Nguvu ya mavazi: Ufahamu mtindo wa mavazi wa kipekee wa Malkia

Yeye ni mmoja wa wanawake waliopigwa picha nyingi zaidi katika historia na katika miaka 70 iliyopita ameonesha nini maana ya kuvaa kama malkia.
Sio mtindo wala kuthubutu, lakini alama.
Amekuwa maarufu kwa nguo na makoti yake ya rangi zinazowaka vikienda pamoja na kofia inayofanana rangi na nguo, akinogesha na mkoba wake maarufu wenye umbo la mraba, akifuatiwa na kidani cha lulu (pearls) na broochi yenye vito. Inaonekana ni rahisi lakini mtindo wa Malkia umekuwa mpangilio wenye nguvu.
Ni mtindo ambao umeimarishwa na kuboreshwa zaidi ya miongo saba, ukisaidiwa na uhusiano wa karibu alionao na wabunifu na wavaaji wanaoaminika.
"Mitindo ya kifalme ni ya kufurahisha, yenye nguvu na iliyojaa maana," anasema mwandishi na mtangazaji wa mitindo ya kifalme Elizabeth Holmes. "Taswira yake ni sehemu kubwa ya urithi wake."
Kung'aa sana na kutatanisha
Malkia amekuwa wazi na wazo la jinsi alitaka kuwa, anasema mwanahistoria Michael Pick.
"Watu wamesema hajui kuhusu nguo, lakini hiyo si kweli. Yeye ni mjanja sana kuhusu kile kinachomfaa," Pick anasema.
Alipokuwa na umri wa miaka 20, Princess Elizabeth alianza kufanya kazi na mbunifu Norman Hartnell, uhusiano ambao alirithi kutoka kwa Mama wa Malkia. Sketi ndefu zenye kiuno kilichobanwa, iliyotokana na nguo ya Kifaransa, inavaliwa Pamoja na skafu nyeupe za manyoya na tiara za almasi.
Alipochukua nafasi yake mpya kama Malkia, Hartnell alimsaidia kumg'arisha katika hafla za serikali na ziara za kifalme akiwa amevalia gauni nyingi zilizobuniwa kwa vitambaa vya tulle na satin, zilizopambwa kwa mbegu za lulu, crystals na shanga.
Hartnell pia alimtengenezea nguo mbili muhimu zaidi ambazo ni- vazi lake la harusi na gauni alilovaa wakati wa kutawazwa kwake. Anaelezea mchakato huo kama ushirikiano. "Kwa vazi lake la kutawazwa Hartnell alibuni nguo karibu nane na alichagua kutoka katika vipengele vyote hivyo na kuifanya yake yake," Pick anasema.

Kwa Malkia, kufanya kazi na watu sawa haikuwa tu juu ya uaminifu, lakini pia ilikuwa muhimu. Hartnell alikuwa na nyumba kubwa zaidi ya mitindo ya nguo huko London pamoja na chumba kikubwa zaidi cha kudarizi, na kwa mtu aliyekuwa na shughuli nyingi kama Malkia ambaye alihitaji mamia ya mavazi mapya kila mwaka, ilimaanisha kuwa alikuwa na uwezo wa kubuni na kuzalisha kile alichohitaji.
Bado, ukubwa wa kazi hiyo ulimfanya pia kumuomba mbunifu Hardy Amies kufanya naye kazi, akianza na mavazi kwa ajili ya ziara ya Canada mnamo 1951.
Amies alimwongoza Malkia katika mwonekano wa kustaajabisha na usioeleweka kidogo, akiwa na nguo za mchana zilizomfaa na nguo maridadi za jioni. Kisha Ian Thomas alimchukua katika miaka ya 1970 na 1980 kwa mfululizo wa nguo za chiffon ya rangi angavu, zenye maua na pinde.
Kwa miaka 24 iliyopita mavazi yake yamebuniwa na kuzalishwa ndani ya nyumba na timu ndogo ya watu wapatao 10, wakiongozwa na mvalishaji wake binafsi nguo Angela Kelly.
Kila kipengee anachovaa Malkia ni cha kawaida, na kabla ya janga alikuwa akihudhuria shughuli zaidi ya 300 kwa mwaka. "Ni kazi kubwa," Pick anasema. "Hutaki Malkia kuvaa kitu ambacho mtu mwingine amevaa. Umma unatarajia kitu tofauti.
"Hartnell na Amies walimfanya kuwa wa kipekee, wakati Angela Kelly amekuwa mjanja na aliweza kuchukua mtindo wake wa binafsi na kumfanya kung'aa."
Kofia, Mkoba, viatu
Malkia anapojitokeza hadharani kila kipengele katika muonekano wake kimepangwa kwa uangalifu.
Vitambaa hukaguliwa ili kuona jinsi vinavyoteleza au vinavyoweza kuwa katika hali ya upepo. Rangi zinazong'aa, zilizochaguliwa kwa ajili ya msimu na tukio fulani, hutoa matokeo ya papo hapo ili asimame katika umati. Kofia humpa Malkia ambaye ana kimo kidogo urefu zaidi na kuangaza uso wake.
Anavaa viatu vya kisigino kifupi kinene - vilivyotengenezwa kwa mikono na kuvaliwa na Kelly mwenyewe ili kuhakikisha kuwa hakisumbui - na kila wakati kuna mwavuli ambao unafanana rangi na ambao huwa tayari kwa matumizi kama utahitajika kutokana na hali ya hewa ya Uingereza isiyotabirika.

Uvaaji huu wa sare huongeza faraja yake kwa siku ndefu, lakini pia husaidia kufafanua jukumu lake, anasema Elizabeth Holmes.
"Kazi yake ni kuwa na utulivu na uwepo thabiti. Nguo zake ni mchanganyiko wa kujua nini cha kutarajia lakini pia uwezo wa kushangaza na kupendeza.
"Hata katika nyakati za kawaida huvaa sare, akiwa na skafu yake ya kichwani na mabuti yake. Inaweka mwendelezo na pia inaonyesha kuwa hayuko kazini kamwe."
Bila shaka sehemu ya kuvutia zaidi ya muonekano wa Malkia ni kitu ambacho hakijabadilika katika utawala wake wote.
Lakini kutokana na mabadiliko ya rangi alipokuwa akizeeka na kupata rangi ya asili ya kijivu, imebakiza mikunjo miwili ya mawimbi ya nywele mbele na mawimbi yaliyopangwa kwa nyuma, mahususi kwa ajili ya kuvaa taji la malkia au kofia.
Ni mtindo wa kitamaduni wa nywele uliopendekezwa kwa wanawake wengi wa Uingereza wanaopenda mitindo katika miaka ya baada ya vita lakini wakati mitindo inabadilika Malkia amekuwa mwaminifu na ameendelea nao tangu wakati huo.
"Nywele zake ni za kawaida kabisa kwa mwanamke wa umri wake, lakini ni mwonekano wenye mamlaka, uliolainishwa na curls ili kuupa utulivu," anasema mtengenezaji wa mitindo ya nywele wa kifalme na mtu Mashuhuri Richard Ward. "Nadhani nywele zake zinajumuisha kile ambacho sisi sote tunathamini sana juu yake," asema. "Ni busara, vitendo na Ufahari."

Alama nyingine ya mtindo wa Malkia ni mkoba maarufu wa Launer anaoubeba kwa kuunyanyua kidogo mkononi.
Tofauti na mikoba mingine ya wabunifu wa hali ya juu na kifahari kama vile Hermes Birkin au Chanel 2.55, ambayo ni maarufu kwa wanawake wenye umri wa miaka 20 hadi 70, Launer haipendelewi na wasichana wadogo wanaopenda mitindo, anasema Charlotte Rogers, mtaalamu wa bidhaa za kifahari.
Mikoba hiyo inauzwa kwa takriban £1,500-£2,000, na Malkia anasemekana kuwa na mkusanyiko wa zaidi ya mikoba 200 ya rangi na mitindo tofauti.
Inaonekana katika mwaka wake wa Jubilee Malkia amekuwa na ushawishi zaidi kuliko hapo awali, ambayo sio jambo la maana kwa mwanamke katika miaka yake ya 90, anasema Rogers.
"Umri wake unafaa, mtindo kama vile bibi yangu alivyokuwa akivaa kwa hafla maalum na nadhani ana ushawishi kwa wanawake wakubwa," anasema. "Pini na broochi zilionekana kuwa sio za mitindo na sasa siwezi kununua vya kutosha. Zinauzwa haraka sana."
Ushawishi wa kifalme
Nguo za Malkia sio chaguo za mtindo tu bali pia taarifa za chapa, zilizojaa maana na ushawishi. Iwe amevaa gauni la vito au sketi ya tweed kila vazi linasema jambo kuhusu yeye na jukumu lake kama balozi na mtu mwenye kielelezo
"Kabati lake la nguo ni mawasiliano yake," anasema Matthew Storey, msimamizi katika Jumba la Kifalme la Kihistoria.
Anapaswa kuwa tayari, kuaminika na kitamaduni. Lakini pia "lazima ziwe za kustahili thamani ya kifalme," Holmes anasema.

"Ni sehemu ya kung'arisha taji. Akiwa kama Malkia nguo zake hutengenezwa kwa ajili yake yeye tu. Huwezi kuzinunua lakini inamaanisha unaweza kuziona na kuvutiwa."
Pia kuna jukumu la kidiplomasia au tukio linaloonyeshwa katika nembo au rangi anazovaa.
"Gauni maridadi la rangi ya waridi alilovaa kwenye sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya London 2012 lilichaguliwa kwa sababu halikuwa kwenye bendera yoyote ya taifa. Lilijitokeza lakini pia halikuonyesha utii wowote," Storey anasema.
Kama alama za chapa zingine pia anamaanisha vitu tofauti tofauti kwa watu.
"Kama kazi ya sanaa unatafsiri kwa njia yako mwenyewe," anasema Jeetendr Sehdev, mwandishi na mtaalam wa chapa mashuhuri.
"Je, tunamfahamu kweli yeye ni nani? Sina uhakika tunafanya hivyo. Lakini tunachojua ni kile anachomaanisha kwetu na mambo anayosimamia - nguvu zake, ujasiri na uhalisia wake - vinabaki kuwa muhimu hata miongoni mwa vijana."
Washiriki wachanga wa familia ya kifalme kama Camilla, Duchess wa Cornwall, na Catherine, Duchess wa Cambridge, wamehamasishwa na yeye, lakini Malkia anasimama mbali na juu, anasema.
Kuna mapenzi makubwa kwa jinsi anavyoonekana, Holmes anasema. Ana mtindo wa kusaini ambao utawakumbusha watu juu yake milele.
"Hakuna mtu mwingine anayevaa kama yeye," anasema. "Hiyo ni kazi yake na ni kubwa."
Taarifa zaidi kuhusu Malkia Elizabeth II wa Uingereza:
















