Uchaguzi Kenya 2022:Ukabila unavyotumiwa kama kigezo cha kuunda miungano ya kisiasa Kenya

    • Author, Joseph Kioko
    • Nafasi, Mchambuzi,Kenya

"Kwenye siasa hakuna maadui wa kudumu na urafiki wa kudumu, isipokuwa maslahi tu" William Clay.

Vyama vya kisiasa vinaundwa kwa madhumuni pekee ya kupata mamlaka kwa kushiriki katika mchakato wa uchaguzi huru na wa haki.

Miungano hii ya maslahi haya mahususi miongoni mwa vyama tofauti vya kisiasa ndiyo inayosababisha kuundwa kwa miungano na (au) muungano wa vyama mbalimbali.

Kwa upande wa Kenya , tangu kuanzishwa kwa siasa za vyama vingi nchini, somo moja ambalo vyama vya upinzani vimejifunza ni mpango wa kuungana ili kuweza kupata ushindi wakati wa uchaguzi mkuu.

Hamu ya kutaka kuchukua mamlaka imeunganisha vyama vya kisiasa ambavyo awali vilikuwa vikipinga miungano .

Uchaguzi Kenya 2022:Unaweza pia kusoma

Jinsi miungano ilivyoanza Kenya

Uanzishaji wa miungano umekuwa msingi wa siasa za Kenya tangu uchaguzi wa 2002. Katika uchaguzi wa 1992 na 1997, vyama vikuu vya vilifanikiwa kujizolea asilimia 60 ya kura dhidi ya chama tawala wakati huo , KANU kilichopata asilimia 35, ijapokuwa Kanu bado ilishinda uchaguzi huo.

Hatua hiyo ilizalisha muungano wa National Rainbow Coalition wakati wa uchaguzi wa 2002, muungano ulioleta Pamoja vyama vyote vikuu vya upinzani wakati huo dhidi ya mgombea wa chama cha KANU.

Katika uchaguzi wa 2007, mchuano wa kisiasa ulikuwa kati ya chama cha PNU cha Rais aliyekuwa madarakani Mwai Kibaki, ambacho kilikuwa muungano wa vyama vya kisiasa vinavyomuunga mkono na Orange Democratic Movement (ODM) chama cha kiongozi wa upinzani Raila Odinga, ambacho kilileta pamoja watu mashuhuri waliowakilisha makabila tofauti tofauti nchini.

Uchaguzi mkuu wa 2013 uliimarisha msingi wa ujenzi wa muungano miongoni mwa vyama tofauti vya kisiasa. Katika uchaguzi huu maalum, Chama cha National Alliance Party (TNA) cha rais Uhuru Kenyatta na kile cha United Republican Party (URP) cha William Ruto viliunda muungano dhidi ya Muungano wa Mageuzi na Demokrasia (CORD), uliomleta pamoja Mheshimiwa Raila Odinga wa chama cha Orange Democratic Party of Kenya (ODM) na Mheshimiwa Kalonzo Musyoka, wa Wiper Democratic Movement.

Uchaguzi wa 2017 pia ulikuwa na ushindani mkali kati ya chama tawala cha Jubilee , ambao ulikuwa muungano wa vyama vyote vilivyounga mkono rais Uhuru Kenyatta na chama cha National Super Alliance (NASA), uliokuwa muungano wa vyama vilivyounga mkono mgombea wa upinzani Raila Odinga.

Kwa hivyo, ujenzi wa muungano ni hatua nyeti ya kuhakikisha washirika wa uchaguzi uliopita hawatupiliwi mbali kwa lengo la kuingiza washirika wapya .

Tunapokaribia uchaguzi Mkuu wa Agosti, 2022, muundo wa kisiasa au miungano inachukua mtindo sawasawa na ilivyokuwa. Tunaweza kuhitimisha kwa urahisi kuwa miungano ya uchaguzi ya 2017 ya NASA na Jubilee haijaweza kusimamia vizuri miungano ya wahusika wapya.

Miungano mipya ilivyojikita

Kwa upande wa muungano wa NASA, kati ya washirika 4 wakuu, washirika wawili (Musalia Mudavadi na Mosses Wetangula) walijiondoa katika muungano wa NASA na wanamuunga mkono naibu wa rais William Ruto katika Muungano wa Kenya Kwanza, huku mshirika mwingine mkuu (Kalonzo Musyoka) hadi hivi majuzi alikuwa mbele ya Muungano wa One Kenya kabla ya kujiunga tena na muungano wa Azimio One Kenya.

Kwa upande mwingine Chama cha Jubilee, ambacho chenyewe kilikuwa muungano wa vyama vingi, pia kimegawanyika katikati kwa sababu ya mpasuko wa kisiasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto.

Rais Uhuru amedokeza hadharani kuwa anamuunga mkono aliyekuwa mpinzani wake NASA Mheshimiwa Raila Odinga chini ya muungano wa Azimio la Umoja, huku naibu rais akiunda muungano mpya chini ya bendera ya Kenya Kwanza.

Muungano wa Azimio ulileta pamoja chama cha ODM cha Raila Odinga, chama cha Wiper cha Kalonzo Musyoka, Chama cha Jubilee cha Uhuru Kenyatta, KANU ya Gideon Moi, NARC ya Charity Ngilu, Prof. Kibwana pamoja na vyama vingine vingi kote nchini; huku muungano wa Naibu Rais William Ruto Kenya Kwanza ukileta pamoja UDA , chama cha ANC cha Musalia Mudavadi, FORD-K ya Mosses Wetangula pamoja na vyama vingine vingi kutoka eneo la kati la Kenya.

