Kwanini Trump anafanya mashambulizi Somalia?

Picha ya Donald Trump, akiwa amevalia suti ya buluu, akinyoosha kidole chake wakati wa mkutano na waandishi wa habari

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa Marekani Donald Trump
    • Author, Mary Harper
    • Nafasi, Somalia analyst
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Kuwasaka na kupigana na wanamgambo ambao ni tegemeo kwa kundi la Dola la Kiislamu (IS) barani Afrika inaweza kuwa kazi ngumu kwani wanajificha mbali kwenye milima ya kaskazini-mashariki mwa Somalia.

Lakini kwa mtindo wa kawaida wa Donald Trump, baada ya rais mpya wa Marekani kuagiza mashambulizi ya angani katika eneo hilo mwishoni mwa juma lililopita, alichapisha kwenye mitandao ya kijamii: "TUTAWAONA NA TUTAWAUA!"

Trump alisema shambulizi hilo, chini ya wiki mbili tangu alipoapishwa, lililenga mpangaji mkuu wa mashambulizi wa IS na wanamgambo wengine katika eneo la Puntland, ambalo ni sehemu ya utawala wa ndani ya Somalia, na liliharibu mapango wanayoishi na kuua magaidi wengi bila kuathiri raia kwa namna yoyote.

Alijipiga kifua kwamba alifanikiwa pale ambapo Rais wa zamani wa Marekani Joe Biden alishindwa.

"Biden na wafuasi wake hawakuweza kufanya haraka kutekeleza kazi hiyo. Mimi nilifanya!"

Somalia kuwa eneo lengwa la operesheni kubwa ya kijeshi ya Marekani chini ya utawala mpya lilishangaza wengi nchini humo ambao walikuwa na hofu kuwa Marekani ingeachana nao.

Katika muhula wake wa kwanza, Trump aliondoa karibu wanajeshi 700 wa Marekani, uamuzi uliofutwa na mrithi wake.

Mkataba wa dola 600,000 (paundi 492,000) kwa mwaka ambao serikali ya Somalia ilitia saini hivi karibuni na kampuni maarufu ya kuhimiza masuala ya kisiasa ya Washington, BGR Group, ni ishara ya wasiwasi wao.

Chini ya Biden, wanajeshi wa Marekani nchini Somalia walikuwa wakifanya operesheni maalumu, wakifundisha kikosi cha Somalia na kufanya mashambulizi ya angani mara kwa mara.

Malori kadhaa yakiwa yamebeba wanajeshi yakiendeshwa katika eneo lisilonyooka katika milima ya Puntland

Chanzo cha picha, @PuntlandSSR

Maelezo ya picha, Milima ya Golis ni mahali ambapo wanamgambo wa IS wanajificha na ambapo vikosi vya usalama vya Puntland vinajaribu kuwasaka.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Siku moja kabla ya shambulizi la angani, Washington Post ilichapisha mahojiano na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud ambapo alisihi Marekani "isiwatoe washauri na wataalam wa Marekani ambao wanatoa mafunzo kwa vikosi vya usalama nchini Somalia".

Baada ya shambulizi la hivi majuzi rais wa Somalia alionesha hali ya kukata tamaa, askikiri "umuhimu wa msaada wa Marekani katika vita dhidi ya ugaidi wa kimataifa" na kukaribisha muendelezo wa kushirikiana na Marekani chini ya utawala wa Rais Donald Trump.

Lakini mashambulizi ya angani ni tofauti na wanajeshi wanaoshika doria katika nchi kavu na pia Trump hakukomesha mashambulizi ya anga katika muhula wake wa kwanza.

Aliyazidisha hadi mashambulizi 400.

Mashambulizi ya angani haina maana kwamba serikali ya Marekani itaongeza ushiriki wake wa kijeshi nchini Somalia," anasema Matt Bryden, mshauri mkakati wa utafiti wa Sahan makao yake yakiwa Nairobi.

"Mawakili kadhaa wa Marekani waliotarajiwa kuchukua nafasi za uongozi katika masuala ya Afrika hawaoni haja tena kushirikiana na Somalia katika masuala ya kiusalama huku wakikosoa vikali viwango vya juu vya msaada wa usalama uliopeanwa katika miaka ya hivi karibuni bila kuleta mabadiliko."

Mbinu ya kupambana na ugaidi ya Puntland ni tofauti na ile ya serikali kuu ya Somalia, ambayo ilivunja uhusiano nayo mwezi Machi mwaka jana.

