Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi wa Kenya 2022: Je ahadi za serikali ya Jubilee kwa Wakenya zimetimizwa?
- Author, Alutalala Mukhwana
- Nafasi, Mchambuzi Kenya
Mwaka wa 2013, tarehe 4 mwezi Machi , serikali mpya ya Jubilee, maarufu "Uhuruto ", ilichukua mamlaka baada ya uchaguzi mkuu.
Utawala huo mpya Uhuru Kenyatta pamoja naye Naibu Rais William Ruto, uliwapa matumaini chungu nzima wafuasi wao kwamba maisha ya Wakenya yangebadilika kuwa bora zaidi.
Wao Uhuru na mwenzake Wiilliam Ruto walionyesha ukuruba mkubwa hadharani na hilo likatia shani uhusiano wao na kuwaongezea matumaini maradufu Wakenya kuwa maisha yao yangelikuwa bora zaidi.
Kabla ya mwaka huo, kwa miaka mitatu mtawalia iliyotangulia, uchumi wa Kenya ulikua kwa viwango vya asilima 5.8,4.4 na 4.5.
Ahadi za serikali ya Jubille kwa Wakenya
Rais Kenyatta akihutubia wabunge Aprili 16 mwaka wa 2013, alianisha, ahadi za serikali yake ifuatavyo: Uongozi ulio wa haki, ukweli na uwazi, kulinda na kutetea haki na uhuru wa raia, kupambana na kumaliza ufisadi, kutekeleza na kufanikisha ugatuzi ili kutimiza katiba mpya, kazi milioni moja kwa vijana kila mwaka, uwajibikaji katika utendakazi kwa umma, barabara za lami pamoja na kusambaza nguvu za umeme na huduma za maji kwa raia wote.
Idadi kubwa ya raia wa Kenya ni vijana walio chini ya umri wa miaka thelathini na mitano, nao waliahidiwa viwanja kumi na sita kote nchini katika nyanja ya michezo, kando na nafasi za kazi milioni moja kila mwaka.
Uchaguzi Kenya 2022:Unaweza pia kusoma
UNAYOFAA KUJUA:Uchaguzi Kenya 2022: Je Naibu wa rais wa Kenya William Ruto anakabiliwa na changamoto gani katika kumteua naibu wake wa rais?
Je serikali ilifanikiwa kutekeleza ahadi zake kwa Wakenya?
Chambilecho wahenga, ahadi ni deni, na dawa yake ni kulilipa. Je, serikakali ya Jubilee, kwa hatamu zote mbili sasa, imelipia ahadi zake? Je, kupigwa kumbo Naibu Rais William Ruto, kumeadhiri vipi kulipwa au kulipwa deni hili.?
Baada ya hatamu ya kwanza, mwaka wa 2017 serikali ya Jubilee ilirejeshwa mamlakani kwa awamu ya pili. Mara hii, serikali ikaahidi kwamba sasa ajenda zake zingekuwa nne: Chakula tosha kwa raia wake, nyumba na makazi kwa bei nafuu, viwanda na mwisho matibabu kwa wote kwa bei nafuu.
Kwa kupunguza ajenda yake, ni ishara tosha kwamba serikali ilikuwa imeshindwa kutimiza ahadi za mwaka 2013? Mathalan: Nafasi za kazi milioni moja hazikupatikana, madai ya visa vya ufisadi bado yaliripotiwa hata kwa viwango vikubwa zaidi kama vile Eurobond, sakata ya Afya House, na kadhalika.
Viwango vya riba viliruka juu zaidi hivi kwamba raia wamekuwa wakitatizika kukopa mikopo ya kujiendeleza kibiashara. Deni la umma hivi sasa limeruka hadi trilioni 8.02 ikilinganishwa na trilioni 6.7 mwezi Juni 2013 miezi mitatu tu baada ya Jubilee kuchukua usukani.
Ukiukaji wa sheria
Rais wa taifa amelaumiwa kwa kukiuka amri za mahakama bila kujali athari zake kwa umma na swala zima la utiifu wa raia kwa sheria za nchi kwa mfano, licha ya mahakama kuamuru zaidi ya mara kumi kwamba Wakili Dkt. Miguna Miguna ni raia wa Kenya na kwamba angepaswa kurejeshewa cheti chake cha uraia wa Kenya na aruhusiwe kurejea Kenya, hilo limepuziliwa mbali hadi leo, kadhalika, rais na serikali yake alikataa kuwateua majaji fulani licha ya kwamba kisheria, huo uwezo haukuwa wake bali wa tume ya kuwaajiri majaji yaani "Judicial Service Commission".
Kuhusu ugatuzi, - licha ya kwamba huduma ya afya imeamriwa na katiba kuwa huduma ya serikali gatuzi, Rais and serikali amekatalia huduma hii na kukwamilia bajeti nzima ya Wizara ya afya Nairobi. Hii ni mifano michache tu inayoonyesha kwamba, kwa ujumla, safari ya serikali hii kutimiza ahadi zake kwa raia wa Kenya imekuwa na changamoto si haba.
Hata hivyo, mgalla muue lakini haki yake mpe! Serikali hii ilijizatiti kujenga barabara za lami kilomita elfu kumi nchini, japo maeneo fulani ya taifa yamefaidika mno kuliko mengine katika nyanja hii.
Barabara tajika mno ni ile inayotoka karibu na uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta hadi mtaa wa Westlands (Expressway).
Pili, katika hospitali za serikali za Ugatuzi, hospitali hizo zimeimarishwa na kupewa mitambo ya kisasa, ikiwemo mashine za kutibu saratani.
Vile vile, kupitia kwa mama taifa, Margaret Kenyatta, mpango wa kuwafikishia kina mama wajawazito huduma za matibabu umefanya makubwa katika kuokoa akina mama wanaojifungua. Mpango huu uliitwa "Beyond Zero Campaign, ukiwa na lengo la kuhakikisha kwamba hakuna hata mama mmoja mjamzito atakayeaga dunia kwasababu ya ukosefu wa matibabu ya kujifungua.
Huduma hizi ambazo ni za bure kujifungua kina mama zimewafikia kina mama wengi na hili limeimarisha hali nzima ya afya ya kina mama, japo kwa viwango vidogo .
Katika usafiri, reli ya kisasa, maarufu "SGR" imejengwa kutoka Mombasa hadi Nairobi na kurahisisha, pakubwa, usafirishaji watu na mizigo.
Serikali imeng'ang'ana katika usafishaji wa mitaa ya mabanda duni katika miji mikuu ya taifa, hususan Nairobi katika mitaa ya Kibra, Korogocho, Mathare na Nyalenda kule Kisumu. Katika mitaa hiyo, taa zimewekwa, barabara kupanuliwa na mitaro ya maji machafu pamoja na uzoaji taka kuimarsihwa. Hili limeleta hali bora ya usalama na maisha afadhali katika mabanda hayo.
Aidha, katika mitaa kadhaa, ujenzi wa nyumba za bei nafuu umefanyika japo kwa mwendo wa aste aste, kwa mfano katika mtaa mdogo wa Soweto, mtaani Kibra, nyumba mia nane kumi na mbili zimejengwa na kupewa wakaaji wa mtaa huo, kwa malipo ya pole na madogo madogo.
Marekebisho na uimarishaji wa uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta umefanywa kwa kiwango kikubwa. Marekebisho haya sasa yanawezesha uwanja huu kupokea wasafiri milioni 7.5 kutoka kwa kiwango cha awali cha wasafiri milioni 2.5. Hili limewezesha uwanja huu kuimarisha utalii na biashara zinginezo nchini Kenya na kwa hivyo kuimarisha uchumi wa Kenya kwa kiwango fulani.
Kuanzishwa kwa vituo vya kupeleka huduma za serikali karibu na raia maarufu "Huduma Centres" kumesaidia serikali kufikisha huduma zake karibu na raia. Hili limewapunguzia dhiki wanananchi katika kutafuta huduma muhimu za serikali.
Viwango vya stima nchini vimeimarishwa kupitia mradi wa kufikisha stima katika kila nyumba ya mkenya kwa jina "last mile connectivity". Kiwango cha stima cha "325 megawatts" kimeongezwa katika nyaya za stima Kenya kutoka kituo cha Olkaria 1 na 2 na 20MW kutoka vilima vya Ngong
Kuvunjika kwa uhusiano wa rais na naibu wake
Kwa ujumla, ni vigumu kutoa uamuzi fika iwapo kupigwa kumbo Naibu Rais William Ruto kumechangia kudhibiti au kudhoofisha uwezo wa serikali ya Jubilee kutimiza au kutotimiza ahadi zake.
Hata hivyo, Dkt. Ruto mwenyewe amenukuliwa mara si moja akidai kuwa asingelisukumwa kando ya serikali aliyoibuni kwa mikono yake, ahadi zote zingetimizwa. Amemlaumu rais Kenyatta pamoja na aliyekuwa Waziri mkuu Kenya, Bwana Odinga kwa kile anachokiona kisirani cha 'handisheki na mzaliwa wake BBI'.
Kwake yeye Dkt. Ruto, laiti wangesalia pamoja kama Uhuruto, serikali ingelitimza hata yale ambayo haikuweza kutimiza katika hatamu yao ya kwanza (2013-2017)
Yote tisa, la kumi ni kwamba, Serikali ya Jubilee, japo ilijaribu kutimiza ahadi zake, kwa sasa uchumi umedorora na hali si hali tena -gharama ya maisha imewazonga raia wa kawaida.