Tanzania kwenye mzani wa nani 'beberu' nani mfadhili

S

Chanzo cha picha, URT

Muda wa kusoma: Dakika 6

Machafuko ya maandamano ya Oktoba 29 na mfululizo wa mijadala iliyofuata kuhusu chanzo cha vurugu hizo yamerejesha mjadala mkongwe: je, Tanzania bado inakabiliwa na mkono wa "mabeberu", au ni tahadhari za kisiasa zinazokinzana na uhalisia wa uhusiano wa nchi hiyo na wahisani wa kimataifa?

Katika siku zilizofuata maandamano hayo, mitandao ya kijamii, maafisa wa serikali, wachambuzi na wanasiasa walitupiana hoja nzito kuhusu nani hasa ananufaika na misukosuko ya kisiasa. Wakati serikali ilipoeleza kwamba mitandao ya "wafadhili waliovuka mipaka yao" ilihusika katika kufadhili baadhi ya shughuli za wanaharakati, wengine hasa waandishi wa habari na wachambuzi waliona tuhuma hizo kama ishara ya kutojifanya "kujichunguza" wenyewe kama taifa.

Akihutubia taifa kupitia wazee, Rais Samia Suluhu Hassan aliweka bayana vurugu za Oktoba 29, 2025 wakati na baada ya uchaguzi zina mkono wa 'mabeberu', akisema serikali haitakubali.

"Nje huko wanakaa ooh Tanzania ifanye moja ifanye mbili, halafu itakuwa hivi who are you? (nyie kina nani? alihoji.

Kauli ya Rais wa Uganda Yoweri Museveni ilizidisha utata, alipoeleza kuwa mataifa makubwa ya Ulaya "yanachochea machafuko Afrika Mashariki" ikiwemo Tanzania, kwa kuwaghilibu vijana ili kudhoofisha serikali zinazojaribu kujitegemea.

Alisema ghasia hizo ni sehemu ya "mashindano mapana kati ya uchumi unaoibuka wa viwanda barani Afrika na ushawishi wa Magharibi," na kuongeza kwamba "madola ya kigeni hayawezi kukubali Afrika yenye nguvu na inayojitegemea."

Lakini ndani ya Tanzania, wapo wanaosema hoja ya mabeberu inatumika kisiasa kupindukia, wakati mwingine kufunika majukumu ya ndani. Hoja hizi zimeipa makala hii msingi wa kuchunguza historia ndefu ya neno hilo, siasa za ufadhili, na namna mjadala huo unavyojitokeza tena Tanzania ikitafuta kusimama baada ya makovu ya Oktoba 29, 2025 kutokana na maandamano yaliyogharimu maisha ya watu, majeruhi na kuharibu kwa kiasi kikubwa mali za umma na binafsi.

1. Mabeberu ni nini? Tangu Nyerere hadi Samia

a

Chanzo cha picha, Ikulu

Katika Kamusi ya Kiswahili, "ubeberu" hufafanuliwa kama mfumo wa kimataifa wa kisiasa, kiuchumi na uzalishaji mali wa kiwango cha juu unaowezesha mataifa tajiri kuvuka mipaka na kunyonya rasilimali za nchi masikini. Katika mazoea ya siasa za Tanzania, neno hili limebeba mzigo wa kihistoria kutoka kwa Mwalimu Julius Nyerere, rais wa kwanza wa taifa hilo hadi marais wa leo.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa karibu miongo sita, marais wote wa Tanzania, kwa viwango tofauti, wamekuwa wakionya dhidi ya ushawishi wa nje. Kutoka kwa Nyerere aliyepinga ukoloni mamboleo, hadi kwa Hayati John Magufuli aliyelitumia neno hilo mara kwa mara katika mijadala ya madini, bandari na uwekezaji; na sasa hadi mijadala inayoibuka katika zama za Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika dhana ya ubeberu, kuna pia neno la "vibaraka" watu wanaotumika au wanaoonekana kutumika na masilahi ya mataifa makubwa yanayotajwa ya mabeberu. Bila kupepesa Mataifa haya sasna ni yale ya Magahribi na Marekani ambayo yamekuwa mstari wa mbele kufadhili ama kusaidia shughuli mbalimbali Tanzania.