Ni ya kujitegemea zaidi na siyo tegemezi sana kwa msaada kutoka kwa vikosi vya Umoja wa Afrika – ambavyo ni takriban 12,000 wakiwa nchi kavu – na kupigwa jeki na mataifa ya kigeni ikiwa ni pamoja na Marekani na Uturuki.

Kama vile anavyosema Mohamed Mubarak, mkuu wa ofisi ya uratibu wa usalama ya Puntland, ni wanajeshi kutoka kaskazini-mashariki ambao wamekuwa wakipigana na IS kwa miaka mingi bila msaada mkubwa au shukrani kutoka kwa wengine.

"Sio haki kuweka mbele mashambulizi ya angani wakati sisi tumekuwa tukipigana na kuhatarisha maisha yetu," anasema Bwana Mubarak.

mwenye ndevu za rangi ya chungwa na amevaa miwani na kilemba cheusi, anainua kidole chake huku akiongea. Miti na kichaka vinaweza kuonekana nyuma yake.

Chanzo cha picha, al-kataib

Maelezo ya picha, Haijabainika iwapo Abdulqadir Mumin, kiongozi mwenye ushawishi mkubwa wa IS-Somalia, aliuawa katika shambulio la anga la Marekani mwaka jana, au kama sasa anaongoza IS duniani kote.

"Hata kama ulimwengu mzima unaendelea na shughuli zao za kawaida, sisi tunapigana na wanamgambo wa IS, ambao wamekuwa ni changamoto kimataifa," anasema.

"Hatujaona msaada mkubwa isipokuwa kutoka Kenya, Ethiopia na UAE. Hatujui kama Wamarekani watafanya mashambulizi zaidi ya angani."

Puntland inasema vikosi vyake vimevamia mapango 48 na vituo vya IS – na kuharibu ndege zisizokuwa na rubani nyingi na vifaa vya kulipua – tangu kuanzisha operesheni yake kamili ya "hilaac" mwaka jana.

Ingawa IS imejikita zaidi nchini Somalia kwa takriban muongo mmoja, haijakuwa tishio kubwa kama kundi la kiislamu la al-Shabab, ambalo linadhibiti sehemu kubwa za nchi na limeelezewa kama tawi lenye mafanikio zaidi la al-Qaeda.

Hata hivyo, kwa muda wa hivi karibuni, IS imekuwa tishio – ndani ya Somalia, kanda na kimataifa.

Mamlaka za Puntland na maafisa wa Marekani ambao hawakutaka kutajwa majina wanasema kiongozi wa IS-Somalia, Abdulqadir Mumin mwenye ndevu za rangi ya machungwa na miwani, sasa ndiye kiongozi mkuu wa IS duniani.

Ripoti za awali zilisema alikuwa ameuawa katika shambulizi la angani la Marekani mwezi Mei lakini hilo halijathibitishwa.

Iwe Mumin ni kiongozi wa IS au yuko hai au amekufa, IS-Somalia imekuwa ikitoa wasiwasi zaidi kwa mataifa ya kigeni.

Wanajeshi wa Puntland wameketi chini. Wamevaa barakoa nyeupe, helmeti za hudhurungi na mshipi wa risasi nyingi shingoni wakiwa wameshikilia bunduki

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Puntland imetoa mafunzo kwa kikosi cha wanajeshi mahiri kuwakabili wanamgambo wa IS

Kama vile Trump alivyosema: "Wauaji hawa, ambao tuliwapata wakijificha kwenye mapango, walitishia Marekani na washirika wetu."

Kwa mujibu wa Tricia Bacon, mkurugenzi wa kituo cha sera za kupambana na ugaidi katika Chuo Kikuu cha Marekani kilichopo Washington DC, "IS-Somalia imechukua majukumu zaidi katika mtandao wa Dola la Kiislamu, hasa barani Afrika lakini pia nje ya bara hilo."

Kwa matawi ya IS yanayoendesha shughuli zao kote Afrika, kuanzia Msumbiji hadi Mali, kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hadi Nigeria, IS-Somalia imekuwa kiungo muhimu katika kikosi hicho cha wanamgambo wa IS.

Bi Bacon anatahadharisha kuwa IS-Somalia inatazama kupambanua mawanda yake nje ya Afrika.

"Ina uwezo wa kurahisisha na kuchangia mashambulizi ya IS katika mataifa ya Magharibi, ikiwa ni pamoja na Marekani. Pia inatafuta mikakati ambayo watashambulia na kuhusishwa moja kwa moja katika mashambuli ya matifa hayo,'' anasema.

