Kwaheri hadi kesho
Na hapa ndio mwisho wa taarifa zetu za moja kwa moja, tukutane kesho.
Ndege ya Shirika la Ndege la Malaysia MH370 ilitoweka Machi 2014 ilipokuwa ikielekea Beijing kutoka Kuala Lumpur ikiwa na watu 239.
Na Asha Juma & Rashid Abdallah
Na hapa ndio mwisho wa taarifa zetu za moja kwa moja, tukutane kesho.

Chanzo cha picha, Reuters
Rwanda imetangaza rasmi mwisho wa mlipuko wa virusi vya Marburg, kufuatia siku 42 mfululizo bila kesi yoyote mpya, hatua ambayo inakidhi vigezo vya Shirika la Afya Duniani (WHO).
Mlipuko huo, uliotangazwa kwa mara ya kwanza tarehe 27 Septemba mwaka huu ulisababisha kesi 66 zilizothibitishwa, wengi wakiwa ni wafanyikazi wa afya, huku watu 15 wakiaga dunia na wengine 51 wakipona.
Kwa mujibu wa Wizara ya afya ya nchi hiyo, tangu tarehe 15 Octoba, Rwanda haijarekodi vifo vyovyote vinavyohusiana na Marburg wala kesi yoyote mpya ya ugonjwa huo.
Virusi vya Marburg ni ugonjwa unaoambukizwa sawa na Ebola. Dalili zake ni pamoja na homa, maumivu ya misuli, kuhara, kutapika, na katika hali mbaya kifo kinachosababishwa na kupoteza damu nyingi, na kwa sasa hakuna matibabu au chanjo zilizoidhinishwa za ugonjwa huo.
Katika kukabiliana na mlipuko huo, Rwanda ilianza kampeni ya chanjo tarehe 6 Oktoba, kwa kutumia chanjo ya majaribio iliyotengenezwa na Taasisi ya Sabin Vaccine ya nchini Marekani.
Taarifa zinasema, hatua kama vile upimaji, ufuatiliaji wa watu walioambukizwa, huduma za kimatibabu, na kampeni za elimu kwa umma, zilipunguza nusu ya idadi ya kesi mpya ndani ya wiki mbili na kuzipunguza kwa 90% muda mfupi baadaye.
Ili kuzuia kuibuka tena, Rwanda itaendelea na ufuatiliaji wa hali ya juu kwa angalau miezi sita.
Pia unaweza kusoma:

Spika wa Baraza la Wawakilishi la Liberia amekanusha kuhusika na moto mkubwa uliotokea katika bunge la taifa hilo la Afrika Magharibi.
Spika Jonathan Fonati Koffa alikuwa miongoni mwa waliohojiwa na polisi baada ya jengo la Bunge kuteketea kwa moto.
Hakuna mtu aliyekuwa kwenye jengo hilo wakati moto ulipotokea lakini serikali imeanzisha uchunguzi na kutoa zawadi ya dola za kimarekani 5,000 kwa yeyote aliye na taarifa za wahusika.
Koffa aliambia BBC alitumia jumla ya saa tisa katika kituo cha polisi kwa mahojiano, lakini anasisitiza alienda huko kwa hiari na hakuitwa.
Moto huo ulitokea Jumatano asubuhi - siku moja baada ya mipango ya kumwondoa Koffa katika nafasi yake, mpango uliozua maandamano makubwa.
Waandamanaji kadhaa, akiwemo msaidizi wa Rais wa zamani George Weah, walikamatwa wakati wa maandamano hayo.
Koffa ametoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi huru wa kimataifa kuhusu moto huo.
Baraza la Wawakilishi la Libeŕia limekumbwa na mzozo wa madaŕaka, ambapo kikundi cha wabunge kinataka kumuondoa Koffa kama spika na kuchukua nafasi yake.
Kundi jingine limepinga hatua hiyo, likisema ni kinyume cha katiba. Uamuzi wa Mahakama ya Juu umeshindwa kutatua mzozo huo.

Chanzo cha picha, Reuters
Polisi wanasema mtoto mmoja ameuawa na wengine kujeruhiwa katika tukio la kuchomwa kisu katika shule ya msingi nchini Croatia.
Waziri wa afya wa nchi hiyo anasema mwalimu mmoja pia amejeruhiwa katika shambulio la kisu huko Zagreb siku ya Ijumaa.
Polisi imeongeza kuwa mshambulizi amekamatwa katika eneo la tukio.
Waziri Mkuu wa Croatia Andrej Plenkovic amesema "ameshtushwa" na tukio hilo katika Shule ya Msingi ya Precko.

