Uganda: Ng'ombe kupewa 'vyeti vya kuzaliwa'

Ngombe

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Ambia Hirsi
    • Nafasi, BBC Swahili

Ng'ombe wote nchini Ugandan wanatarajiwa kupewa vyeti vya kuzaliwa ili kufikia masharti ya kibiashara katika soko la Muungano wa Ulaya, EU.

Kwa mujibu wa Gazeti la Daily Monitor, Waziri wa kilimo, ufugaji na uvuvi Vincent Ssempijja amesema kuwa mataifa yanayokuza chakula kwa ajili ya soko la EU lazima yatoe stakabadhi inayo onesha bidhaa hiyo imetoka wapi.

Bw. Ssempijja aliongeza kuwa bidhaa kutoka Uganda zinashikiliwa au kupigwa marufuku Barani Ulaya.

"Wakulima watasajliliwa na bidhaa zao kupewa nambari maalum ili kurahisisha mchakato wa kibiashara kati nchi hiyo na mataifa mengine hasa yale ambayo ni wanachama wa Muungan wa Ulaya," alisema.

"Hatuwezi kunufaika katika masoko makubwa hadi wakulima wetu wasajiliwe ,"aliongeza.

Ng'ombe

Chanzo cha picha, Getty Images

Bw. Ssempijja amesema wakulima watasajiliwa kivyao na ng'ombe pia kupewa cheti cha kuzaliwa kwasababu waagizaji bidhaa za nyama wanahitaji nyama kutoka kwa ng'ombe waliona na miezi kati ya 15 hadi 24. Kwa hivyo tunauza bidhaa zetu kulingana na umri wao," alisema.

Kwa mujibu wa Bw. Ssempijja, kundi la washirikishi wa mpango huo kutoka Muungano wa Ulaya wanatarajiwa nchini Uganda mwezi Septemba mwaka huu ili kuhakikisha wakulima wanauza bidhaa zao katika soko la Ulaya wanafikia masharti hayo.

''Kando na kufahamu chanzo cha bidhaa wanazouziwa washirikishi hao pia wanataka kuhakikisha wakulima wananufaika moja kwa moja kutokana na biashara zao kwasababu wakati mwingine wanapujwa na wafanyibiashara walaghai.

Serilakali ya Uganda imetoa arifa kuwa haitafanya kazi na mkulima yeyote ambaye hata timiza masharti hayo.

Serikali pia imekanusha madai kuwa mpango huo unalenga kuwatoza wakulima ushuru wa zaida ambao uliondolewa Julai Mosi mwaka huu.

Taarifa iliyowasilishwa na Waziri mkuu, Dkt Ruhakana Rugunda,kwa niaba ya Rais Museveni ilisema Waganda wanahitaji kujitoa kimaso maso katika ushindani wa kibiashara ili kupenya katika soko la kimataifa.

Yoweri Museveni

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Rais wa Uganda,Yoweri Museveni

"Watu wanataka kujua chakula wanachonunua na kula kinatoka wapi, na kupata thamani fedha zao.Kuwasajili wakulima ndio jambo la muhimu zaidi na hatuwezi kupuuza masharti hayo kwasababu tutapoteza soko la kimataifa'', ilisema taarifa ya rais Museveni.

Kilimo ni sekta muhimu kwa uchumi wa Uganda na huchangia 25% ya pato jumla la taifa.

Sekta hiyo pia huchangia 70% ya ajira kwa taifa hilo na kuimarisha usalama wa chakula

Mapato yanayotokana sekta hiyo iliongezeka kwa 9.6% kati ya mwezi Julai mwaka 2018 na mwezi Machi mwaka 2019.

Rais Museveni amesema ongezeko hilo limechangiwa ongezeko la bidhaa zinazouzwa nje ya nchi hiyo kama vile kahawa, chai,mahindi,maharagwa na kuimarishwa kwa uwekezaji wa katika sekta hiyo.