Mkasa wa mafuta Mauritius: Je, mikasa ya meli kumwaga mafuta inaongezeka?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Peter Mwai
- Nafasi, BBC Reality Check
Mkasa wa hivi majuzi ambapo meli ilimwaga mafuta baharini katika visiwa vya Mauritius umefufua tena mjadala kuhusu hatari ya kusafirisha mafuta kupitia baharini.
Meli hiyo ya MV Wakashio inayosimamiwa na kampuni ya Japan ilikwama kwenye matumbawe karibu na visiwa vya Mauritius kwenye Bahari ya Hindi.
Inakadiriwa kwamba meli hiyo ilimwaga zaidi ya tani 1,000 za mafuta katika eneo la bahari ambalo ni muhimu sana kimazingira kwa utalii na viumbe wa baharini.
Mikasa ya mafuta kumwagika baharini inatokea sana?
Idadi ya ajali za meli zinazosababisha mafuta kumwagika baharini imekuwa ikishuka miaka inavyosonga, kwa mujibu wa Shirikisho la Wamiliki wa Meli za Kusafirisha Mafuta kuhusu Uchafuzi (ITOPF).
Katika miaka ya 1970, kulikuwa na ajali 80 kwa wastani zilizohusisha kumwagika kwa mafuta tani saba na zaidi. Idadi hii imeshuka hadi kuwa ajali sita kwa mwaka katika mwongo ulioanza mwaka 2010.
Hii ni licha ya ongezeko la mafuta yanayosafirishwa kupitia bahari.
Hatua hizi zilizopigwa katika kupunguza umwagikaji wa mafuta baharini, kwa mujibu wa Bi Naa Sackeyfio wa ITOPF, ni kutokana na kuwekwa kwa sheria kali pamoja na wamiliki na wahudumu wa meli kuimarisha viwango vya usalama.
Baadhi ya mikasa mibaya zaidi ya kumwagika kwa mafuta ilitokea kati ya 1978 na 1991. Kati ya mikasa mikubwa ya umwagikaji wa mafuta iliyotokea tangu 1970, ni asilimia 4 pekee kati ya hiyo ilitokea baada ya 2010.
Lakini kuna changamoto kubwa katika takwimu zilizopo kuhusu mikasa ya umwagikaji wa mafuta.

Takwimu zilizopo hazijaangazia mikasa ya umwagikaji mdogo wa mafuta (ambao ni wa chini ya tani saba). ITOPF wanasema mikasa hiyo huchangia takriban 80% ya mikasa yote ya umwagikaji mafuta baharini.
Shirikisho hilo linasema huwa vigumu sana kukusanya takwimu kuhusu mikasa hiyo na wakati mwingine maelezo yanapotolewa huwa ni kamilivu.
Shirika la uhifadhi wa mazingira la Greenpeace linasema mkasa wowote ule wa umwagikaji wa mafuta baharini, hata kiasi kiwe kidogo aje, unafaa kuzua wasiwasi kutokana na uharibifu unaotokea kwa mazingira.
"Hata mkasa mmoja pekee bado si jambo zuri. Kwa sasa, kuna mikasa mingi ya umwagikaji wa mafuta inayoendelea maeneo mbalimbali duniani," Tal Harris kutoka Greenpeace aliambia BBC.
Greenpeace walisema pia kwamba takwimu za ITOPF haziwezi kuaminika sana kwa kuwa hawanakili taarifa kuhusu meli zote zinazosafirisha mafuta, na hivyo huenda kuna baadhi ya ajali ambazo huwapita.
ITOPF wanasema takwimu zao huangazia sio tu meli maalum za kusafirisha mafuta, bali pia meli zinazobeba mafuta na mizigo mingine. MV Wakashio iliyomwaga mafuta Mauritius ilikuwa meli ya kubeba mizigo mseto.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mafuta yaliyomwagika ni kiasi gani?
Ni muhimu kukumbuka kwamba mikasa mikubwa zaidi ya umwagikaji wa maji baharini katika historia haikuhusisha meli.
Mwaka 1991, wanajeshi wa Iraq walipovamia Kuwaita walimwaga makusudi karibu mapipa milioni nane ya mafuta kwenye Ghuba ya Uajemi. Walifanya hivyo kujaribu kuzuia majeshi ya Marekani yasifike Kuwait.
Na mwaka 2010, kulikuwa na mkasa mkubwa baharini katika mtambo wa kuchimba mafuta baharini waDeepwater Horizon nchini Marekani. Kiasi kikubwa cha mafuta kilimwagika katika Ghuba ya Mexico.
In tonnes
287,000 Atlantic Empress off Tobago in 1979
260,000 ABT Summer off Angola (1991)
252,000 Castillo De Bellver off South Africa (1983)
223,000Amoco Cadiz off France (1978)
"Ni muhimu kutambua kwamba kiasi cha mafuta ambacho kilimwagika kutoka kwenye meli miaka ya zamani kinazidi mafuta yaliyomwagwa katika miaka yote ya mwongo uliopita kwa pamoja," ITOPF wanasema.
Mikasa michache mikubwa pia ndiyo huchangia sana mafuta yanayomwagika.
Kuanzia 2010 hadi 2019, kulikuwa na mikasa zaidi ya 60 iliyochangia tani 164,000 za mafuta kumwagika. Lakini mikasa 10 ndiyo iliyochangia asilimia 90 ya mafuta hayo yaliyomwagika.
Nini husababisha mikasa hii?
Kuanzia 1970 hadi 2019, nusu ya mikasa mikubwa ya umwagikaji wa mafuta ilikuwa kwenye bahari wazi meli ilipogongana na nyingine au kugonga kitu fulani au ikakwama.
Mikasa ya kugongana kwa meli ilitokea kwa kiwango kikubwa kwenye maziwa, mito au bandarini.
Ni idadi ndogo sana ya ajali zilitokea wakati wa meli kupakiwa mafuta au kutolewa mafuta au zilitokana na kuvunjika kwa sehemu ya meli iliyo chini ya maji, kuharibika kwa mitambo, moto au milipuko au uharibifu uliotokana na hali ya hewa.
Ingawa jumla ya mikasa inayosababisha mafuta kumwagika baharini imekuwa ikipungua, idadi ya mikasa inayotokana na meli kugongana imekwua ikiongezana (hili pengine likitokana na ongezeko la meli baharini).
Tangu 2010, 44% ya ajali zilizomwaga mafuta zaidi ya tani saba baharini zilitokana na kugongana kwa meli au meli kugonga kitu baharini. Kiwango hicho ni cha juu kuliko miongo ya awali.
Na uharibifu unaotokea?
Umwagikaji wowote wa mafuta baharini unaweza kusababisha madhara makubwa kwa mazingira, hata kiasi cha mafuta yanayomwagika kikiwa kidogo.
Kwa kuwa mafuta si mazito kuliko maji ya chumvi, huelea na kuwa kama tabaka juu ya bahari.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mafuta hayo yanayoelea hukwamilia kwenye manyoya na ngozi za viumbe wa baharini na ndege, na kuathiri uwezo wake kuzuia maji kufikia mwili na hilo huwafanya kuathiriwa na baridi.
Isitoshe, viumbe hawa huathiriwa na kemikali zilizo kwenye mafuta iwapo watayanywa.
Kiwango cha mafuta yaliyomwagika mara nyingi huwa sio kielekezi cha madhara yanayotokea.
Madhara hutegemea ni wapi mafuta yamemwagika na hali ya hewa au kiwango cha kuchafuka kwa bahari. Kadhalika, hutegemea muda unaopita kabla ya juhudi za kusafisha bahari na kuyaondoa mafuta baharini kuanza.
Baadhi ya miaka mikubwa ya umwagikaji wa mafuta iliyotokea ilitokea mbali sana na pwani na haikusababisha dharura kubwa. Mikasa mingine haikuwa mikubwa sana - kwa mfano mkasa wa meli ya Exxon Valdez uliotokea Alaska - uliosababisha madhara makubwa kutokana na eneo ulikotokea.
Umwagikaji wa karibuni wa meli ya MV Wakashio pwani ya Mauritius - ingawa si kiasi kikubwa cha mafuta kilimwagika - ulitokea karibu na maeneo ya uhifadhi wa viumbe wa baharini.
"Hata kiasi kidogo tu cha mafuta yakimwagika baharini yanaweza kusambaa sana na kusababisha madhara makubwa, hasa iwapo umwagikaji utatokea karibu na pwani na hali ya hewa ikiwa nzuri na pia katika maeneo ya uhifadhi wa viumbe wa baharini," anasema David Santillo, mwanasayansi katika Greenpeace.