Chanzo cha picha, Getty Images
Walinzi wa pwani ya Ugiriki wanasema watu wanane wamekufa maji baada ya boti ya mwendo kasi iliyokuwa imebeba wahamiaji kujaribu kukwepa meli ya doria ya walinzi wa pwani katika Bahari ya Aegean.
Boti ya mwendo kasi ilipinduka, mlinzi wa pwani ya Ugiriki amesema, baada ya nahodha wa boti "kupoteza mwelekeo" katika jaribio la kuitoroka meli ya doria ya Ugiriki.
Boti hiyo ilikuwa ikisafiri kwa mwendo wa kasi na iligonga upande wa meli ya walinzi wa pwani ya Ugiriki ilipokuwa ikijaribu kutoroka, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Ugiriki.
Kufikia sasa watu 18 wameokolewa kutoka baharini, wanasema walinzi wa pwani, huku wengi wa walionusurika wakiwa na majeraha baada ya tukio hilo.
Tukio la Ijumaa lilitokea karibu na kisiwa cha Rhodes, ng'ambo ya pwani ya Uturuki, kwenye bahari ambayo mara nyingi hutumiwa na wasafirishaji haramu wa wahamiaji.
Meli na helikopta za walinzi wa pwani zinaendelea na msako wa kuwatafuta manusura zaidi.
Maelfu ya wahamiaji wanaojaribu kufika Ulaya hufa wakati wa safari za aina hiyo katika bahari ya Mediterania kila mwaka.
Mwezi uliopita miili ya watu wanane, wakiwemo watoto sita, ilipatikana baada ya mashua ya wahamiaji kuzama kwenye kisiwa cha Ugiriki cha Samos.
Hadi kufikia mwaka huu, zaidi ya wahamiaji 50,000 wamewasili Ugiriki kwa boti, na kuifanya kuwa nchi ya pili kwa wahamiaji wengi kupita kwenda Ulaya nyuma ya Italia.
Takwimu zinaonyesha takribani wahamiaji 180,000 wamewasili Ulaya kwa njia ya bahari mwaka huu, huku 2,000 wakiwa wamekufa au kutoweka. Karibu 23% ya waliofika walikuwa watoto.
Pia unaweza kusoma:

Chanzo cha picha, Getty Images
LeBron James amevunja rekodi ya kucheza dakika nyingi zaidi katika historia ya ligi ya mpira wa kikabu ya Marekani ya NBA, pale alipoisaidia timu yake ya Los Angeles Lakers kuwashinda Sacramento Kings.
Mmarekani huyo mwenye umri wa miaka 39 amempita Kareem Abdul-Jabbar alipomaliza dakika yake ya 57,447 katika uwanja kwa ushindi wa 113-100 siku ya Ijumaa.
James, ambaye amempita Abdul-Jabbar kwa rekodi ya ufungaji katika NBA mapema mwaka huu, alifunga pointi 19 katika mchezo huo.
"Ni kujitolea tu katika ufundi na kuwa na shauku na upendo nilionao kwa mchezo huu," amesema James.

Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Malaysia imekubali kuanza tena utafutaji wa ndege ya abiria ambayo ilitoweka miaka kumi iliyopita, mojawapo ya tukio lililoacha fumbo kubwa juu ya usafiri ya anga.
Ndege ya Shirika la Ndege la Malaysia MH370 ilitoweka Machi 2014 ilipokuwa ikielekea Beijing kutoka Kuala Lumpur ikiwa na watu 239.
Juhudi za kutafuta mabaki ya ndege hiyo aina ya Boeing 777 zimefanyika kwa miaka mingi na mamia ya familia za waliokuwa ndani ya ndege hiyo zimesalia na maswali bila majibu.
Siku ya Ijumaa, waziri wa uchukuzi wa Malaysia, Anthony Loke alisema baraza la mawaziri limeidhinisha mkataba wa dola za kimarekani milioni 70 kwa kampuni ya Marekani ya uchunguzi wa baharini ya Ocean Infinity kutafuta ndege hiyo.
Chini ya mkataba huo "usipoipata, hakuna malipo," Ocean Infinity italipwa pale tu mabaki ya ndege hiyo yatakapopatikana.
Utafutaji wa 2018 wa Ocean Infinity chini ya masharti kama hayo uliisha bila mafanikio baada ya miezi mitatu ya utafutaji.
Juhudi za kimataifa ambazo ziligharimu dola za kimarekani milioni 150 zilimalizika mwaka 2017 baada ya miaka miwili ya kutafuta.
Utafutaji mpya utashughulikia eneo la kilomita za mraba 15,000 kusini mwa Bahari ya Hindi.
Ndege MH370 ilipaa kutoka Kuala Lumpur mapema tarehe 8 Machi 2014. Ilipoteza mawasiliano chini ya saa moja baada ya kupaa na rada ilionyesha ilikengeuka kutoka njia yake iliyopangwa ya ndege.
Wachunguzi kwa ujumla wanakubali ndege hiyo ilianguka mahali fulani kusini mwa Bahari ya Hindi - ingawa haijulikani ni kwa nini ilianguka.
Pia unaweza kusoma:

Chanzo cha picha, Getty Images
Maisha ya Angelina Jolie ni ya faragha sana, lakini katika mahojiano mapya na BBC, nyota huyo wa Hollywood amezungumza kwa uwazi kuhusu uzoefu wake wa kufanya kazi pamoja na watoto wake wakubwa, akisema waliona "uchungu" ambao huwa anauwaficha.
Mwigizaji huyo anaigiza katika katika filamu mpya inayoitwa Maria, kuhusu mwimbaji wa opera, Maria Callas.
Watoto wawili kati ya sita wa Jolie na mume wa zamani Brad Pitt, Maddox na Pax, walichukua jukumu la kuwa watayarishaji wasaidizi wa filamu hiyo.
"Mhusika [Callas] anapitia maumivu makali sana na bila shaka (watoto wangu) wameniona nikipitia mambo mengi, lakini hawakuwahi kuniona nikipitia maumivu ambayo kwa kawaida mzazi humficha mtoto wake," amesema.
"Kwa hiyo walikuwepo kushuhudia baadhi ya hayo, lakini tulikumbatiana au walikuwa wakiniletea vikombe vya chai."
Filamu hiyo imeandikwa na muundaji wa tamthilia ya Peaky Blinders, Steven Knight, na inaangazia miaka ya mwisho ya Callas, katika miaka ya 1970, alipokuwa akiishi Paris.
Pia unaweza kusoma:

Chanzo cha picha, Getty Images
Jumla ya dola za kimarekani bilioni 2.2, fedha za mtandaoni zimeibiwa mwaka huu, huku wadukuzi wa Korea Kaskazini wakichukua zaidi ya nusu ya pesa hiyo, kulingana na utafiti.
Kampuni ya utafiti ya Chainalysis inasema wadukuzi wanaohusishwa na serikali wameiba dola bilioni 1.3 sarafu za kidijitali - mara mbili zaidi ya walivyoiba mwaka jana.
Ripoti inaeleza, sehemu ya wizi huo unahusishwa na wadukuzi wa Korea Kaskazini wanaojifanya kuwa wafanyakazi wa tehama ili kupenya kwenye makampuni ya sarafu za mtandaoni na teknolojia nyingine.
Ripoti hii inakuja wakati ambao thamani ya bitcoin imeongezeka zaidi ya mara mbili mwaka huu baada ya rais anayekuja wa Marekani Donald Trump kuonekana kuwa rafiki zaidi wa sarafu hizo kuliko mtangulizi wake, Joe Biden.
Ripoti inaeleza, kwa ujumla, kiasi cha fedha zilizoibiwa na wadukuzi mwaka 2024 kiliongezeka kwa 21% kutoka mwaka jana lakini bado kilikuwa chini ya viwango vilivyorekodiwa 2021 na 2022.
Serikali ya Marekani imesema utawala wa Korea Kaskazini unatumia fedha za wizi na aina nyingine za uhalifu mtandaoni ili kukwepa vikwazo vya kimataifa na kupata pesa.
Wiki iliyopita, mahakama ya shirikisho huko St Louis, Marekani iliwafungulia mashtaka raia 14 wa Korea Kaskazini kwa madai ya kuwa sehemu ya njama ya kupora fedha kutoka makampuni ya Marekani na kupeleka pesa hizo katika programu za silaha za Pyongyang.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pia ilitangaza itatoa zawadi ya hadi dola milioni 5 kwa yeyote atakayetoa maelezo zaidi kuhusu mpango huo.
Pia unaweza kusoma:

Chanzo cha picha, Reuters
Wanadiplomasia wa Marekani wako katika mji mkuu wa Syria Damascus ambako wanapanga kukutana na wawakilishi kutoka Hayat Tahrir al-Sham (HTS), kundi ambalo sasa linaongoza nchi hiyo lakini Washington bado inalitaja kama shirika la kigaidi.
Ziara hiyo inafuatia zile za wajumbe katika siku za hivi karibuni kutoka Umoja wa Mataifa na nchi nyingine zikiwemo Uingereza, Ufaransa na Ujerumani.
Hii ni mara ya kwanza kwa Marekani kuonekana rasmi kidiplomasia mjini Damascus katika zaidi ya muongo mmoja.
Ni ishara zaidi ya mabadiliko makubwa yanayoendelea nchini Syria tangu kuanguka kwa utawala wa Rais Bashar al-Assad zaidi ya wiki moja iliyopita, na kasi ya juhudi za Marekani na Ulaya, pia zinazoegemea nchi za Kiarabu, kujaribu kushawishi utawala wake unaoibukia.
"Watakuwa wakijadiliana moja kwa moja na watu wa Syria, ikiwa ni pamoja na wanachama wa mashirika ya kiraia, wanaharakati, wanachama wa jumuiya mbalimbali, na sauti nyingine za Syria kuhusu maono yao ya mustakabali wa nchi yao na jinsi Marekani inaweza kuwasaidia," taarifa ilisema.
Washington inaweka masharti kadhaa kabla ya kufikiria kuliondoa kundi hilo kwenye orodha ya makundi ya kigaidi - hatua muhimu ambayo inaweza kusaidia kurahisisha njia kuelekea kuondolewa kwa vikwazo ambao Damascus inahitaji sana.
Soma zaidi:

Chanzo cha picha, Reuters
Kaka yake Paul Pogba, kiungo wa zamani wa Manchester United, amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela, miaka miwili ikiwa imepunguzwa, baada ya kukutwa na hatia ya kujaribu kumnyang'anya kaka yake.
Mathias Pogba, ambaye pia alipigwa faini ya Euro 20,000 (£16,500), ataepuka kukaa jela na badala yake atatumikia mwaka mmoja uliosalia akiwa amevalia bangili ya kielektroniki.
Wanaume wengine watano walipatikana na hatia ya unyang'anyi na uhalifu mwingine, na kuhukumiwa kati ya miaka minne na minane katika mahakama ya Paris siku ya Alhamisi.
Paul Pogba, 31, alisema "alidanganywa na marafiki zake wa utotoni" ambao walimshikilia mtutu wa bunduki mnamo 2022 na kumtaka awape €13m (£10.8m). Alisema aliwalipa €100,000 (£82,600).
Wakili wa Mathias Pogba, Mbeko Tabula aliiambia RMC Sport hukumu hiyo ilikuwa "kali sana" na akaongeza "Nadhani tutakata rufaa".
Mwaka jana, Paul Pogba aliiambia Al Jazeera kwamba alikuwa amefikiria kustaafu soka kwa sababu ya jaribio la unyang'anyi.
Soma zaidi:

Chanzo cha picha, AFP
Malaria imetambuliwa kama sababu inayowezekana ya ugonjwa ambao umeua zaidi ya watu 80 kusini-magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, shirika kuu la afya la Afrika lilisema.
Waathiriwa wa ugonjwa ambao haukujulikana hapo awali walikuwa wakiugua dalili kama za mafua kama vile homa, maumivu ya kichwa, shida ya kupumua na anemia.
Sampuli nyingi ambazo zimejaribiwa zilionyesha kuwa wana malaria - ambayo husababishwa na vimelea vinavyobebwa na mbu na ni janga katika ukanda huo - huku utapiamlo ukiendelea kuzidisha hali hiyo kuwa mbaya zaidi.
Hata hivyo wataalam wa afya hawaondoi uwezekano wa sababi zingine katika eneo la afya la Panzi.
Wasiwasi kuhusu ugonjwa huo umeongezeka kufuatia kifo cha mgonjwa wa kiume aliyekuwa akionyesha dalili zinazohusiana na homa ya kuvuja damu.
Hii ilisababisha uvumi kuhusu uwezekano wa maambukizi ya virusi kuanzia wakati huo huo kama malaria, Dk Ngashi Ngongo, kutoka Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), aliwaambia waandishi wa habari siku ya Alhamisi.
Sampuli za mgonjwa aliyefariki zimetumwa katika mji mkuu wa Kongo, Kinshasa, kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi, huku matokeo yakitarajiwa ndani ya wiki ijayo.
Afrika CDC, Shirika la Afya Duniani la Umoja wa Mataifa, na mashirika mengine yanazidisha uchunguzi kuhusu mlipuko huo, huku majaribio zaidi yakiendelea.
Soma zaidi:

Chanzo cha picha, Getty Images
Tyson Fury na Oleksandr Usyk waangaliana ana kwa ana kwa kwa dakika 11 na sekunde 20 katika moja ya tukio la kipekee, pengine refu zaidi katika historia ya ndondi.
Briton Fury, 36, atakutana ulingoni kuwania taji la uzito wa juu la Usyk nchini Saudi Arabia Jumamosi.
Akizungumza katika mkutano wa wanahabari, Usyk alisema: "Mimi? [Niangalie kando?] Hapana."
Hakuna kati yao aliyekuwa na la kusema katika mkutano wa wanahabari wa Alhamisi, wote wakisisitiza muda wa mazungumzo umepita.
Fury na Usyk waliangaliana kwa ghadhabu na wote walikataa kuangalia kando.
Dakika chache baadaye, waandaaji walianza kupanga mpango wa kuwatenganisha wawili hao. Rais wa WBC Mauricio Sulaiman alikuwa wa kwanza kujaribu kuwashawishi, lakini hakuna mpiganaji aliyewatazama.
Kipande cha kadi na leso kiliwekwa kati yao.
Jasho lilimtiririka Fury huku wapiganaji hao wakianza kurushiana maneno.
"Ni wakati wa sungura sasa. Kuchinjwa. Kukatwa vipande vipande," Fury alimwambia Usyk.
"Usiogope," Usyk alijibu.
Mnamo mwezi Mei, Usyk mwenye umri wa miaka 37 alimshinda Fury na kuwa bingwa wa kwanza wa uzani wa juu bila kupingwa katika kipindi cha miaka 25.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanajeshi na wataalam wengine wa Korea Kaskazini waliotumwa Ukraine kusaidiana na vikosi vya Urusi vitani hawapaswi kudharauliwa, wamesema wanajeshi wa zamani.
Kulingana na ujasusi wa Korea Kusini, wengi wao ni wa kitengo cha wasomi wa Storm Corps, na "wana ari ya juu", lakini "hawana ufahamu wa vita vya kisasa".
Mwasi Lee Hyun Seung, alifundisha kikosi maalum cha Korea Kaskazini mapema miaka ya 2000 kabla ya kuasi mwaka 2014.
‘’Niliwafundisha sanaa ya kijeshi, jinsi ya kurusha visu na kutengeneza silaha kwa vipandikizi na vyombo vingine vya jikoni’’, amesema.
Lakini ingawa mafunzo ya kikosi cha Storm Corps ni ya hali ya juu zaidi kuliko yale ya vikosi vya kawaida vya Korea Kaskazini, wanajeshi hao hawapati chakula cha kutosha na isitoshe wana utapiamlo.
Haneul ambaye ni mwanajeshi wa zamani wa Korea Kaskazini, anachokumbuka zaidi kuhusu wakati wake katika jeshi la Korea Kaskazini ni njaa ya kila siku.
Alipoteza kilo 10 katika mwezi wake wa kwanza wa huduma, kwa sababu ya lishe ya mahindi na kabichi kila siku.
Miezi mitatu ya mafunzo, anasema karibu kikosi chake kizima kilikuwa na utapiamlo na walihitaji kupelekwa kwenye kituo cha matibabu ili kuongeza uzito.
Baadaye walipowekwa kama walinzi vitani kwenye mpaka na Korea Kusini, mchele ulichukua nafasi ya mahindi. Lakini ilipofika mabakuli yao, kiasi kikubwa ulikuwa ushaliwa na vitengo vya nyuma, na uliobaki mara nyingi ulikuwa na mchanga.
Haneul anasema kitengo chake kilikuwa miongoni mwa waliolishwa vyema zaidi, kama mbinu ya kuwazuia kuhamia Korea Kusini. Lakini ilishindikana kumzuia Haneul.
Mnamo mwaka wa 2012, alifunga safari ambayo iwapo angekamatwa adhabu yake ingekuwa kifo katika eneo lisilo na kijeshi (DMZ) - ukanda wa ardhi unaogawanya Kaskazini na Kusini.
Uzoefu wake na wa waasi wengine wa kijeshi unasaidia kutoa mwanga kuhusu hali ya maelfu ya wanajeshi wa Korea Kaskazini waliowekwa mstari wa mbele katika vita vya Urusi dhidi ya Ukraine.
Pyongyang imeripotiwa kutuma karibu wanajeshi 11,000 kusaidia vikosi vya Urusi kurudisha sehemu ya eneo lake la Kursk lililotekwa na Ukraine katika shambulio la majira ya joto.
Mapema wiki hii, Seoul, Washington na Kyiv walisema "idadi kubwa" ya wanajeshi hao sasa wameingia kwenye mapigano, na kuripoti majeruhi wa kwanza, huku maafisa wa Korea Kusini wakikadiria zaidi ya 100 tayari wameuawa na wengine kujeruhiwa. Takwimu hii haijathibitishwa.
Soma zaidi:

Chanzo cha picha, X
Kiongozi wa waasi nchini Syria, Ahmed al-Sharaa, ametupilia mbali mabishano ya mtandaoni kuhusu video zinazomuonyesha akimpa ishara msichana ili afunike nywele zake kabla ya kupiga naye picha wiki iliyopita.
Tukio hilo lilizua ukosoaji kutoka kwa wachambuzi wasio na misimamo mikali na wahafidhina huku kukiwa na uvumi kuhusu mwelekeo wa siku za usoni baada ya waasi kuingia madarakani.
Wanaopendelea mabadiliko waliona ombi hilo kutoka kwa mkuu wa kundi la waislamu wa Sunni Hayat Tahrir al-Sham (HTS) kama ishara kwamba anaweza kutaka kutekeleza mfumo wa Kiislamu nchini Syria baada ya kuongoza kupinduliwa kwa Bashar al-Assad, huku wahafidhina wenye misimamo mikali wakimkosoa kwa kukubali kupigwa picha na mwanamke huyo.
"Sikumlazimisha. Lakini ni uhuru wangu binafsi. Nataka nipigwe picha jinsi inavyonifaa," Sharaa alisema katika mahojiano na mwandishi wa BBC Jeremy Bowen .
Mwanamke huyo, Lea Kheirallah, pia amesema kwamba hakuona ubaya wowote wa ombi hilo.
Hata hivyo, tukio hilo lilionyesha baadhi ya matatizo ambayo kiongozi yeyote wa baadaye wa Syria anaweza kuwa nayo katika kuomba na kuunganisha nchi hiyo yenye dini tofauti.
Waislamu wa madhehebu ya Sunni ndio idadi kubwa ya watu, na waliobaki wamegawanyika kati ya Wakristo, Alawites, Druze na Ismailis.
Soma zaidi:

Chanzo cha picha, Wizara ya Ulinzi ya Norway
Wizara ya Ulinzi ya Poland imesema mfumo wa ulinzi wa anga wa NASAMS na wanajeshi 100 wa Norway wamewasili kama sehemu ya ujumbe wa NATO kulinda kituo cha anga cha Rzeszow karibu na mpaka wa Ukraine.
Ujumbe uliotumwa kwenye mtandao wa X ambao (zamani ulijulikana kama Twitter) ulisema kuwa Rzeszow, kituo kikuu cha usafirishaji ambacho nchi za Magharibi hutumia kutuma msaada wa kijeshi kwa Ukraine, pia kitalindwa na wapiganaji wa F-35.
Misheni hiyo inatarajiwa kudumu hadi kipindi cha Pasaka, idara ya jeshi la Poland ilisema.
Mfumo wa hali ya juu wa ulinzi wa anga wa Norway umewekwa kuzuia makombora yanayorushwa kwa umbali mdogo na wa kati katika hali zote za hali ya hewa.
Mfumo huo ulitengenezwa na kampuni ya Norway ya Kongsberg pamoja na kampuni ya Marekani ya Raytheon na tayari unatumiwa na jeshi la Ukraine.
Ukraine imekuwa ikitoa wito kwa washirika wake wa Magharibi kuangusha makombora na ndege zisizo na rubani za Urusi ikiwa zitaruka juu ya eneo la NATO (siku za nyuma zilipita juu ya anga ya Poland na Romania) au hata karibu na mipaka ya magharibi ya Ukraine.
Hata hivyo, maafisa wa NATO wamekuwa wakisema hilo haiwezekani.
Soma zaidi: