Rais Samia -Nguvu Iliyotumika Oktoba 29 ilistahili

s

Chanzo cha picha, Standard NP

Muda wa kusoma: Dakika 2

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametetea hatua zilizochukuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama wakati wa machafuko ya Oktoba 29, 2025, siku ambayo maandamano na mapambano baina ya waandamanaji na Polisi yaliripotiwa kusababisha vifo na majeruhi katika maeneo kadhaa nchini.

Akizungumza leo katika mkutano na wazee wa Dar es Salaam, Rais Samia alisema nguvu iliyotumika na vyombo vya dola ilikuwa ya lazima kulinda amani na kuzuia kile alichokitaja kama jaribio la kuvuruga utulivu wa nchi na mapinduzi.

"Nguvu inayotumika inaendana na tukio lililopo, tunapoambiwa kwamba tumetumia nguvu kubwa sana kwenye tukio lile, nguvu ndogo ilikuwa ipi?" ilikuwa tuwaangalie waandamanaji waliojiandaa kufanya mapinduzi mpaka wafanikiwe, hapo patakuwa na dola kweli? dola haiko hivyo"

Rais Samia alitupia lawama mataifa ya nje kushiriki kushawishi na kuchochea vurugu hizo. Alisema: "Mwanamke mzuri ndio anayepiganiwa", akionyesha mataifa ya nje yanaionea wivu Tanzania.

Who are you? (Nyie kina nani?), alihoji hayo mataifa ya kigeni yanayoingiza mkono wao Tanzania na kuchochea vurugu, Rais Samia: "kwao hayatokei", wanadhania wao ni wakoloni kwetu, ni kitu gani? ni fedha chache wanayotugaia?"

Aliongeza: "Wanaporudi kutulaumu kwamba tumetumia nguvu kubwa, wao walitaka nini, tujiulize Je hao ndiyo wafadhili wa kile kilichofanyika, walitaka tuangalie ile mob (kundi) mpaka lifanikiwe walichowapa fedha, walichowatuma, hapana!"

Anasema nguvu kubwa imekuwa ikitumika katika mataifa mengine duniani katika kuzuia aina ya maandamano na vurugu zilizotokea Tanzania wakati wa uchaguzi.

"Tulishashuhudia kwa wenzetu wandamanaji wengi wanaingia njiaani, na wakiingia njiani ikiona huu uandamanaji unakwenda pasipo wanaweka nguvu kubwa, yameshafanyika kwenye mataifa huko na tumeyaona".

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Alisema baadhi ya makundi yaliyoshiriki maandamano hayo yalikuwa na nia ya kusababisha mabadiliko ya kisiasa kupitia vurugu, akisisitiza kuwa dola haiwezi kutazama kimya katika mazingira ya namna hiyo.

Aliendelea kusema kuwa Tanzania imekumbwa na shinikizo kutoka nje kwa sababu ya rasilimali nyingi zilizopo nchini, zikiwemo madini adimu, ardhi yenye rutuba, mbuga za wanyama, maziwa na bahari, akitahadharisha kuwa Watanzania wasikubali kushawishiwa na watu wanaotafuta maslahi yao binafsi.

Kuhusu maandamano mengine yanayodaiwa kupangwa kufanyika Disemba 9, 2025 na wengine wakati wa sherehe za Chrismass, Rais alionya Serikali imejipanga.

"likija wakati wowote tumejipanga", akaongeza "tutasimama na kuilinda nchi hii kwa nguvu zote", alisema.

"Kama humpendi samia hakuna haja ya kuvuruga nchi".

Aidha kuhusu madai ya mabadiliko ya Katiba, alisema mchakato huo haujakataliwa na Serikali, na kwamba madai ya kisiasa yasitumike kama sababu ya kuvuruga nchi.

Rais Samia aliwataka Watanzania kuendeleza umoja na kulinda amani, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kulinda raia, mali zao na mipaka ya nchi.

"Yaliyopia si ndwele tugange yajayo".