"Washirika wa kimataifa wanapaswa kutoa msaada zaidi kwa juhudi za Puntland dhidi ya kundi hilo."

Bwana Bryden anasema kushirikiana na waasi wa Houthi walioungwa mkono na Iran kupitia Bahari Nyekundu huko Yemen pia ni tatizo.

"Kama al-Shabab, IS-Somalia imepokea silaha na mafunzo kutoka kwa Houthi huko Yemen, ambayo ni chanzo cha wasiwasi kwa serikali ya Marekani na washirika wake," anasema.

Wanaume wawili waliovalia koti na kofia za kijani kibichi wanaonekana wakiwa na jeti ya jeshi la Marekani nyuma yao - picha iliyotolewa na Kamanda wa Marekani ya Afrika, Februari 2025

Chanzo cha picha, @USAfricaCommand

Maelezo ya picha, Vikosi vya usalama nchini Somalia vinatumai shambulizi la anga la utawala wa Trump halitakuwa la mara moja

Idadi ya wapiganaji wa kigeni wanajiunga na kikosi hicho, ikiongezea ujuzi na wingi wa wanamgambo.

Wanaoshukiwa zaidi kuajiriwa na IS-Somalia ni wakimbizi kutoka Ethiopia, ambao hujipata katika kisiwa cha Puntland cha Bosaso wakiwa na matumaini ya kuvuka ng'ambo wakitafuta maisha mazuri.

IS huwalipa mshahara mnono zaidi ya kile wangelipwa katika mataifa ya uarabuni na wataalamu wanasema huenda viongozi wengi wa kikosi hicho wana asili ya Ethiopia.

''Tunatathmini IS-Somalia inajumuisha wapiganaji wa kigeni asilimia 80%,zaidi kutoka Afrika Kaskazini, Ethiopia, Tanzania na mataifa ya uarabuni, katika orodha hiyo,'' anasema Mubarak.

Anaendelea kutathmini akidai huenda kikosi hicho kina wapiganaji 1,000; ingawa Umoja wa Mataifa UN unasema idadi ya wanamgambo hao ni takriban 600 hadi 700.

Mwaka jana mwezi Oktoba, mkuu wa Amri ya Kijeshi ya Afrika ya Marekani, Michael Langley, alisema alifikiri IS imeongezeka kaskazini mwa Somalia "maradufu" kwa mwaka mmoja.

Kundi hili lilifanya mojawapo ya mashambulizi yake ya kushtukizia mwezi Disemba, ikilenga kambi ya kijeshi katika eneo la Bari la Puntland.

Kundi hilo lilitoa taarifa ikisema hakuna raia yoyote wa Kisomali aliyehusika.

Washambulizi 12 walikuwa kutoka nchi saba - Tanzania, Algeria, Morocco, Libya, Tunisia, Yemen na Ethiopia.

Wapiganaji hawa pia wana ujuzi zaidi wa namna ya ukusanyaji wa fedha.

Marekani, Umoja wa Mataifa na wataalamu wa Somalia wanasema sehemu muhimu ya miundombinu ya kifedha ya IS - ofisi ya al-Karrar - iko Puntland, ikigawa fedha na utaalamu kwa matawi mengine ya kundi hili barani Afrika na nje ya bara.

Ofisi ya Udhibiti wa Mali za Nje ya Hazina ya Marekani (OFAC) ilisema IS-Somalia ilikusanya takriban dola milioni 2 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2022 kwa kutoza biashara zilizoko mitaani, bidhaa zinazoingizwa nchini humo, wafugaji na wakulima.

Ikiwa vikosi vya Puntland vitafanikiwa kuwatimua wapiganaji, msaada wa angani utakuwa muhimu.

Baada ya shambulizi la Marekani, polisi wa Puntland walisema mkuu wa kikosi cha mauaji cha IS-Somalia, Abdirahman Shirwa Aw-Said, alijisalimisha.

Lakini wataalamu wanasema mashambulizi kama haya yatakuwa na ufanisi ikiwa yatafanyika mara kwa mara ili kuwafuatilia mapango wanayojificha IS zilizopo nchini Somalia na kuzuia zingine kutokea.

Haijulikani ikiwa Marekani na kiongozi wake ambaye hubadilisha maamuzi kila dakika wanahamu ya kuendelea kulipua milima iliyoko kaskazini-mashariki mwa Somalia.

Mary Harper ameandika vitabu viwili kuhusu Somalia, ikiwemo "Everything You Have Told Me Is True," kuhusu maisha chini ya utawala wa al-Shabab.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid