Uwanja wa soka ambao pia unatumiwa kuwaua wahalifu Somalia

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Na Naima Said Salah
- Nafasi, Mogadishu
Katika ufuo wa bahari katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu kuna nguzo sita kwenye mchanga mweupe. Mawimbi ya Bahari ya Hindi ya buluu hufika karibu na mara nyingi ndiyo hushuhudia matukio fulani ya kutisha.
Onyo: Makala haya yana maelezo ambayo yanaweza kuwa ya kuogofia kwa baadhi ya watu
Kila mara vikosi vya usalama huleta wanaume mahali hapa, huwafunga kwenye nguzo kwa Kamba, huwafunika vichwa vyao na kuwapiga risasi.
Wanachama wa kikosi cha kufyatua risasi waliopewa mafunzo maalum pia huwa wamefunika nyuso zao.
Vichwa vya watu waliokufa huinama chini lakini miili yao inabaki wima, iliyopigwa kwenye miti. Mashati yao chakavu na hupeperushwa na upepo.
Baadhi wamekutwa na hatia na mahakama ya kijeshi kwa kuwa kwenye kundi la Kiislamu la al-Shabab, ambalo limeeneza ugaidi nchini Somalia kwa takriban miaka 20 na kudhibiti maeneo makubwa ya nchi.
Wengine ni askari waliopatikana na hatia ya kuua raia au wafanyakazi wenzao. Mara kwa mara mahakama hushughulika na wahalifu wa kawaida waliohukumiwa kifo kwa sababu makosa yao ni makubwa sana.
Takriban watu 25 walinyongwa kwenye ufuo huo mwaka jana.
Mtu wa hivi punde anayekabiliwa na hukumu ya kifo ni Said Ali Moalim Daud ambaye alihukumiwa kifo tarehe 6 Machi kwa kumfungia mkewe, Lul Abdiaziz, ndani ya chumba na kukichoma moto. Alisema alimchoma moto akiwa hai kwa sababu alikuwa ameomba talaka.
Nyuma ya eneo la mauaji kuna makazi madogo yasiyo rasmi katika wilaya ya Hamar Jajab - yaliyojaa makazi ya muda ambapo takriban familia 50 zinaishi kwenye eneo la kile kilichokuwa chuo cha polisi.
"Mara tu wavulana wangu wadogo watano wanaporudi nyumbani kutoka shuleni, wanakimbilia ufukweni kukimbia au kucheza mpira," anasema Fartun Mohammed Ismail, mmoja wa wakazi wa ufukweni wa kituo cha zamani cha mafunzo ya polisi.

Chanzo cha picha, Naima Said Salah
"Wanatumia nguzo za kuuawa kama nguzo za goli," anasema.
"Nina wasiwasi na afya ya watoto wangu kwa sababu wanacheza kwenye damu iliyomwagika mahali ambapo watu wanapigwa risasi.
"Eneo hilo halijasafishwa baada ya watu kuuawa."

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Makaburi ya wale ambao wamepigwa risasi hupatikana karibu na pwani.
Bi Ismail anasema watoto wake wamezoea vurugu na ukosefu wa usalama kwa sababu walizaliwa Mogadishu, jiji lililoathiriwa na vita kwa miaka 33.
Hata hivyo yeye na wazazi wengine wanahisi kuwa kucheza katika damu ya wahalifu waliohukumiwa ni kitu kibaya sana.
Hata hivyo, ni vigumu kuwazuia watoto kujiunga na marafiki zao kwenye ufuo wa bahari wakati wazazi wengi wanajaribu kutafuta riziki kwa hivyo si mara zote wako karibu kuweza kuwazuia.
Kwa kawaida mauaji haya hufanyika mapema asubuhi, kati ya 06:00 na 07:00.
Wanahabari pekee ndio hualikwa kushuhudia mauaji hayo lakini hakuna anayewazuia wakaazi wa eneo hilo wakiwemo watoto kukusanyika na kutazama.
Ufuo huo ulichaguliwa kama mahali pa kuulia mnamo 1975 na Siad Barre alipokuwa rais kwa sababu wenyeji wa karibu wangeweza kutazama.
Serikali yake ya kijeshi ilisimamisha nguzo kwa baadhi ya maulama wa Kiislamu ambao walipigwa risasi papo hapo kwa kupinga sheria mpya ya familia ambayo iliwapa wasichana na wavulana haki sawa katika urithi.
Wazazi wana wasiwasi kwamba watoto wanaocheza kwenye uwanja wa kunyongwa wana hatari ya kupigwa risasi mtu anapouawa.
Wanasema watoto wao wanawaogopa polisi na wanajeshi kwa sababu wanawahusisha tu na kuua watu mbele yao.

Chanzo cha picha, AFP
"Ninatatizika kulala usiku na kuhisi wasiwasi mwingi wakati wote," anasema Faduma Abdullahi Qasim, ambaye pia anaishi katika kitongoji kilicho umbali kidogo kutoka zuwanja wa kunyongwa.
"Wakati mwingine nasikia milio ya risasi asubuhi na kujua mtu ameuawa," anasema.
"Ninajaribu kuwaweka watoto wangu ndani wakati wote. Sipendi kwenda nje na kuona damu ikitiririka kwenye mchanga kando yangu."
Ingawa wakazi wengi wanaoishi katika ukaribuhuo wana kiwewe kwa kuishi karibu sana na uwanja wa kunyongwa, Wasomali wengi wanaunga mkono hukumu ya kifo, hasa kwa wanachama wa al-Shabab.
Bi Qasim hapingi jambo hilo - hasa ikizingatiwa kwamba mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 17, ambaye alifanya kazi ya kusafisha katika duka vitafunio, aliuawa katika mlipuko mkubwa wa magari mawili mjini Mogadishu mnamo Oktoba 2022. Zaidi ya watu 120 walikufa na 300 walijeruhiwa katika shambulio hilo, lililolaumiwa kwa al-Shabab.
“Binafsi siwafahamu watu wanaouawa lakini naamini kitendo hicho si cha kibinadamu,” anasema.
Sio tu watoto kutoka kitongoji cha pwani wanaocheza kwenye mchanga karibu na nguzo za kunyongwa.
Vijana kutoka maeneo mengine ya jiji hukusanyika hapo, haswa siku za Ijumaa, wikendi ya Somalia.

Chanzo cha picha, AFP
Kati yao ni Abdirahman Adam mwenye umri wa miaka 16.
“Mimi na kaka yangu huja hapa kila Ijumaa kuogelea na kucheza soka ufukweni,” anasema.
"Dada yangu anakuja pia, akiwa amevalia nguo zake nzuri zaidi ili aweze kuonekana mrembo tunapompiga picha."
Yeye na wengine wanaomiminika ufukweni wanajua kuhusu kuuawa na makaburi ya watu waliopigwa risasi huko - lakini wanaenda bila kujali.
Kwao eneo lililo kati na zuri ni muhimu zaidi.
"Wanafunzi wenzetu wana wivu wanapoona picha. Hawajui tunabarizi kwenye uwanja wa kunyongwa."
Imetafsiriwa na Jason Nyakundi












