Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Matokeo ya uchaguzi Kenya 2022:Ngoja ngoja ya muda mrefu huku kura za urais zikionyesha Raila Odinga na William Ruto wamekabana koo
- Author, Dickens Olewe
- Nafasi, BBC News
Mfumo wa kuhesabu kura nchini Kenya haujaingiliwa kwa njia yo udukuzi huku kukiwa na ukosefu wa Subira ya matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika Jumanne, afisa mkuu wa uchaguzi amesema.
"Hakuna kitu kama hicho kilichotokea. Ni habari potofu," Afisa mkuu mtendaji wa tume ya uchaguzi Marjan Hussein Marjan alisema.
Mitandao ya kijamii imekumbwa na madai kuwa matokeo ghushi yamepakiwa huku hesabu hiyo ikithibitishwa.
Taratibu za vyombo vya habari zinaonyesha wagombeaji wawili wakuu - Raila Odinga na William Ruto - wapo katika ushindani mkali.
Lakini ni tume ya uchaguzi pekee ndiyo inaweza kutangaza mshindi - na ina siku saba kufanya hivyo.
"Tulitarajia kwamba watu wangejaribu kudukua mifumo yetu... tunaihakikishia nchi nzima kwamba mifumo yetu iko salama," Bw Marjan aliwaambia waandishi wa habari Ijumaa alasiri.
Awali mkuu wa uchaguzi Wafula Chebukati alisisitiza kuwa hakuna haja ya kuogopa kuona tofauti za idadi ya watu kutoka makundi mbalimbali ya vyombo vya habari kwani zitafanana mwishowe: "Matokeo yanatoka kwenye tovuti moja ya umma; mbinu [ya kila chombo cha habari] ni tofauti. ."
Ni nini kinaendelea katika kituo kikuu cha kuhesabia kura?
Haya yanajiri katika kituo cha kitamaduni kiitwacho Bomas katika mji mkuu, Nairobi, ambapo maafisa kutoka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wanashughulika na kuthibitisha matokeo.
Wanalinganisha picha za fomu za matokeo kutoka zaidi ya vituo 46,000 vya kupigia kura nchi nzima na fomu halisi zinazoletwa na maafisa kutoka kila moja ya maeneo bunge 290.
Hii ni kuhakikisha kuwa matokeo yanalingana.
Haya yanashuhudiwa na maajenti wa vyama kutoka vyama vikuu, ambao Bw Chebukati anasema wanaendelea kuchelewesha hilo kwa kuligeuza kuwa la "uchunguzi" wa matokeo.
Alisema maafisa hawapaswi kuchukua zaidi ya dakika 15 kuthibitisha matokeo.
Shughuli ya kuhesabu kura katika baadhi ya vituo pia ilicheleweshwa na kusafiri hadi Nairobi, haswa na maafisa kutoka maeneo ya mbali, kunaweza kuwa sababu zaidi ya kupunguza kasi ya mambo.
Uthibitishaji pia ulisitishwa kwa muda siku ya Ijumaa baada ya mzozo kuzuka, unaodaiwa kuhusisha mtu asiye na kibali kuonekana na kompyuta ndogo.
Je, hesabu za vyombo vya habari zinafanywa vipi?
Vikundi vya waandishi wa habari wanaofanya kazi katika vituo mbalimbali vimekuwa na kazi kubwa ya kuweka takwimu zilizopokelewa kutoka kwa kila kituo cha kupigia kura moja baada ya nyingine.
Kila chombo cha habari kinafanya hivyo kwa kasi tofauti na kuchagua vituo vya kupigia kura kwa mpangilio tofauti.
Kufikia Ijumaa asubuhi, vyombo vya habari vya ndani vilikuwa vimepunguza kasi ya hesabu yao - ingawa sababu haiko wazi, wengine wakisema wafanyikazi walikuwa wamechoka.
Bw Chebukati alisema alitumai makundi ya wanahabari yangeungana ili kujumlisha matokeo, lakini wameamua kila moja kufanya kivyake.
Wakenya wanajisikiaje?
Kuna hali ya wasiwasi nchini kwani chaguzi zilizozozaniwa huko nyuma zilisababisha vurugu au mchakato mzima kufutwa.
Kufuatia kura ya 2007, takriban watu 1,200 waliuawa na 600,000 walikimbia makazi yao kufuatia madai ya kuibiwa kwa kura.
Mnamo 2017, hitilafu kubwa za vifaa zilisababisha Mahakama ya Juu kubatilisha matokeo na kuamuru uchaguzi wa urais urudiwe.
Viongozi wanakabiliwa na shinikizo la kurekebisha mambo wakati huu.
Nchi mara nyingi hukwama wakati wa uchaguzi, shughuli kote nchini zimepungua na shule zimefungwa angalau hadi wiki ijayo Jumatatu. Kati kati mwa Nairobi, mitaa yenye shughuli nyingi mara nyingi haina watu.
Madai ya wizi wa kura ni ya zamani kama nchi. Ilikuwa ni sehemu ya siasa hata kabla ya chaguzi za vyama vingi kuanzishwa tena katika miaka ya 1990, lakini msukumo wa uchaguzi huru na wa haki haujawahi kulegalega.
Baada ya ghasia zilizofuatia uchaguzi wa 2007, vyama vya siasa na wanaharakati walibishania matumizi ya teknolojia badala ya sajili halisi, ambayo inaweza kubadilishwa kwa urahisi, ili kuhakiki wapiga kura.
Uchaguzi wa mwaka huu ni mara ya tatu kwa teknolojia kutumika lakini bado haujafanya uchaguzi ambao haujapingwa mahakamani.
Wakati huo huo, kundi la watumishi wakuu wa umma waliwaambia waandishi wa habari siku ya Ijumaa kwamba maandalizi ya kukabidhi madaraka kwa njia laini yataanza punde tu tume ya uchaguzi itakapomtangaza rais mteule.
Tutajua matokeo lini?
Haijulikani ni lini matokeo ya mwisho yatajulikana, lakini tume ya uchaguzi imeanza kutangaza hesabu zilizothibitishwa kutoka kwa maeneo bunge 290.
Iwapo kuna kiongozi wazi wa kinyang'anyiro hicho, huenda sherehe zikazuka - lakini IEBC pekee ndiyo inaweza kufanya hivyo rasmi.
Ili kushinda kinyang'anyiro cha urais katika awamu ya kwanza, mgombea anahitaji:
• zaidi ya nusu ya kura zote zilizopigwa kote nchini
• Takribani 25% ya kura zilizopigwa katika kaunti zisizopungua 24
Vinginevyo upigaji kura unakwenda kwa duru ya pili ambayo kwa mujibu wa sheria inapaswa kufanyika ifikapo tarehe 8 Septemba.
Uchaguzi Kenya 2022:Unaweza pia kusoma