Zaidi ya watu 2,000 wameripotiwa kuugua Ebola nchini DRC

Chanzo cha picha, EPA
Zaidi ya watu 2,000 wameripotiwa kuugua ugonjwa wa Ebola nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika kipindi cha miezi 10, maafisa wameeleza.
Theluthi mbili walikua kwenye hali mbaya zaidi, wizara ya afya imeeleza.
Mlipuko wa ebola ni wa pili kwa ukubwa nchini DRC,kukiwa na ripoti ya kutokea maambukizi mapya wiki za hivi karibuni.
Lakini wafanyakazi wa afya wamekua wakipata vikwazo vya kutoaminika na machafuko nchini humo.
Watu wengine hawawaamini watoa huduma za afya, hivyo hufanya watu wenye dalili za ugonjwa huo kukwepa matibabu, hali hii inawia vigumu kuzuia kuenea kwa virusi vya ebola.
Ingawa zaidi ya watu 1,300 wamepoteza maisha tangu mwezi Agosti, Shirika la misaada la Oxfam linasema linakutana na watu kila siku ambao hawaamini kama kuna virusi vya ebola.Mhariri wa BBC Africa Will Ross anaripoti.
Kati ya mwezi Januari na Mei kulikua na matukio 40 ya mashambulizi dhidi ya vituo vya afya, Hata hivyo machafuko yamepungua majuma ya hivi karibuni.
Shirika la afya duniani WHO, limesema kuwa hatari ya kusambaa zaidi si kubwa sana, lakini inawezekana ugonjwa huo kuingia nchi jirani.
Mlipuko wa ebola mara nyingi husambaa haraka na kuathiri idadi ndogo ya watu.
Ebola ni nini?
- Ebola ni ugonjwa unaoambukizwa na virusi ambapo aliyepata maambukizi hupata dalili za homa, uchovu, maumivu ya viungo na koo.
- Kisha mgonjwa hutapika, kuharisha na kutoka damu.
- Watu huambukizwa kwa njia ya kugusana, njia ya mdomo na pua, pia kwa njia ya damu, matapishi, kinyesi,majimaji ya kwenye mwili wa mtu mwenye Ebola
- Wagonjwa hupoteza maisha kutokana na kupungukia maji mwilini na viungo kushindwa kufanya kazi.












