WHO yatangaza Ebola kuwa suala la dharura duniani

Chanzo cha picha, Getty Images
Shirika la afya duniani, WHO limetangaza ugonjwa wa Ebola nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuwa ni ''dharura ya kiafya inayohitaji jumuia ya kimataifa kuitazama''.
Hatua hiyo inaweza kuzifanya nchi tajiri zinazotoa msaada kutoa fedha zaidi kukabiliana na ugonjwa huo.
Lakini shirika hilo limesema hatari ya ugonjwa huo kusambaa nje ya Congo si kubwa.
Ugonjwa wa Ebola umesababisha vifo vya watu 1,600 nchini humo.
Juma hili ugonjwa ulibainika mjini Goma, kuliko na wakazi zaidi ya milioni moja.
''Sasa ni wakati wa kuchukua tahadhari, ''Mkuu wa WHO Adhanom Ghebreyesus amewaambia wana habari mjini Geneva siku ya Jumatano, siku ambayo hali ya dharura ilitangazwa.
Amesema amekubali mapendekezo yaliyotolewa kwamba kusiwe na zuio la watu kusafiri au kwa ajili ya kufanya biashara wala kuwapima abiria katika bandari au viwanja vya ndege.
Shirika la msalaba mwekundu limeunga mkono mapendekezo hayo.
''Ingawa haibadili ukweli wowote kwa waathirika na washirika wanaosaidia kupambana na Ebola, tuna matumaini kuwa itafanya jumuia ya kimataifa kulichukulia kwa uzito unaotakiwa.'' Taarifa ya shirika hilo ilieleza.

Chanzo cha picha, AFP
Hali ni mbaya kiasi gani nchini humo?
Mlipuko wa Ebola ni ugonjwa wa pili kwa ukubwa katika historia ya nchi hiyo, ulianza mwezi Agosti na inaathiri majimbo mawili nchini DRC, Kivu Kaskazini na Ituri.
Zaidi ya watu 2500 wameathiriwa na ugonjwa huo na theluthi mbili kati yao wamepoteza maisha.
Ilichukua siku 224 kwa idadi ya walioathirika kufika 1,000 , lakini ndani ya siku 71 zaidi idadi ilifika 2,000.
Watu takribani 12 huripotiwa kupata ugonjwa huo kila siku.
Kwanini ugonjwa huu haujadhibitiwa?
Wafanyakazi wa afya wamekua wakipata vikwazo vya kutoaminika na machafuko nchini humo.
Watu wengine hawawaamini watoa huduma za afya, hivyo hufanya watu wenye dalili za ugonjwa huo kukwepa matibabu, hali hii inawia vigumu kuzuia kuenea kwa virusi vya ebola.
Ingawa zaidi ya watu 1,300 wamepoteza maisha tangu mwezi Agosti, Shirika la misaada la Oxfam linasema linakutana na watu kila siku ambao hawaamini kama kuna virusi vya ebola.
Tangu mwezi Januari kulikua na matukio 198 ya mashambulizi dhidi ya vituo vya afya, na kusababisha majeruhi 58.
Shirika la afya duniani WHO, limesema kuwa hatari ya kusambaa zaidi si kubwa sana, lakini inawezekana ugonjwa huo kuingia nchi jirani.
Ebola ni nini?
◾Ebola ni ugonjwa unaoambukizwa na virusi ambapo aliyepata maambukizi hupata dalili za homa, uchovu, maumivu ya viungo na koo.
◾Kisha mgonjwa hutapika, kuharisha na kutoka damu.
◾Watu huambukizwa kwa njia ya kugusana, njia ya mdomo na pua, pia kwa njia ya damu, matapishi, kinyesi,majimaji ya kwenye mwili wa mtu mwenye Ebola
◾Wagonjwa hupoteza maisha kutokana na kupungukia maji mwilini na viungo kushindwa kufanya kazi.