Lakini kuna kundi linalokataa kabisa nadharia hiyo, wakisema mfumo wa uchumi wa dunia ni mpana na mgumu kuliko kudai kwamba kila changamoto ya Afrika imetengenezwa na mataifa ama watu kutoka nje. Kwao, hoja ya ubeberu hutumika kisiasa "kuumiza zaidi nchi masikini" kwa kuzuia uwajibikaji wa ndani.

2. Mstari mwembamba kati ya ubeberu na ufadhili

Hili ndilo eneo linalochochea mabishano makubwa zaidi hasa pale misaada, mikopo, au ufadhili wa mashirika ya kiraia unapogusa masuala ya demokrasia.

Serikali ya Tanzania, kama zilivyo serikali nyingi barani Afrika, hutegemea kwa kiwango fulani fedha kutoka nje. Kwa mfano katika bajeti ya 2024/25 yenye thamani ya shilingi trilioni 49, kiasi cha trilioni 5 kilitarajiwa kutoka nje kwa namna mbalimbali ikiwemo mikopo ya kibiashara, misaada ya maendeleo na mikopo nafuu. Kwa mantiki ya kiuchumi, hawa ni "washirika wa maendeleo." Lakini katika siasa, mara nyingi huitwa "mabeberu."

Utata huanza pale fedha hizo zinapofadhili shughuli za wananchi au makundi yanayotetea haki, uwajibikaji, au mageuzi ya kisiasa. Baada ya maandamano ya Oktoba 29, mitandao ilieneza madai kuwa taasisi kadhaa za Kimagharibi ikiwemo Ford Foundation, ya Marekani zilitoa mabilioni ya shilingi kufadhili "vurugu."

Katika hotuba yake, Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba alipowazungumzia wanaharakati wanaofadhiliwa, ingawa hakutaja mtu wala shirika alisema: "Juzi hivi wakati wa hizi vurugu, wakati wanatumiana meseji, tukazipata meseji. Kijana mmoja masikini tu juzi alikuwa anatuomba songesha, juzi kapewa dola milioni 2, takribani shilingi bilioni 4 kwenda 5. Za nini? Eti demokrasia. Unafanya demokrasia unapata hela nyingi hivyo kwa kuua watoto wa Kitanzania?"

Kauli hiyo iliwasha moto wa mjadala. Wachambuzi wengine walihoji ushahidi wa madai hayo, huku wengine wakisema ufadhili wa nje wa asasi za kiraia si jambo jipya wala la ajabu lakini unatakiwa kuwa na uwazi.

Mhariri wa Gazeti la Jamhuri, Manyerere Jackton, alitoa mtazamo mwingine akisema Tanzania inapaswa kujiangalia yenyewe. Alisema: "Bunduki zilishikwa na watanzania, maamuzi yalifanywa na taasisi zetu, mipango ilitoka kwenye mifumo yetu wenyewe."

Na akaongeza: "Mauaji, mateso, watu kutekwa na kupotea yamekuwa majeraha ya taifa letu bila kushinikizwa na taifa lolote kubwa."

Kwa upande mwingine, taasisi zinazotajwa kama Ford Foundation zimewahi kushutumiwa pia nchini Kenya kwa mada kama hizo, lakini pia zimechangia maendeleo makubwa ikiwemo kufadhili utafiti wa kilimo, elimu ya juu na miradi ya mahakama. Na mara zote imesimama ikisema lengo lake ni kuboresha hali za watu kwa kuhakikisha wanapata haki zao za msingi ikiwemo upande wa demokrasia na utawala bora.

