Willy Mutunga, Martha Karua kuishtaki Tanzania kwa kuwaweka kizuizini na kuwafukuza

Jaji Mkuu wa zamani wa Kenya Willy Mutunga, Wakili Martha Karua wamewasilisha kesi katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki dhidi ya serikali ya Tanzania, wakiishutumu kwa kuwaweka kizuizini kinyume cha sheria, kuwakatazwa kuingia Tanzania na kufukuzwa.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma & Dinah Gahamanyi

  1. Na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo yetu ya mubashara kwa leo, tukutane tena hapo kesho.

  2. Willy Mutunga, Martha Karua kuishtaki Tanzania kwa kuwaweka kizuizini na kuwafukuza

    g

    Jaji Mkuu wa zamani wa Kenya Dkt. Willy Mutunga, Wakili Mwandamizi Martha Karua na watu wnegine wanne wamefungua kesi katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) dhidi ya serikali ya Tanzania, wakiishutumu kwa kuwaweka kizuizini kinyume cha sheria, kukatazwa kuingia Tanzania na kufukuzwa.

    Kikundi hicho, ambacho pia kinajumuisha wanaharakati wengine wanne na watetezi wa haki za binadamu; Gloria Kimani, Lynn Ngugi, Hussein Khalid na Hanifa Adan, wanadai kuwa haki zao kama raia wa Afrika Mashariki zilikiukwa waziwazi walipozuiwa kuingia Tanzania kufuatilia kesi ya uhaini ya kiongozi wa upinzani Tundu Lissu.

    Sasa wanadai msamaha wa umma kutoka kwa serikali ya Tanzania, pamoja na fidia ya jumla na maalum kwa uchungu wa kiakili, madhara ya sifa, na gharama za usafiri walizopata wakati wa tatizo hilo.

    Walalamishi wanadai kuwa mnamo Mei 18-19, 2025, walizuiliwa bila maelezo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, walinyang'anywa pasipoti zao, na baadaye kurudishwa nchini Kenya.

    Wamebainisha kuwa walikuwa Tanzania kama sehemu ya ujumbe wa kimataifa wa waangalizi, wakikusudia kuhudhuria na kufuatilia kesi ya Lissu ambayo ilipangwa kuanza Mei 19.

    Katika ombi lao, kundi hilo linaishutumu Tanzania kwa kukiuka masharti mengi ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ikiwa ni pamoja na yale yanayohakikisha utawala wa sheria, utawala bora, uwazi, na haki ya vinatekelezwa kwa uhuru katika nchi wanachama.

    Kesi hiyo pia inadai kutengwa kwao kulidhoofisha ushiriki wa raia na kukiuka kanuni ya haki wazi, kwani walinyimwa fursa ya kufuatilia kesi za kisheria za umma zenye umuhimu wa kikanda.

    Kesi hiyo iliyowasilishwa kwa pamoja na walalamikaji wawili wa maslahi ya umma, Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki (EALS) na Umoja wa Wanasheria wa Afrika Pan African, inasema kuwa hatua za Tanzania haziendani na Ibara ya 6(d), 7(2), 76, 104, na 8(1)(c) ya Mkataba wa EAC na Itifaki ya Soko la Pamoja la EAC ya 2009.

    Walalamishi pia wanataka kuondolewa kwa nukuu za "kukataliwa kuingia" kutoka kwa pasipoti zao na amri ya mahakama inayoizuia Tanzania kutokana na ukiukaji zaidi wa harakati huru za raia wa Afrika Mashariki.

    Kesi hiyo inatarajiwa kuhamishiwa kwenye mahakama ya EAC mjini Arusha ambapo tarehe inatarajiwa kuwekwa na mahakama katika wiki zijazo kwa maelekezo.

    Unaweza pia kusoma:

  3. Albert Ojwang: Uchunguzi wa maiti waonyesha mwanablogi aliyefia rumande Kenya hakujiua

    g

    Chanzo cha picha, Mitandao ya kijamii

    Uchunguzi wa mwili uliofaywa dhidi ya mwili wa mwanablogi wa Kenya Albert Ojwang', aliyefariki akiwa kizuizini katika Kituo Kikuu cha Polisi umebaini kuwa alivamiwa na kupata majeraha mengi mwilini.

    Baada ya kukamilisha uchunguzi wa mwili wake Jumanne Mchunguzi mkuu mwili wa serikali Bernard Midia, alifichua kuwa Ojwang' hakujigonga ukutani kama ilivyoripotiwa awali katika ripoti ya polisi.

    "Tulipochunguza ... muundo wa jeraha, hasa kidonda cha kichwani .... inaonyesha kuwa alipigwa na kitu butu kama ukuta ," alisema.

    Midia alisema kwamba katika tukio la mtu kujigonga kwenye ukuta, damu ya mbele juu ya kichwa ingeonekana.

    "Lakini damu ambazo tulizipata kichwani…kwenye ngozi ya kichwa zilikuwa zimetengana, ikiwa ni pamoja na usoni, pande za kichwa, na nyuma ya kichwa," alieleza.

    Mchunguzi huyo wamwili, ambaye aliendesha mchakato huo pamoja na mwakilishi wa familia hiyo Mutuma Zambezi alipuuzilia mbali uwezekano wa Ojwang' kujijeruhi.

    Kifo cha Ojwang kilichotokea ndani ya kizuizi katika kituo cha polisi jijini Nairobi kimesababisha ghadhabu miongoni mwa wakenya wengu huku wakitaka wahusika wa kifo chake wachukuliwe hatua za kisheria.

    Mamia ya waandamanaji wakiwemo wanaharakati nchini kenya waliandamana kudai haki itendeke.

  4. Bellingham ajiunga na Dortmund kwa pauni milioni 27 kwa mkataba wa miaka mitano

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Jobe Bellingham alicheza mechi 43 akiwa na Sunderland msimu uliopita, akifunga mabao manne katika mashindano yote

    Jobe Bellingham amejiunga na Borussia Dortmund kutoka Sunderland kwa mkataba wa miaka mitano hadi Juni 2030.

    Sunderland wanasema ada hiyo ni rekodi ya klabu, inayoaminika kuwa euro 32m (£26.96m) pamoja na euro 5m (£4.2m) kama nyongeza.

    Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 19 amewachezea Paka Weusi tangu 2023, na kucheza mechi 90, akiwasaidia kupata fursa ya kupanda Ligi Kuu msimu uliopita.

    Bellingham alianza uchezaji wake katika klabu ya Birmingham City, akipitia shule ya soka kabla ya kuichezea klabu hiyo kwa miaka miwili ya soka la wachezaji wakubwa.

    Katika taarifa, Bellingham alisema anajivunia uhusiano "nguvu" alionao na wafuasi wa Sunderland.

    Kwa mkataba huo kukamilika ifikapo Juni 10, Bellingham anaweza kuichezea Dortmund kwenye Kombe la Dunia la Klabu, ambalo litaanza Jumapili.

    Bellingham ameitwa katika kikosi cha England kwa ajili ya michuano ya Ulaya ya Vijana chini ya miaka 21, itakayofanyika Slovakia kuanzia Juni 11-28.

    Lakini kocha mkuu Lee Carsley amesema atawaachilia wachezaji ili waweze kushiriki michuano ya Kombe la Dunia la Klabu nchini Marekani.

    Bellingham anafuata nyayo za kaka mkubwa Jude kwa kuhamia Bundesliga, kwani kiungo wa kati wa Uingereza - ambaye pia alipitia mfumo wa vijana wa Birmingham City - alitumia miaka mitatu na Dortmund kabla ya kujiunga na Real Madrid mnamo 2023.

    Soma zaidi:

  5. Jeshi la wanamaji la Israel lashambulia mji wa bandari wa Hudaydah unaodhibitiwa na Wahouthi

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Picha ya setilaiti ya bandari ya Hudaydah

    Meli za jeshi la wanamaji la Israel zimeshambulia maeneo ya bandari ya Hudaydah nchini Yemen inayodhibitiwa na Wahouthi.

    Jeshi la Israel limesema katika taarifa kwamba mashambulizi hayo yalifanywa kujibu makombora ya Wahouthi yaliyoilenga Israel na yalilenga kusitisha matumizi ya bandari hiyo kwa "malengo ya kijeshi".

    Hakukuwa na ripoti za mara moja za majeruhi.

    Picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha moshi mweusi ukipanda kutoka bandarini, huku Televisheni ya al-Masirah inayoongozwa na Wahouthi ikiripoti mahsmabulizi mawili tofauti tofauti.

    Waasi wa Kihouthi wamekuwa wakirusha makombora mara kwa mara huko Israel wakishirikiana na Wapalestina huko Gaza. Siku ya Alhamisi, kombora la Wahouthi liliangushwa juu ya Jerusalem, huku mwezi uliopita moja liliupiga uwanja wa ndege mkuu wa Israel.

    Mashambulizi ya Hudaydah, ambayo kwa njia isiyo ya kawaida yalitekelezwa na meli za jeshi la wanamaji badala ya ndege, yalifanywa alfajiri ya Jumanne asubuhi.

    Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) awali lilitoa onyo la kuhama kwa wale wote waliokuwepo katika bandari ya Hudaydah, pamoja na bandari nyingine zinazodhibitiwa na Wahouthi za Ras Isa na Salif.

    "Kutokana na utawala wa kigaidi wa Houthi kutumia bandari kwa shughuli zake za kigaidi, tunawaomba wote waliopo kwenye bandari hizi kuhama na kukaa mbali nazo kwa usalama wenu hadi taarifa nyingine," msemaji wa IDF wa lugha ya Kiarabu Avichay Adraee aliandika kwenye X.

    Soma zaidi:

  6. Spika wa Bunge la Uganda amuita Museveni 'Mungu' na Muhoozi 'mwana Mungu'

    k

    Chanzo cha picha, Ikulu ya Uganda

    Maelezo ya picha, Anita Among (kushoto) anafahamika kuwa mmoja wa wafuasi hodari wa utawala wa Rais Yoweri Museveni.

    Watu mbalimbali katika mitandao ya kijamii wametoa ujumbe wa kumlaani Spika wa Bunge la Uganda baada ya kusema kuwa Rais Yoweri Museveni ni Mungu na kumwita mwanae mwana wa Mungu.

    Siku ya Jumapili, Anita Among alikuwa akiwafanyia kampeni wabunge wa chama tawala cha NRM katika uchaguzi mkuu wa rais na wabunge uliopangwa kufanyika Januari (1) mwaka ujao.

    Hivi majuzi Anita alitangaza kuwa anataka kubaki katika nafasi yake kwa muhula mwingine kuanzia 2026–2031, ambao alisema utakuwa wa mwisho katika nafasi hiyo ambayo ameshikilia tangu 2022.

    Akiwa Kyazanga, kilomita 50 kusini mwa mji wa Masaka, Anita Among alipiga magoti na kuwaomba watu wa eneo hilo kuwapigia kura wabunge wa chama cha NRM aliowateua, akisema: "Napiga magoti, namuunga mkono Rais Museveni" na wagombea wa NRM. Kisha akasimama.

    Katika video hiyo iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii, Anita aliongeza: "Kama nilivyowaambia mara ya mwisho, sisi katika Teso [eneo lililo mashariki mwa Uganda] tunaamini Utatu Mtakatifu. Tunaamini katika Mungu Baba, na Mungu Baba ni Rais Museveni, [anarudia] Mungu Baba ni Rais Museveni. Mungu Mwana ni MK [Muhoozi Kainerugaba], sasa nyinyi mko katika Roho Mtakatifu, kwa hiyo muwachague.

    Gazeti la Daily Monitor la Uganda limeripoti kuwa kumtaja Rais Museveni kwa Mungu kumewakasirisha baadhi ya viongozi wa kidini wanaosema ni kufuru. Gazeti la Daily Monitor linaripoti kwamba bunge la Uganda limejibu kwa kusema kwamba matamshi ya Anita yalikuwa "mfano tu kwa madhumuni ya maelezo".

    Soma zaidi:

  7. Zelensky: Mashambulio ya leo ni mojawapo ya mapigo makubwa yaliyoipata Kyiv

    h

    Chanzo cha picha, t.me/Klymenko_MVS

    Maelezo ya picha, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ukraine amechapisha picha ya jengo la juu la Kyiv lililoharibiwa vibaya na shambulio la ndege isiyo na rubani

    "Mashambulizi ya Urusi ni makubwa zaidi kuliko majaribio ya Marekani na wengine ya kuilazimisha Urusi kurejesha amani," Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliyaita mashambulizi ya usiku dhidi ya Kyiv kupigwa na mojawapo ya mashambulizi mkubwa zaidi katika siku za hivi karibuni.

    Usiku wa Juni 10, wanajeshi wa Urusi walishambulia Ukraine kwa makombora 7 na drones 315.

    Kulingana na Jeshi la anga la Ukraine, ndege zisizo na rubani 284 hazikutekelezwa: "Ulinzi wa anga ulipunguza athari za mashambulizi ya ndege zisizo na rubani 284 ya adui, 220 zilipigwa kwa risasi na ilaha za moto, na 64 zilipotea."

    Kulingana na mkuu wa utawala wa kijeshi wa jiji la Kyiv, Timur Tkachenko, kazi ya vikosi vya ulinzi wa anga, "iliwezesha kupunguza hasara kwa kiwango cha chini."

    Kutokana na shambulio hilo huko Odessa, watu wawili waliuawa na zaidi ya watu 13 walijeruhiwa. Majengo ya makazi, jengo la hospitali ya uzazi, kituo cha ambulensi, kliniki ya matibabu ya kibinafsi, uwanja wa michezo, mbuga ya wanyama, na jengo la kituo cha reli viliharibiwa.

    Huko Kyiv, watu 4 walijeruhiwa, majengo ya makazi, kituo cha biashara, maghala na reli pia viliharibiwa.

    Zelensky alitoa wito kwa washirika kufanya kazi pamoja ili kujibu uchokozi wa Urusi: "Ni muhimu kwamba jibu la shambulio hili na mengine kama hayo ya Urusi kwa vitendo madhubuti.

    Unaweza pia kusoma:

  8. Habari za hivi punde, Austria: Watu kadhaa wauawa kwa kupigwa risasi shuleni

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wizara ya mambo ya ndani ya Austria inasema watu kadhaa wameuawa kwa kupigwa risasi katika shule ya upili ya Dreierschützengasse, kulingana na shirika la utangazaji la umma ORF.

    Tayari tunajua kwamba wanafunzi na walimu ni miongoni mwa waliopoteza maisha na kwamba mhalifu anaaminika kujipiga risasi kwenye choo cha shule.

    Kwa mujibu wa jarida la Kronen Zeitung watu wanane wameuawa katika shambulio hilo, ingawa maelezo hayajathibitishwa rasmi.

  9. Wafanyakazi wanne hawajulikani walipo baada ya meli kushika moto

    .

    Chanzo cha picha, Indian Coast Guard

    Walinzi wa Pwani wa India wanaendelea na juhudi za kuzima moto kwenye meli ya mizigo iliyokuwa na bendera ya Singapore katika Bahari ya Arabia karibu na pwani ya jimbo la kusini la Kerala.

    MV Wan Hai 503, iliyokuwa ikielekea Mumbai nchini India kutoka Colombo nchini Sri Lanka, iliripoti mlipuko wa ndani ya kontena siku ya Jumatatu, na kusababisha moto mkubwa.

    Wafanyakazi 18 wameokolewa, huku wanne wakiwa bado hawajulikani walipo. Singapore imetuma timu kusaidia katika juhudi za uokoaji.

    Kituo cha Kitaifa cha India cha Huduma za Taarifa za Bahari (INCOIS) kimetoa tahadhari kwa pwani ya Kerala kutokana na uwezekano wa kumwagika kwa mafuta na uchafu kutoka kwenye meli.

    Pia unaweza kusoma:

  10. UNFPA: Wengi wanasita kupata watoto kisa ukosefu wa fedha

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu UNFPA ameonya kuhusu kushuka kwa viwango vya watoto wanaozaliwa duniani akisema ulimwengu unashuhudia kuporomoka kwa idadi ya watu.

    Ripoti mpya ya UNFPA inasema watu wengi wanataka watoto wawili na zaidi lakini mamilioni ya watu duniani hawawezi kufikia matamanio yao ya kufanya hivyo.

    Uchunguzi uliohusisha watu elfu kumi na nne kutoka mataifa kumi na nne ulionesha kuwa matatizo ya kifedha na kukosa mwenza anayefaa kuwa sababu kuu za watu kusita kupata watoto.

    Mtu mmoja kati ya watano waliohojiwa wamesema bado hawajapata au hawatarajii kupata idadi ya watoto wanaotaka.

    Nchi zilizohusishwa katika utafiti huo ni Korea Kusini, Thailand, Italy, Hungary, Ujerumani, Sweden, Brazil, Mexico, Marekani, India, Indonesia, Morocco, Afrika Kusini na Nigeria ambazo zote kwa jumla zina theluthi moja ya idadi ya watu duniani.

    Waliohojiwa ni kutoka matabaka mbali mbali, wakiwemo vijana walio katika umri wa kuweza kuzaa au kuzalisha na waliopita umri wa kufanya hivyo.

    Mkuu wa UNFPA Dr Natalia Kanem amesema ulimwengu hivi sasa unashuhudia kushuka kwa kiwango cha kuzaliana kwa kiwango ambacho hakikutarajiwa kutokana na watu wengi kuhisi hawana uwezo wa kuanzisha familia wanazozitaka na kulitaja hilo kuwa tatizo linalotoa picha halisi ya mfumo wa familia duniani.

    Dr Kanem anaongeza kusema alishangazwa na idadi ya waliohojiwa ambao walisema wana watoto wachache kinyume na mapenzi yao.

    Katika mataifa yote 14 ambapo utafiti huu ulifanywa, asilimia 39 ya watu walisema ukosefu wa fedha au kuwa na uwezo mdogo kifedha ndiko kunawazuia wao kupata watoto.

    Korea Kusini ikiandikisha idadi kubwa zaidi ya wanaosita kupata watoto kwa asilimia 58 na Sweden ikiwa na kiwango kidogo cha wanaohisi fedha ni tatizo ikiwa ni asilimia 19 tu ya wanaohisi hivyo.

    Profesa Gietel Basten wa chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Hong Kong anasema kwa muda mrefu, shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani UNFPA, liliangazia pakubwa kuhusu wanawake walio na watoto wengi kuliko wanavyohitaji na mzigo mkubwa wa kuwashughulikia watoto wengi waliozaliwa bila ya kuwepo njia za mpango wa uzazi.

    Licha ya hayo, UNFPA inatahadharisha kuhusu namna ya kushughulikia uchunguzi huu wa hivi punde wa watu kuzaa watoto wachache au kutotaka watoto kabisa.

    Dr Kanem wa UNFPA anasema miaka arobaini iliyopita, China, Korea, Japan, Thailand na Uturuki zilikuwa na wasiwasi kuwa idadi ya watu wake iko juu mno lakini kuanzia mwaka 2015, mataifa hayo yameelekeza juhudi kutaka kuongeza idadi ya watu wake kwa kuhimiza watu kuzaa.

    Mbali na gharama ya kulea na kutunza watoto, kutopata mwenza anayestahili kuzaa naye, UNFPA pia imegundua kuwa kikwazo kingine cha kutokuwa na muda wa kuzaa na kulea.

    Soma zaidi:

  11. Ashtakiwa kwa madai ya kumtilia mwenzake dawa ya kutoa mimba

    .

