Fahamu uhusiano wa matumizi ya vipodozi vyenye kemikali na matatizo ya uzazi

Matumizi ya muda mrefu ya viambato vyenye sumu katika vipodozi yanaweza kusababisha matatizo katika mfumo wa uzazi ikiwemo kuharibika kwa mimba au kusababisha kutokuwa na uwezo wa mtu kushika mimba na hata matatizo ya mfumo katika mishipa ya fahamu kwa mtoto anayezaliwa.
Shirika la Viwango nchini Tanzania Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa hivi karibuni juu ya viambato ambavyo vinaruhusiwa kutumika kwa masharti ya kiasi maalumu , imebainika kwamba matumizi ya muda mrefu ya baadhi ya viambato yana athari katika mwili wa binadamu.
Viambato vilivyopigwa marufuku.
Matumizi yaliyozidi ya viambato vitatu katika kipodozi chochote na hatari kwa afya ya binadamu ambavyo huathiri mfumo wa uzazi.
Zinc pyrithione
Butyphenyl methypropional
Sodium hydroxymethylglycinate.
Viambato hivi vyote vinaharibu mfumo wa Uzazi kwa wanawake na wanaume kwa ujumla. Na viambato vipo katika baadhi ya vipodozi mbalimbali vilivyo katika mzunguko matumizi na vinaendelea kuuzwa katika baadhi ya maduka nchini humo.

Chanzo cha picha, TBS/INSTAGRAM
Madhara gani yanaweza kujitokeza katika mfumo wa uzazi?
Mtaalamu wa Masuala ya uzazi Daktari Manuwar Kaguta wa hospitali ya Aghakan Dar es Salaam anasema kuwa ni kitu ambacho kipo na watu wengi hawajakifikiria lakini ni vitu vinavyoleta athari kwenye mfumo wa homoni.
Athari hizi huathiri mayai ya uzazi, mbegu, homoni, uwezo wa mtu kushika mimba ambapo
"Mfumo huo ukipata athari unapelekea mayai yasitoke vizuri, yanatoka yakiwa na athari, mimba kutoka au unashindwa kushika mimba kabisa vitu ambavyo vinaonekana kama ni vidogo lakini mtu anapotumia muda mrefu vinajikusanya mwilini na kuleta matokeo kama hayo."
Kwa mujibu wa Dr Kaguta matatizo mengine yanayoweza kusababishwa na viambata hivi vyenye kemikali ni pamoja na kujifungua mtot mwenye uzito mdogo au mtoto kupata shida kwenye mfumo wa mishipa ya fahamu anapozaliwa.
Wananchi wanaelewa nini?
Viambata hivi vipo katika vipodozi vingi vinavyotumiwa na wananchi mbalimbali ambapo wengi wanasema kuwa wanajua vina matatizo kwenye ngozi tu na si masuala ya uzazi.
"Naambiwa kuna vipodozi vina kemikali hatari kwenye ngozi kwa uelewa najua ni muonekano wa nje tu vitaniharibu labda kuniletea vipele lakini kuhusu kuharibu kizazi hapo mi ni mgeni" anasema Enery Twambo mkazi wa Dar es Salaam.
"Ninavofahamu mtu akitaka kuwa mweupe kwa haraka labda akichoma sindano au kumeza vidonge ndio inaweza kumletea madhara kwnye kizazi lakini sio hivi vya kupaka tu, hivi vinaleta madhara kwenye ngozi. anasema Husna Dakhery mkazi wa Dar es Salaam

Nini kifanyike
Daktari Kaguta anasema ni vyema watumiaji wa vipodozi kusoma maelezo ya nje kabla ya kufanya maamuzi ya kununua bidhaa.
"Hatua ya mwanzo ni kuwa mwangalifu Kabla hujanunua asome lile box linavitu gani, watu wanasema ukija dukani unanunua brand name kwanza hafikirii kemikali kwanza. watu wasifikirie brand name kwanza, wafikirie ile bidhaa ina vitu gani" anasema Dr Kaguta
Anaelezea kwamba wauzaji na wazalishaji hawawezi kukwambia ni mbaya kiasi gani zaidi ya kukushawishi kununua bidhaa au atakwambia ni dozi ndogo tu.
Hata hivyo Shirika la Viwango nchini humo limetoa muda wa miezi mitatu kwa waagizaji, wasambazaji na wazalishaji wa vipodozi kufanya marekebisho ya kanuni za uzalishaji na ambao bidhaa zao zilisajiliwa kabla ya katazo wanatakiwa kusitisha uagizaji wa bidhaa zenye viambato.















