Utafungwa maisha gerezani kwa kusema unashiriki mapenzi ya jinsia moja Uganda

Mswada uliopitishwa na bunge la Uganda ambao utawafanya watu wanaojitambulisha kuwa wapenzi wa jinsia moja kuwa wahalifu umezua hofu miongoni mwa jamii ya LGBTQ.
"Kuna ulaghai mwingi. Watu wanapokea simu ambazo 'usiponipa pesa, nitaripoti kwamba wewe unashiriki uhusiano wa jinsia moja," mwanaharakati aliambia BBC.
Watu binafsi wanaweza kukabiliwa na vifungo vya muda mrefu ikiwa mswada
huo utatiwa saini na Rais Yoweri Museveni kuwa sheria.
Uhusiano wa jinsia moja umeharamishwa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Lakini mswada wa Kupinga mapenzi ya jinsia moja unalenga kwenda mbali zaidi na kuwafanya watu kuwa wahalifu kwa msingi wa utambulisho wao wa kijinsia. Ilipitishwa kwa uungwaji mkono mkubwa katika bunge la Uganda Jumanne jioni.
Chini ya sheria iliyopendekezwa, marafiki, familia na wanajamii watakuwa na wajibu wa kuripoti watu walio katika mahusiano ya jinsia moja kwa mamlaka.
"Wapenzi wa jinsia moja wamelaghaiwa, kunyang'anywa pesa au hata kunaswa kwenye mitego kwa ajili ya mashambulizi dhidi ya makundi yao," mwanaharakati alisema.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Katika baadhi ya maeneo hata wasimamizi wa sheria wanatumia mazingira ya sasa kuwanyang'anya fedha watu wanaowatuhumu kuwa wapenzi wa jinsia moja. Hata baadhi ya familia zinaripoti watoto wao polisi."
Mswada huo sasa utawasilishwa kwa Rais Museveni ambaye anaweza kuchagua kutumia kura yake ya turufu - na kudumisha uhusiano mzuri na wafadhili na wawekezaji wa Magharibi - au kutia saini kuwa sheria.
Ametoa kauli kadhaa dhidi ya wapenzi wa jinsia moja katika wiki za hivi karibuni, na pia alikosoa nchi za Magharibi kwa kuweka shinikizo kwa Uganda juu ya suala hilo.
Mwanaharakati mwingine wa LGBTQ+ alishutumu serikali kwa kutumia mswada huo kuvuruga umma kutokana na kushindwa kwake kushughulikia baadhi ya matatizo yao ya kiuchumi.
"Wanajaribu kuibua masuala yanapinga wapenzi wa jinsia moja ili kugeuza mawazo kutoka kwa kile ambacho ni muhimu kwa Waganda kwa ujumla. Hakuna sababu kwa nini unapaswa kuwa na mswada unaowafanya watu kuwa na hatia ya kuwa na mahusiano ya watu wazima wa jinsia moja," Clare Byarugaba, Mwanaharakati wa Haki za LGBTQ+ Uganda aliiambia BBC.
Wanaounga mkono wa mswada huo wanasema wanajaribu kuwalinda watoto lakini Bi Byarugaba alisema: "Uwe unashiriki mapenzi ya jinsia moja au la, serikali na bunge wanapaswa kuanzisha sheria, au angalau kutekeleza sheria zilizopo zinazolinda watoto wote - wavulana, wasichana dhidi ya unajisi.Suala la kuwashirikisha watoto katika mahusiano ya jinsia moja halijathibitishwa, halina msingi, lina upendeleo."
Mswada huo unasemaje?

Chanzo cha picha, AFP
Toleo la mwisho bado halijachapishwa rasmi lakini vipengele vilivyojadiliwa bungeni ni pamoja na:
- Mtu anayepatikana na hatia ya kulea au kusafirisha watoto kwa madhumuni ya kuwashirikisha katika vitendo vya wapenzi wa jinsia moja anakabiliwa na kifungo cha maisha jela.
- Watu binafsi au taasisi zinazounga mkono au kufadhili shughuli au mashirika ya haki za LGBT, au kuchapisha, kutangaza na kusambaza nyenzo na fasihi za vyombo vya habari vinavyounga mkono wapenzi wa jinsia moja, pia watakabiliwa na mashtaka na kufungwa gerezani.
Kikundi cha wabunge wachache wa Uganda katika kamati inayochunguza mswada huo hawakukubaliana na msingi wake. Wanasema makosa ambayo inataka kuharamisha tayari yamejumuishwa katika Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya nchi.
Mnamo mwaka wa 2014, mahakama ya kikatiba ya Uganda ilibatilisha kitendo kingine ambacho kilikuwa kimeimarisha sheria dhidi ya jumuiya ya LGBT.
Ilijumuisha kuifanya kuwa haramu kukuza na kufadhili vikundi na shughuli za LGBT, na pia kusisitiza kwamba vitendo wapenzi wa jinsia moja vinapaswa kuadhibiwa kwa kifungo cha maisha, na ilishutumiwa sana na nchi za Magharibi.
Mahakama iliamua kwamba sheria hiyo ibatilishwe kwa sababu ilipitishwa na bunge bila idadi ya wabunge inayotakiwa.
Mahusiano ya watu wa jinsia moja yamepigwa marufuku katika nchi zipatazo 30 za Afrika, ambapo watu wengi wanashikilia maadili ya kihafidhina ya kidini na kijamii.















