WHO yaidhinisha chanjo ya kwanza dhidi ya Ebola ambayo ni ya kwanza kutumika duniani

Ebola DRC

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Karibu watu 1800 wamefariki kutokana na Ebola nchini DRC katika kipindi cha mwaka mmoja uliyopita

Shirika la afya duniani, WHO imeidhinisha chanjo dhidi ya Ebola, chanjo ya kwanza kabisa duniani. Dawa hiyo inayoitwa Ervebo iliyotengenezwa na kampuni ya MERCK pharmaceuticals, ilikuwa ikitumika kwenye hatua za majaribio nchini Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo. lakini sasa WHO inasema kuna ushahidi tosha unaoonesha kuwa chanjo hiyo inafanya kazi.

Hii ni hatua moja kubwa. Inamaanisha kuwa dunia sasa ina dawa ya kwanza kabisa ya kuzuia Ebola. Kabla ya kuidhinishwa,dawa hiyo hupitia kwenye awamu mbalimbali kwenye masuala ya usalama wa dawa na umadhubuti.

Lakini chanjo hiyo imekuwa ikitumika tangu mwaka jana ili kupambana na milipuko miwili ya Ebola nchini DRC.

Serikali ya nchi hiyo iliomba ruhusa kutumia dawa hiyo wakati utafiti ukiendelea kufanyika. Na ushahidi uliokusanywa wakati huo ndio ulioshawishi mamlaka za udhibiti kuwa dawa hizo zilikuwa zikifaa kwa matumizi dhidi ya virusi vya Ebola.

Chanjo hiyo itapatikana sokoni kuanzia katikati ya mwaka ujao.

Awali data za shirika la afya duniani (WHO) zilionyesha kuwa chanjo ya Merck ilikuwa na ufanisi kwa kiwango cha asilimia 97.5 kwa wale waliopatiwa chanjo, ikilinganishwa na wale wasiochanjwa.

WHO inasema chanjo hii imethibitisha kuwa salama na yenye ufanisi dhidi ya Ebola, lakini majaribio zaidi yanahitajika kabla dawa haijapatiwa leseni.

chanjo

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mhudumu wa afya akitoa chanjo ya Ebola

Mvutano kuhusu dawa za chanjo

Mjadala ulipamba moto miezi kadhaa iliyopita kuhusu mapendekezo kuhusu kuanzishwa kwa chanjo ya pili kwa ajili ya kupambana na Ebola nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Waziri wa afya wa Drc, dokta Oly Ilunga, ambaye aliacha kazi baada ya kuvuliwa majukumu ya udhibiti wa virusi vya Ebola, alisema chanjo ya sasa ni pekee iliyothibitishwa kufaa, na mbunge wa upinzani amesema chanjo mpya haijafanyiwa majaribio , na amehofu kuwa watu nchini humo watatumika kama ''nguruwe wa Guinea''.

Wataalamu wa masuala ya afya wamesema chanjo ya pili ni salama na inaweza kuwa muhimu katika kupambana na virusi vinavyosambaa.

Mwezi Julai, Kamati ya dharura ya WHO ilisema ''inatambua upungufu wa dawa'' ya chanjo ya MERCK.

Dokta Josie Golding wa mfuko wa Wellcome, alisema inawezekana kusiwe na chanjo ya kutosha ya kupambana na mlipuko.

''Ikiwa ni hivyo, hali inaweza kuwa mbaya zaidi. Tuna imani kubwa kuwa kuna uhitaji wa haraka wa kuwa na chanjo ya pili iliyotengenezwa na Johnson and Johnson.''

Kwa kifupi ni kuwa, dawa za chanjo kwa sasa zinaweza kuwa zenye kufaa, lakini zisiwe msaada ikiwa mlipuko wa maradhi utaendelea.

Kampuni ya dawa ya Merck ilisema kuwa kuna chanjo ya kutosha kwa ajili ya watu 500,0000, na wako kwenye mchakato wa kutengeneza zaidi.

Wale wanaotaka kutumia chanjo ya Johnson & Johnson, walipendekeza kutumia kwa maeneo ambayo hayajakumbwa na Ebola, ili kuwachanja watu walio nje ya maeneo yalioathiriwa.

Unaweza pia kusoma