UN yashutumu kuongezeka kwa ukandamizaji dhidi ya upinzani Uganda

Chanzo cha picha, Bobi Wine/X
Umoja wa Mataifa umeshutumu Jumatano kuongezeka kwa ukandamizaji dhidi ya upinzani na vyombo vya habari nchini Uganda kabla ya uchaguzi mkuu mwezi ujao, na kutaka uchunguzi ufanyike bila upendeleo kuhusu madai ya kukamatwa kiholela, kutoweka na "mateso".
Ofisi ya haki za Umoja wa Mataifa iliangazia "ripoti za kuaminika" zinazoonyesha kuwa takriban watu 550, wakiwemo wanachama na wafuasi wa chama kikuu cha upinzani cha National Unity Platform (NUP) na mgombea urais Bobi Wine, wamekamatwa na kuzuiliwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Zaidi ya 300 kati yao walikuwa wamekamatwa tangu kampeni za uchaguzi zilipoanza mwezi Septemba kabla ya kura ya urais ya Januari 15.
"Wengi wa waliokamatwa wamesalia rumande, wakikabiliwa na mashtaka kuanzia kero ya umma na kutotii amri hadi kushambulia, kuzuia na kuchochea vurugu," ilisema taarifa ya tume ya umoja wa mataifa ya haki za binadamu.
Ofisi ya tume hiyo pia ilionyesha jinsi vikosi vya usalama vilivyojihami vilikuwa vimetumwa katika maeneo ambayo NUP ilipanga kufanya mikutano.
"Pia wametumia mabomu ya machozi, mijeledi, marungu, maji ya kuwasha na virutubishi vya kemikali miongoni mwa silaha nyingine wakati wa maandamano ya kuwatawanya wafuasi wa NUP, na kujeruhi watu wengi," ilisema, ikiongeza kuwa wiki iliyopita pia waliripotiwa kutumia "risasi za moto" katika mkutano wa hadhara wa Bobi Wine mashariki mwa mji wa Iganga, ambapo angalau mtu mmoja aliuawa.
Inasikitisha sana kwamba kampeni za uchaguzi kwa mara nyingine tena zimekuwa na matukio mengi ya kukamatwa kiholela, kuwekwa kizuizini na matumizi ya nguvu zisizo za lazima dhidi ya upinzani," mkuu wa haki za Umoja wa Mataifa Volker Turk alisema katika taarifa hiyo. Huku akisisitiza "Ninaziomba mamlaka za Uganda kusitisha matumizi ya mbinu hizo za ukandamizaji."
Turk alitoa wito kwa mamlaka ya Uganda "kuchunguza kikamilifu na bila upendeleo" madai yote kama hayo, kuwaachilia wale "waliozuiliwa kiholela, na "kuadhibu wanaowajibika na kutoa fidia kamili kwa waathiriwa".
Taarifa ya Jumatano pia ilipinga vizuizi vya uhuru wa wanahabari, ikiangazia kesi za hivi majuzi ambapo wanahabari waliondolewa kibali chao kwa sababu ya ripoti muhimu.
Kwa mjibu wa ripoti hiyo ya tume ya umoja wa mataifa ya haki za binadamu- Makumi ya waandishi wa habari pia walivamiwa au kupokonywa vifaa vyao au kuharibiwa na maafisa wa usalama wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge katika eneo bunge la Kawempe Kaskazini mnamo mwezi Machi.
"Mamlaka za Uganda lazima zisitishe vurugu zote dhidi ya vyombo vya habari na upinzani na kuchukua hatua kikamilifu kulingana na wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu," Turk alisema.
Pia unaweza kusoma:
















