Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Matokeo ya Uchaguzi Kenya 2022: Wanawake waliong’ara katika uchaguzi
- Author, Asha Juma & Dinah Gahamanyi
- Nafasi, BBC Swahili
Huku matokeo rasmi ya uchaguzi mkuu nchini Kenya yakiendelea kutolewa, katika uchaguzi wa mwaka huu wanawake wameonekana kuibuka washindi na kujinyakulia viti mbali mbali.
Hii inajiri huku Kenya ikiwa bado haijaweza kutekeleza sheria ya theluthi mbili ya uwakilishi wa jinsia, jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wanawake kwamba linawanyima wao fursa ya uwakilishi katika ngazi za uongozi.
Hatahivyo katika uchaguzi huu wanawake wameweza kujitokeza na kupata ushindi utakaowawezesha kupata fursa hiyo.
Baadhi ya waliojinyakulia viti ni sura ngeni huku wengine wakirejea au kubadilisha nyadhifa.
Linet Chepkorir 'Toto'
Akiwa mbunge mwanamke mwenye umri mdogo zaidi, Linet Chepkorir mweye umri wa miaka 24 amechaguliwa kuwa mbunge wa kiti cha uwakilishi wa wanawake yaani (Women Rep) kutoka jimbo la Bomet katika Bonde la Ufa.
'Toto' alipata umaarufu hivi maajuzi baada ya kushinda tiketi ya chama cha Muungano wa United Democratic Alliance (UDA) unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto kwenye uchaguzi wa ngazi ya vyama na kumshinda Joyce Korir.
Atakuwa mwakilishi mdogo zaidi katika bunge la 13.
Agnes Pareiyo aweka historia kama mbunge mwanamke wa kwanza Narok
Mwanaharakati wa kupambana na ukeketwaji wa wanawake, Bi Agnes Pareiyo amechaguliwa kuwa mbunge wa kwanza wa eneo la Narok Kaskazini.
Ni mgeni katika siasa za Kenya awali akifahamika kwa harakati zake za kupambana na ukeketaji wa wanawake ambapo mwaka 2018 aliendesha kampeni iliyoitwa END FGM ambapo wanaharakati walituma jumbe kwenye mitandao ya kijami kupitia hashtag 'DontTouch FGMLaw'.
Bi Pareiyo alizua gumzo na kuvunja ukimya wa kile kilichoonekana kama kisichowezekana katika jamii ya Kimasai kwa kuchaguliwa kuwa mbunge wa kwanza mwanamke.
Eneo bunge la Narok Kaskazini liliongozwa na marehemu William Ole Ntimama kabla ya Moitalel Ole Kenta kuchukua nafasi hiyo ambaye kwenye uchaguzi huu anawania nafasi ya ugavana wa Narok.
Mnamo 2017, aligombea kwa tiketi ya chama cha Jubilee lakini akashindwa na Kaitikei Rotiken kwenye kura za mchujo za chama.
Ruweida Obbo
Ruweida Obbo, mwanamke wa kwanza rubani wa kibajuni, ndiye aliyepata ushindi wa kiti cha ubunge katika jimbo la Lamu Mashariki.
Kabla ya kuchaguliwa kwake, Ruweida Obbo al Maarufu ''Captain Ruweida'' alikuwa mbunge wa kiti cha uwakilishi wa wanawake katika Bunge la taifa.
Pia aliahidi kuendeleza uwezeshaji wa wanawake, watoto na watu wenye mahitaji maalum.
Wakati wa kampeni zake za kisiasa, Bi Obbo alikuwa ameahidi kutoa hamasa juu ya utumizi wa dawa za kulevya ambao unaendelea kuathiri vijana wengi Lamu.
Gladys Wanga
Wanga anaingia katika historia kama gavana mwanamke mwenye umri mdogo zaidi na gavana wa kwanza katika eneo la Nyanza.
Gladys Wanga amemuangusha mpinzani wake wa karibu aliyekuwa gavana wa Nairobi Dkt. Evans Kidero.
Alikuwa mwanamke wa kwanza mwenyekiti wa chama cha ODM katika eneo la Homa Bay na pia wa kwanza kuongoza Kamati ya Kitaifa ya Fedha na Mipango ya Kitaifa.
Akizungumza wakati wa kampeni zake, Wanga aliwaahidi wakazi wa Homa Bay atatumia rasilimali zilizogatuliwa kuboresha maisha ya wananchi na kuendeleza kaunti ya Homa bay.
"Kama kijana naamini nina nafasi ya kutengeneza urithi, sio ule ninaouacha bali ule ninaoishi, kwa maana ya kwamba ninapofanya vibaya naweza kuishi miaka mingi kuona ubaya, na ninapofanya kilicho sawa, ninaishi kuona mema ambayo nimefanya," alisema.