    Chanzo cha picha, Parker County Sheriff's Office

    Mwanamume mmoja huko Texas ameshtakiwa kwa mauaji baada ya kudaiwa kuingiza dawa ya kutoa mimba kwenye kinywaji cha mpenzi wake mjamzito.

    Justin Anthony Banta alikamatwa siku ya Ijumaa baada ya uchunguzi wa miezi kadhaa kuhusu tuhuma za mpenzi wake wa zamani kwamba alimpa tembe ya Plan C (inayojulikana kama dawa ya kutoa mimba) bila yeye kujua, kulingana na polisi katika jimbo la Marekani.

    Mpenzi wa zamani wa Bw Banta alisema alipofichua ujauzito wake mwaka jana, alijitolea kulipia gharama ya kuavya mimba, lakini alionyesha nia yake ya kulea mtoto wake.

    Polisi walisema baada ya kukutana na Bw Banta katika mgahawa mmoja, alipata damu nyingi na kupelekwa katika chumba cha huduma za dharura, lakini akampoteza mtoto wake siku chache baadaye.

    Polisi walisema mpenzi wa zamani wa Bwana Banta alikuwa na ujauzito wa takriban wiki sita alipoenda kwa daktari wake, ambaye alimwambia mtoto alikuwa mwenye afya njema na "mapigo ya moyo" stahiki.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Korea Kusini: Mwanamke atozwa faini kwa kumvua suruali mwenzake wa kiume

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mahakama ya Korea Kusini imemtoza faini mwanamke mmoja kwa kosa la utovu wa nidhamu baada ya kumvua suruali mwenzake wa kiume – na kwa bahati mbaya, pia nguo yake ya ndani ikavuka mbele ya wenzao, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.

    Mbali na faini ya milioni 2.8 aliyotozwa ($2,100; £1,500), mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 50 pia ameamriwa kufanya mafunzo ya elimu ya kuzuia unyanyasaji wa kingono ya saa nane.

    Kisa hicho kinaripotiwa kutokea Oktoba mwaka jana katika mgahawa mmoja jimbo la Gangwon kaskazini-mashariki.

    Uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Chuncheon siku ya Jumamosi ulikataa madai ya mwanamke huyo kwamba alikusudia kufanya mzaha kwa mwenzake, ambaye yuko katika umri wa miaka 20.

  13. Urusi yaanzisha shambulizi "kubwa" la ndege zisizo na rubani Ukraine - maafisa

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Urusi imeanzisha shambulizi "kubwa" la ndege zisizo na rubani kwenye mji mkuu, Meya wa Kyiv Vitali Klitschko amesema, huku wodi ya wazazi huko Odesa pia ikilengwa.

    Shambulizi hilo huko Odesa lililenga vituo vya matibabu na majengo ya makazi, na kumuua mzee wa miaka 59 na kujeruhi wengine wanne, Gavana Oleg Kiper alisema kwenye mtandao wa Telegram.

    Katika mji mkuu, huduma za dharura zilihitajika katika wilaya nne saa chache baada ya usiku wa manane Jumanne, Klitschko alisema kwenye mtandao wa Telegraph.

    Mashambulizi ya hivi punde zaidi yanatokea baada ya shambulizi kubwa zaidi la ndege zisizo na rubani za Urusi dhidi ya Ukraine siku ya Jumatatu, ambalo Moscow ilisema ni hatua ya kulipiza kisasi kwa mashambulizi ya hivi majuzi ya Ukraine ndani ya Urusi.

    Baada ya Operesheni ya Ukraine iliyopewa jina ‘Spider Web’ kushambulia kambi za anga ndani ya Urusi tarehe 1 Juni, Rais wa Marekani Donald Trump alimpigia simu Vladimir Putin na kusema rais wa Urusi aliahidi kujibu "vikali" mashambulizi hayo.

    Meya wa Kyiv Vitali Klitschko amewaomba wakazi wa mji huo kusalia majumbani mwao.

    Walioshuhudia mashambulizi hayo wanasema kulikuwa na milipuko kadhaa na milio ya risasi.

    Shambulio hili linafuatia kuanza kwa mabadilishano ya wafungwa siku ya Jumatatu ambayo yatajumuisha wafungwa wa kivita wagonjwa na waliojeruhiwa vibaya, walio chini ya umri wa miaka 25 na miili ya wanajeshi 12,000 kurejeshwa.

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema mabadilishano hayo yatafanyika "katika hatua kadhaa", akielezea kama mchakato "ngumu" wenye "maelezo mengi nyeti".

    Rais wa Urusi Vladimir Putin alianzisha uvamizi dhidi ya Ukraine mnamo 2022.

    Soma zaidi:

  14. Wapalestina wafyatuliwa risasi na watu wenye silaha wa eneo na wanajeshi wa Israel

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wapalestina huko Gaza wanasema wamefukuzwa kwa mara nyingine tena walipokuwa wakielekea katika moja ya vituo vya kupokea misaada vinavyoendeshwa na Wakfu wa Kibinadamu wa Gaza unaoungwa mkono na Israel na Marekani siku ya Jumatatu.

    Mashahidi walisema kuwa kwa mara ya kwanza walifyatuliwa risasi na wapiganaji wa Kipalestina karibu na eneo la GHF la Tal al-Sultan kusini mwa Rafah.

    Pia walisema wanajeshi wa Israel waliwafyatulia risasi.

    Wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas ilisema watu sita waliuawa na 99 kujeruhiwa katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kupokea misaada.

    Jeshi la Israel limesema linachunguza ripoti hizo.

    GHF ilisema eneo la Tal al-Sultan halikufunguliwa Jumatatu na kwamba hakukutokea chochote katika maeneo mengine mawili ambayo yalitoa misaada.

    Haya yanajiri siku chache baada ya waziri mkuu wa Israel kukiri kuwa inazipa silaha koo za Wapalestina huko Gaza ambao walikuwa wakipinga Hamas.

    GHF, ambayo inatumia wanakandarasi binafsi wa usalama wa Marekani, inalenga kuukwepa Umoja wa Mataifa kama msambazaji mkuu wa misaada kwa Wapalestina.

    Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada yanakataa kushirikiana na mfumo huo mpya, wakisema unakiuka kanuni za kibinadamu za kutoegemea upande wowote, kutopendelea na kujitegemea.

    Marekani na Israel wanasema mfumo wa GHF utazuia misaada kuibiwa na Hamas, jambo ambalo kundi hilo linakanusha kufanya.

    Pia unaweza kusoma:

  15. Marekani: Wanajeshi wengine 2,000 kupelekwa Los Angeles

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Gavana wa California amesema amearifiwa kuwa wanajeshi elfu mbili zaidi watatumwa mjini Los Angeles kufuatia siku kadhaa za makabiliano kati ya waandamanaji na maafisa wa usalama kuhusu misako ya kuwakamata wahamiaji.

    Hilo limethibitishwa na utawala wa Trump.

    Msemaji mkuu wa Ikulu ya Marekani Sean Parnell amethibitisha kuwa walinzi wengine wanapelekwa mjini humo.

    "Kwa agizo la Rais, Idara ya Ulinzi inakusanya Walinzi wa Kitaifa wa ziada 2,000 wa California kuitwa katika huduma ya usalama ya taifa kuwezesha maafisa wa kutekeleza sheria kwa ajili ya udumishaji usalama," Parnell alisema.

    "Trump hatarudi nyuma", JD Vance amesema

    Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance alisisitiza kutumwa kwa wanajeshi kukabiliana na maandamano ya kupinga uvamizi wa wahamiaji huko LA.

    "Utawala huu hautatishwa na uvunjaji sheria," Vance alisema. "Rais Trump hatarudi nyuma."

    Hata hivyo Gavana Gavin Newsom ameitaja hatua hiyo ya Trump kuwa ni kutimiza ndoto ya rais dikteta huku mwanasheria mkuu wa California akimshitaki Rais Trump kwa kutuma majeshi jimboni humo bila ya ridhaa ya Gavana.

    Soma zaidi:

  16. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara ikiwa ni tarehe 10/06/2025