Hakuna shaka kwamba nguvu za taasisi za kimataifa kama Benki ya dunia, Shirika la fedha duniani (IMF), lile la biashara (WTO) na n ahata Mahakama ya kimataifa ya uhalifu (ICC) zinaathiri dunia. Swali linabaki: je, beberu anaepukika?

3. Siasa za ubeberu na ubeberu wa siasa

Katika medani za siasa, neno "mabeberu" limekuwa silaha ya kisiasa. Humphrey Polepole, wakati akiwa Katibu Mwenezi wa CCM, aliwahi kumuita Tundu Lissu, kiongozi wa upinzani Tanzania "mwakilishi mkazi wa mabeberu nchini," akisema: "Tanzania ni nchi huru, inaamua mambo yake yenyewe, na vibaraka wa mabeberu hawatakuwa na chao." Hii ilikuwa wakati wa uchaguzi mkuu wa 2020. Lissu hakujibu moja kwa moja ila alitoa msimamo ule ule wa kwamba haw ani wafadhili na watu wanaosaidia haki Tanzania, si vinginevyo, hoja inayoupunguza zaidi mstari mwembamba ulipo kati ya mfadhili na beberu

Kada wa CCM Anthony Diallo, akiwa Mwenyekiti wa chama mkoani Mwanza, hakukubali na mtazamo wa mtu kukusaidia na ukamuita beberu. Alisema: "Kuita watu wanaokusaidia maendeleo mabeberu (sis awa) tulitumia huko miaka ya 1960… lakini leo mtu amekuja kukujengea shule unamuita beberu, si sawa." Hata hivyo akaonya dhidi ya "mikopo mibovu."

Wachumi kama Profesa Haji Semboja nao wamewahi kuhoji matumizi ya neno hilo, wakisema hawaoni "uwezo wa mataifa hayo kuangusha uchumi wa Tanzania," isipokuwa kwenye siasa ambapo "kuchafuana kunaweza kutokea."

Duniani kote, mifumo inayoendeshwa na mataifa tajiri yanayoitwa mataifa ya mabeberu inatawala: IMF, World Bank, G20, Umoja wa Mataifa. Kwa mtazamo wa kiuchumi, huwezi kuishi nje ya mfumo huu. Lakini kwa mtazamo wa kisiasa, unaweza kuukosoa kwa nguvu.

Nani tumuamini?

Kama ilivyo kwa nchi masikini Afrika, na kwingineko duniani, Tanzania iko katikati ya mifumo yenye nguvu duniani lakini pia iko katikati ya changamoto zake za ndani. Mstari unaotenganisha mfadhili, mshirika wa maendeleo na "mbeberu" ni mwembamba kiasi kwamba wakati mwingine huathiriwa zaidi na joto la siasa kuliko uhalisia wa uchumi.

Kwa muktadha wa kilichotokea Oktoba 29 kuna maswali manne ambayo kila utakayemuuliza huenda akaja na majibu haya. Je, kukuza demokrasia ni maendeleo? Ndiyo. Je, vurugu zinastahili kufadhiliwa? Hapana. Je, Tanzania inaweza kuikwepa mifumo ya kimataifa? Hapana. Na je, inaweza kujiboresha yenyewe? Ndiyo.

Katika mkutano wa IMF na Benki ya Dunia Oktoba 2025, nchi 14 za Afrika ikiwemo Tanzania ziliahidi kuongeza mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi wa misaada. Labda inaweza kusaidia kupunguza lakini bado mkakati huo una mkono wa IMF. Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Tanzania, Dkt. Natu Mwamba, alisema baada ya mkutano huo kwamba mipango hiyo inalenga "kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kupunguza utegemezi wa mikopo na misaada kutoka nje."

Kwa msingi huu mjadala huu wa mabeberu, ubeberu na vibaraka wa ubeberu, hauhusu tu nani ametoa fedha au nani amechochea vurugu bali unahusu mustakabali wa nchi inayojiuliza swali gumu: ni wakati gani mfadhili anageuka kuwa mbeberu na nani ndiye anayepima mizani hiyo?