Je Miungano inatokana na sera au Maslahi ya kikabila?

Miungano ya vyama vya kisiasa nchini Kenya kwa kiasi kikubwa ni zoezi la uhamasishaji wa kikabila kupitia kuunganishwa kwa wanaochukuliwa kuwa viongozi wa makabila , kinyume na miungano ya maadili ya kisera.

Kila kabila huangalia ni wapi kiongozi wake anaangaziwa vyema ndani ya chama au muungano wa vyama kama mshawishi mkuu wa jinsi ya kupiga kura.

Ugawaji wa nafasi muhimu kwa kiongozi/viongozi wa kabila wanaotambulika ni kipengele muhimu katika uundaji wa miungano, mara tu maslahi makuu ya mtu binafsi yanapoafikiwa basi maslahi ya jamii yanachukuliwa kuwa yametolewa.

Kwa upande wa Azimio, kwa kukidhi matakwa kibinafsi ya Kalonzo Musyoka, wapiga kura wa kabila la Akamba kutoka eneo la mashariki "wanahisi" kuridhika na kwa uwezekano mkubwa wangempigia kura Mheshimiwa. Raila Odinga, ambaye ndiye mgombea wa urais wa Azimio.

Hivyobasi kuridhika kwa viongozi hao wa makabila ni muhimu katika uundaji wa miungano nchini Kenya.

Je uamuzi wa mahakama kuhusu BBI uliathiri vipi miungano?

Uamuzi wa Mahakama ya juu zaidi mnamo mwezi Machi tarehe 31 uliobaditilisha mpango wa BBI, umetoa nafasi kubwa katika muungano wowote unaoundwa kwa msingi wa kugawana mamlaka.

Mchakato wa BBI, miongoni mwa masuala mengine, ulikuwa ni jaribio la kupanua mamlaka ya utendaji wa kitaifa kupitia kuanzishwa kwa nyadhifa kama vile Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu, ambazo zingesaidia kikamilifu katika kuzizawadi jamii tano kubwa nchini nchini kinyume na nyadhifa mbili (2) za Rais na Naibu Rais zilizopo kwa sasa.

Kuundwa kwa nyadhifa hizi za ziada kungehakikisha kuwa kuna mpangilio mpana zaidi wa ugavi wa mamlaka ndani ya muungano wowote utakaoundwa.

Je wadhfa wa naibu wa rais una muhimu gani uchaguzi huu?

Katika maandalizi ya uchaguzi wa 2022 nafasi ya Mgombea Mwenza na Naibu Rais aliyefuata (ikiwa ameshinda) ilikuwa imeshuka thamani kwa sababu ya unyanyasaji na kushushwa kwa hadhi na afisi ya sasa ya Rais Uhuru Kenyatta.

Naibu Rais kwa kipindi cha miaka minne (4) iliyopita amejipata nje katika serikali ambayo alikuwa mchangiaji mkubwa katika muundo wake.

Hata hivyo kutokana na kushindwa kwa pendekezo lililotarajiwa la BBI, nafasi ya mgombea mwenza itachukua jukumu kubwa sana katika muungano wowote utakaoundwa; anayepata nafasi hiyo atalazimika kuwa na mchango mkubwa katika jinsi kabila lake litakavyopiga kura.

Hivi sasa, miungano yote miwili ya Azimio na Kenya Kwanza inakabiliwa na mtanziko wa mgombea mwenza; kwa upande wa Azimio, swali muhimu ni iwapo muungano wa zamani kati ya Raila/Kalonzo ndio utakaowaslishwa na hivyo kuhatarisha kuwatenga washirika wapya walio na idadi kubwa ya upigaji kura ambayo imeletwa na Rais Uhuru Kenyatta, au muungano huo utaangazia kadi ya jinsi ya kike ambayo pia itatoka mlima Kenya?

Hili naamini ndilo tatizo la kisiasa ambalo muungano wa Azimio unapaswa kulishughulikia tunapoelekea Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2022.

Kwa upande wa muungano wa Kenya Kwanza, uongozi wake umekuwa ukisisitiz kwamba haukuegemea kwenye mgao wa nafasi kwa wachache, badala yake, ulikuwa wa kutatua changamoto za kiuchumi za siku nyingi zinazoikabili nchi na kwamba nafasi ya mgombea mwenza haikuwa na umuhimu wowote.

Hata hivyo kandokando kumekuwa na fununu kwamba vinara wake wakuu walikuwa wanahifadhi nafasi hiyo kwa wapiga kura wake wengi kutoka mlima Kenya.

Tangu kuingia kwa siasa za vyama vingi nchini Kenya mwaka 1992, uchaguzi Mkuu wa 2022 utakuwa ni uchaguzi wa kwanza ambapo eneo la mlima Kenya halitakuwa na mwanasiasa anayewania nafasi ya rais wa jamhuri, na hivyo Muungano wowote wa kisiasa unaoundwa utralazimika kutilia maanani muhimu wa eneo hilo lenye wapiga kura wengi.

Hivyobasi Muungano wowote utalazimika kutoa wadhfa huo kwa eneo hilo kwa lengo la kuvutia wapiga kura wake.