mbinu ambazo hutumia kukandamiza wapinzani nyumbani na nje ya nchi, kuanzia unyanyasaji hadi vitisho vya kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria, kutoweka, kuteswa, na hata kuwarudisha wapinzani wa Rwanda kutoka nchi nyingine kurudi Rwanda bila kupitia taratibu za uhamishaji ... na kutishia wanafamilia pia. "

Ubalozi wa Rwanda huko London ilisema tuhuma hizo hazina msingi wowote, na zinaenezwa na "wapinzani wachache… ili kuharibu sifa na safari ya maendeleo ya Rwanda".

'Utawala wa kiimla'

Rais Kagame alipata 99% ya kura katika uchaguzi uliopita wa urais nchini Rwanda mnamo 2017.

Huko London, Abdulkarim Ali, afisa wa chama cha upinzani cha Rwanda National Congress, alisema: "Ama unakuwa mtiifu kwa RPF au… unakuwa adui wa nchi. Kwa kawaida tunailinganisha na Korea Kaskazini."

Huko Canada, Bwana Himbara alielezea itikadi ya serikali ya Rwanda kama moja ya "utawala wa kiimla - serikali ambayo inataka kudhibiti mambo yote ya watu wa Rwanda, hata huko ughaibuni".

Ubalozi wa Rwanda huko London ulisema lengo kuu la serikali ni kuwaondoa Wanyarwanda kutoka kwenye umasikini na kuunda maisha bora na fursa kwa wote.

"Lengo la ubalozi si kwa wapinzani wachache ambao mara kwa mara wanaeneza habari za uwongo ili kuharibu sifa na safari ya maendeleo ya Rwanda."