Gaza: Kwanini udondoshaji wa misaada kutokea angani unakosolewa?

DF

Chanzo cha picha, US CENTRAL COMMAND

Maelezo ya picha, Jeshi la Marekani limesema kudondosha misaada Gaza kwa ushirikiano na Jordan ni sehemu ya juhudi endelevu za kupeleka msaada zaidi huko Gaza
    • Author, Luis Barrucho
    • Nafasi, BBC

Marekani inasema ilidondosha vifurushi 36,000 kaskazini mwa Gaza siku ya Jumanne kwa ushirikiano na Jordan – operesheni ya pili ya pamoja katika siku za hivi karibuni.

Imejiri siku moja baada ya Shirika la Afya Ulimwenguni kusema watoto wanakufa kwa njaa kaskazini mwa Gaza, karibu Wapalestina 300,000 wanaishi na chakula kidogo au maji safi.

Lakini mkakati huo umezua mjadala mkubwa, huku mashirika ya kibinadamu yakisema mbinu hiyo haiwezi kukidhi mahitaji yanayoongezeka. Pia ni ishara ya kushindwa kwa juhudi za kupeleka misaada kupitia ardhini.

Malori ya misaada yamekuwa yakiingia kusini mwa Gaza kupitia kivuko cha Rafah kinachodhibitiwa na Misri na kivuko cha Kerem Shalom kinachodhibitiwa na Israel wakati wa vita kati ya Israel na Hamas.

Lakini upande wa kaskazini, ambao ulilengwa katika awamu ya kwanza ya mashambulizi ya ardhini ya Israel, kwa kiasi kikubwa haupokei msaada katika miezi ya hivi karibuni.

Tarehe 20 Februari, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilisema linasitisha utoaji wa chakula kaskazini mwa Gaza kwa sababu misafara yake ilikumbana na "machafuko na vurugu kutokana na kuporomoka kwa utawala wa sheria," ikiwa ni pamoja na uporaji na vurugu.

Alhamisi iliyopita, zaidi ya Wapalestina 100 waliuawa wakati umati wa watu ukikimbilia kufikia msafara wa misaada uliokuwa ukiendeshwa na wanakandarasi binafsi uliokuwa ukisindikizwa na majeshi ya Israel magharibi mwa mji wa Gaza.

Maafisa wa afya wa Palestina walisema makumi ya watu waliuawa wakati vikosi vya Israel vilipofyatua risasi. Jeshi la Israel lilisema wengi walikufa kutokana na mkanyagano au kukanyagwa na malori ya misaada.

Lilisema wanajeshi waliokuwa karibu na msafara wa misaada walifyatua risasi kwa watu waliowakaribia na ambao waliwaona kuwa tishio.

Jeshi la Israel lilianzisha kampeni ya anga na ardhini huko Gaza baada ya mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba, ambapo takribani watu 1,200 waliuawa na wengine 253 walichukuliwa mateka.

Zaidi ya watu 30,000 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas inasema.

Misaada Haitoshi

rfd

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Wapalestina waliokata tamaa wamekuwa wakiivamia misafara ya malori inayopeleka msaada wa chakula kaskazini mwa Gaza
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Zaidi ya operesheni 20 za kudondosha misaada Gaza zimefanyika wiki chache zilizopita kwa ushirikiano na jeshi la Israel, huku Ufaransa, Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri zikiongoza pamoja na Marekani na Jordan.

Mkazi mmoja wa Gaza, Ismail Mokbel, aliiambia BBC Arabic - vifurushi vya misaada vilivyoshuka siku ya Ijumaa vilijumuisha mboga za jamii ya kunde na baadhi ya mambo muhimu ya afya ya wanawake.

Mtu mwingine, Abu Youssef, alisema hakuweza kupata msaada ambao ulidondoshwa karibu na Hospitali ya al-Shifa katika Jiji la Gaza.

"Ghafla, tulipokuwa tukitazama juu angani, tuliona maparachuti ya msaada. Kwa hiyo tulibaki pale pale [tulipokuwa] hadi misaada ulipotua umbali wa mita 500 kutoka tulipo. Kulikuwa na watu wengi, lakini msaada ulikuwa mdogo, na hivyo hatukuweza kupata chochote."

Mokbel alisema hakuna misaada ya kutosha iliyodondoshwa ili kukidhi mahitaji ya kimsingi ya idadi kubwa ya watu katika eneo hilo.

"Wakati maelfu wakisubiri katika maeneo hayo, ni watu 10 hadi 20 ndio wanapata vitu, wengine wanarudi bila kitu. Kwa bahati mbaya, njia hii ya kudondosha sio njia inayofaa ya misaada," aliongeza.

"Gaza inahitaji njia ya ardhini na majini ili kupata msaada badala ya kufanya kwa njia hiyo, ambayo haikidhi mahitaji ya raia wote."

Gharama na kubahatisha

FD

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Mwanamke na mtoto wakiwa katikati ya mahema katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa Gaza

"Misaada kutoka angani ni ghali, hatari na kwa kawaida husababisha watu wasiofaa kupata msaada," Jan Egeland, katibu mkuu wa Baraza la Wakimbizi la Norway na mkuu wa zamani wa misaada ya Umoja wa Mataifa, aliiambia BBC baada ya kurejea kutoka ziara ya siku tatu Gaza.

Vifurushi vya kudondoshwa kwa ndege ni ghali mara saba ikilinganishwa na misaada inayotolewa ardhini kutokana na gharama zinazohusiana na ndege, mafuta na wafanyakazi, inasema WFP.

Mbali na hayo, ni kiasi kidogo tu kinaweza kutolewa kwa kila ndege, kwa kulinganisha na kile ambacho msafara wa malori unaweza kuleta, na uratibu muhimu wa ardhini unahitajika ndani ya eneo la utoaji, inasema WFP.

Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu pia inasisitiza umuhimu wa kudhibiti usambazaji ili kuzuia watu kuhatarisha maisha yao kwa kutumia vitu visivyofaa au visivyo salama.

"Kuwasilisha chakula na bila kusimamiwa kwa watu walio na utapiamlo na njaa kunaweza kusababisha hatari kubwa kwa maisha," shirika hilo lilionya katika Ripoti ya 2016 iliyochapishwa wakati misaada ikitupwa Syria wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Vifurushi kutoka angani vinaweza kutupwa kuanzia mita 300 hadi 5,600 (futi 985-18,370) katika maeneo yenye migogoro, na hivyo kuhakikisha ufungashaji imara ni muhimu ili vifurushi viweze kustahimili kutua ardhini, WFP inaongeza.

Kulingana na shirika hilo, ondondoshaji unapaswa kufanywa katika eneo kubwa na sio dogo, maeneo ya wazi yasiwe madogo kuliko uwanja wa mpira, na ndiyo maana udondoshaji mara nyingi umekuwa ukifanyika katika ufuo wa Gaza.

Hata hivyo, hilo wakati mwingine limesababisha misaada kuanguka baharini au kubebwa na upepo hadi Israel, kulingana na mashuhuda waliopo Gaza.

'Marekani inapaswa kuishinikiza Israel'

BV

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Wanajeshi wa kigeni wamedondosha misaada Gaza kutokea angani

Mkazi wa Gaza, Samir Abo Sabha aliiambia BBC, anaamini Marekani inapaswa kufanya zaidi na kuweka shinikizo kwa mshirika wake Israel kwa ajili ya kusitisha mapigano.

"Kama raia wa Gaza, tunachotaka ni Marekani kuishinikiza Israel kusitishaji mapigano na kuacha kuwapa Israel silaha na makombora."

Baadhi ya wafanyakazi wa misaada wameunga mkono wazo hili.

Wiki iliyopita, Scott Paul wa Oxfam America aliandika kwenye X: "Badala ya kudondosha misaada kiholela huko Gaza, Marekani inapaswa kupunguza mtiririko wa silaha kwa Israel ambazo hutumiwa katika mashambulizi ya kiholela, na kushinikiza kusitishwa mara moja mapigano na kuachiliwa kwa mateka na kuisisitiza Israel itekeleze wajibu wake wa kutoa misaada ya kibinadamu na upatikanaji wa huduma nyingine za kimsingi."

Melanie Wadi kutoka Medical Aid for Palestinians alisema Marekani, Uingereza na wengine wanapaswa "kuhakikisha Israel inafungua mara moja njia zote za kuingia Gaza kwa ajili ya misaada na wafanyakazi wa misaada kusaidia wale wanaohitaji."

Lakini kadiri mzozo unavyozidi kuongezeka, wengine wanasema chakula lazima kiwasilishwe kwa njia yoyote.

"Tunahitaji kupeleka chakula Gaza kwa njia yoyote tunayoweza," José Andrés, mpishi na mwanzilishi wa World Central Kitchen, ambayo imekuwa ikituma chakula Gaza, aliiambia ABC News.

"Sidhani kama tunapaswa kuikosoa Jordan na Marekani kuleta msaada kwa kutumia anga. Badala yake, tunapaswa kupongeza mpango wowote unaoleta chakula Gaza."

Rais Biden amesema Marekani itaongeza maradufu juhudi za kufungua ukanda wa baharini, na kupanua usafirishaji kwa njia ya nchi kavu - lakini juhudi hizo bado hazijafanikiwa.

Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel, Admiral Daniel Hagari alisema Jumapili, walikuwa wakiwezesha misafara ya misaada ya anga kuelekea kaskazini mwa Gaza "kwa sababu tunataka msaada wa kibinadamu kuwafikia raia wa Gaza wanaohitaji."

"Tutaendelea kupanua juhudi zetu za kibinadamu kwa wakazi wa Gaza huku tukitimiza malengo yetu ya kuwakomboa mateka wetu kutoka kwa Hamas na kuikomboa Gaza kutoka kwa Hamas," aliongeza.

Pia Unaweza Kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi