Kwanini kuna mvutano kuhusu chanjo mpya dhidi ya Ebola?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mjadala unapamba moto kuhusu mapendekezo kuhusu kuanzishwa kwa chanjo ya pili kwa ajili ya kupambana na Ebola nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Waziri wa afya wa Drc, dokta Oly Ilunga, ambaye aliacha kazi baada ya kuvuliwa majukumu ya udhibiti wa virusi vya Ebola, amesema chanjo ya sasa ni pekee iliyothibitishwa kufaa, na mbunge wa upinzani amesema chanjo mpya haijafanyiwa majaribio , na amehofu kuwa watu nchini humo watatumika kama ''nguruwe wa Guinea''.
Wataalamu wa masuala ya afya wamesema chanjo ya pili ni salama na inaweza kuwa muhimu katika kupambana na virusi vinavyosambaa.
Masuala gani yanayogusiwa?
Imejaribiwa?
Imejaribiwa kwa watu 6,000 na ''imeonyesha kuwa salama,'' anasema profesa Peter Piot, mtaalamu wa masuala ya mapambano dhidi ya Ebola na Mkurugenzi wa shule ya masuala ya afya na dawa za kupambana na maradhi ya kitropiki jijini London ambayo ilishirikiana na Kampuni ya dawa ya Johnson& Johnson katika kutengeneza chanjo.
Tafiti zimeonyesha kuwa ingawa dawa iko kwenye ngazi ya majaribio na haijajaribiwa kwa wagonjwa wa Ebola, imeonyesha kufaa kwa kiasi kikubwa kwenye majaribio yaliyofanyika kwa nyani.
Njia pekee ya kufanya majaribio kwa binadamu ni kutumika katika mazingira ya ugonjwa huo, kwa kuwa haitakuwa salama kujaribu dawa kwa watu walioathirika na virusi.
Hii ni namna ambavyo chanjo ya kwanza- iliyotengenezwa na Marck & Co drug company ilifanikiwa kutolewa nchini Guinea mwaka 2015.
Ilitumika kama ''matumizi ya dharura'' ambayo huruhusu matumizi ya dawa ambazo hazina leseni ( leseni huchukua miaka au miongo kuipata) wakati hakuna namna ya kufanya, lakini kwa idhini ya serikali ya nchi iliyoathiriwa.
Data za shirika la afya duniani (WHO) zinaonyesha kuwa chanjo ya Merck ina ufanisi kwa kiwango cha asilimia 97.5 kwa wale waliopatiwa chanjo, ikilinganishwa kwa wale wasiochanjwa.
WHO inasema chanjo hii imethibitisha kuwa salama na yenye ufanisi dhidi ya Ebola, lakini majaribio zaidi yanahitajika kabla dawa haijapatiwa leseni.
Hivyo, tuko mahali palepale kama ilivyokuwa kwa chanjo ya kwanza mwaka 2015 inayotumika sasa- kuna ushahidi thabiti kuwa iko salama na kuwa itakuwa na ufanisi, lakini haijajaribiwa kwenye eneo lililoathiriwa na virusi vya Ebola na pia haina leseni.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kuna chanjo ya kutosha?
Je kuna chanjo tayari ambayo imethibitishwa kuwa na ufanisi dhidi ya Ebola, kwa nini kusiwe na nyingine zaidi?
Mwezi Julai, Kamati ya dharura ya WHO ilisema ''inatambua upungufu wa dawa'' ya chanjo ya Marck.
Dokta Josie Golding wa mfuko wa Wellcome, anasema inawezekana kusiwe na chanjo ya kutosha ya kupambana na mlipuko kwa sasa.
''Ikiwa ni hivyo, hali inaweza kuwa mbaya zaidi. Tuna imani kubwa kuwa kuna uhitaji wa haraka wa kuwa na chanjo ya pili iliyotengenezwa na Johnson and Johnson.''
Kwa kifupi ni kuwa, dawa za chanjo kwa sasa zinaweza kuwa zenye kufaa, lakini zisiwe msaada ikiwa mlipuko wa maradhi utaendelea.
Kampuni ya dawa ya Merck inasema kuwa kuna chanjo ya kutosha kwa ajili ya watu 500,0000, na wako kwenye mchakato wa kutengeneza zaidi.
Takribani dozi milioni moja na nusu za chanjo zinapatikana.
Kuna takribani watu milioni kumi katika majimbo mawili kwa pamoja yaliyoathirika.
Chanjo ya sasa inatolewa kwa wafanyakazi wa afya na watu ambao wako hatarini kupata maambukizi ya virusi.
Hivyo, ikiwa serikali ya Drc itataka chanjo itolewe katika eneo kubwa zaidi, itahitaji dawa zaidi.
Wale wanaotaka kutumia chanjo ya Johnson & Johnson, walipendekeza kutumia kwa maeneo ambayo hayajakumbwa na Ebola, ili kuwachanja watu walio nje ya maeneo yalioathiriwa.
Kuna matumaini kuwa hatua hiyo itazuia virusi kusambaa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kutoaminiwa na jamii
Serikali ya DRC imeeleza kuhusu ugumu wa kutumia chanjo aina mbili kwa pamoja katika kupambana na Ebola.
Inasema kuna hatari ya kukanganya watu na kuongeza hali ya kutoaminika miongoni mwa jamii zilizoathirika.
Mapambano dhidi ya Ebola kwa sasa yamekuwa yakikumbwa na changamoto ya kutoaminika na jamii.
Pia kumekuwa na maoni kuwa chanjo mpya -ambayo itahitaji sindano mbili itakuwa ngumu kusimamia kwa kuwa watu hutembea tembea na hata kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine kwa sababu ya usalama.