Alifichua kwamba alijihusisha na siasa akiwa na umri wa miaka mitano aliposaidia kusambaza 'chumvi' kwa wanakijiji wakati wa kampeni za uchaguzi za babake.
Wanga pia angeandamana na babake kwa shughuli za kisiasa na mikutano.
Kawira Mwangaza
Mwakilishi wa wanawake wa Meru Kawira Mwangaza, ameshangaza wengi kwa kuwabwaga vigogo wa kisiasa Mithika Linturi na gavana anayeondoka Kiraitu Murungi kwenye kinyang'anyiro cha kumchagua gavana wa kaunti ya Meru.
Mwangaza, ambaye alishindana kama mgombea huru amefanikiwa kuibuka na ushindi baada ya kutawala siasa za humu nchini kwa miaka mingi.
Bi Mwangaza, aliyekuwa mbunge kwa mara ya kwanza, alitangaza nia ya kumwondoa madaraka gavana wa Meru, Kiraitu Murungi mwaka wa 2019.
Mwakilishi huyo wa kike, ambaye pia ni mwanzilishi na askofu wa Kanisa la Baite Family Fellowship, alimteua Isaac Mutuma, kasisi wa Kanisa hilo kama mgombea mwenza wake.
"Nimemtambua Isaac Mutuma kama mgombea mwenza wangu katika kinyang'anyiro cha Agosti. Hii ni timu ya watu wenye ujuzi wa hali ya juu na watumishi wa watu. Siwezi kuteua bila maombi," alisema.
Katika ulingo wa kisiasa, Bi Mwangaza ameonyesha umahiri wake katika ujuzi alionao wa kuhamasisha watu mashinani.
Bi Mwangaza ameahidi kuwapa wakazi wa Meru uongozi bora kupitia matumizi ya busara ya pesa za umma.
Pia ameshinda uungwaji mkono wa kasisi Kiambi Atheru, ambaye alikuwa amepanga kuwania ugavana kwa mara ya pili mwaka huu, baada ya kushindwa mwaka wa 2017.
Wavinya Ndeti
Wavinya Ndeti alijiunga na siasa mwaka wa 2007 akigombea na kuchaguliwa kuwa mbunge wa eneo bunge la Kathiani chini ya Chama Cha Uzalendo (CCU).
Katika kushinda kiti hicho, Ndeti alikuwa mwanamke pekee aliyewakilisha eneo bunge hilo tangu uhuru.
Ndeti aliteuliwa katika serikali kuu ya muungano kama Waziri Msaidizi wa Vijana na Michezo chini ya Helen Sambili.
Ndeti, ni mmoja wa wanachama waanzilishi wa Muungano wa Mageuzi na Demokrasia - CORD, ulikuwa muungano wa vyama vingi vya kisiasa vilivyojengwa kwa karibu na Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, na Moses Wetangula, kuwania uchaguzi mkuu wa Kenya wa 2013.
Ndeti, aliwania kiti cha Gavana wa Machakos kwa tiketi ya CCU mwaka wa 2013. Alimchagua aliyekuwa waziri wa Maji na Maliasili Mutua Katuku kama mgombea mwenza wake.
Katika uchaguzi wa mwaka huu uliofanyika Agosti 9, Wavinya ndeti amejitosa kwenye kusaka kiti cha ugavana kupitia chama cha Wiper na Gavana wa Machakos anayeondoka Alfred Mutua wa chama cha Maendeleo Chap Chap, alimuunga mkono kwenye ugombea wake.
"Ninakubali kwa ukarimu kuidhinishwa na gavana anayeondoka Dkt. Alfred Mutua na ninathamini kujitolea kwake kwa umma kunipigia kura. Ni faida kubwa kwetu na inatusaidia sana kuonyesha imani kuwa timu yetu pekee ndiyo inayohitaji kuongoza Kaunti," alisema alipoidhinishwa.
Wavinya ndiye ndiye mzaliwa wa mwisho kati ya watoto 10 wa Ndeti, lakini kati ya hao wote, ni yeye tu na marehemu kaka yake, Ignatius Dick Ndeti walioingia kwenye siasa. Dick Ndeti alikuwa diwani wa Athi River baada ya babake.
Susan Kihika amwangusha kigogo Lee Kinyanjui
Seneta wa Nakuru Susan Kihika wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) amemwangusha kigogo Lee Kinyanjui wa chama cha Jubilee katika kinyang'anyiro cha ugavana kaunti ya Nakuru.
Susan Wakarura Kihika alichaguliwa katika bunge la seneti mwaka wa 2017.
Katika uchaguzi wake, aliteuliwa kuwa kinara wa wengi wa chama cha Jubilee.
Alishikilia wadhifa huo hadi tarehe 11 Mei 2020 ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Seneta Irungu Kangata.
Ni mmoja wa viongozi waliojiondoa katika chama cha Jubilee pamoja na naibu rais baada ya makubaliano ya maridhiano kati ya Rais Uhuru na kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Pia unawezakusoma: