Vikwazo vya Ukraine: Ni changamoto gani zinazotarajiwa kwa uchumi wa Urusi?

A woman looking at pickled foods in a supermarket in Russia

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa mtazamo mmoja, Urusi hadi sasa imeweza kujikinga na kuporomoka kwa uchumi kufuatia uvamizi wake nchini Ukraine.

Imeathiriwa na vikwazo vilivyoletwa na nchi za Magharibi tangu Februari.

Mshtuko wa awali ulilazimisha soko la hisa nchini Urusi kufungwa kwa muda na kuona watu wakipanga foleni kwenye mashine za pesa, wakiwa na wasiwasi juu ya akiba yao.

Sarafu ya Urusi, ruble, hata hivyo, imerejea katika viwango vya kabla ya vita, kutokana na usimamizi makini wa benki kuu ya Urusi.

Uingiliaji kati wake ulijumuisha kupunguza kiwango cha pesa ambacho watu wanaweza kuhamisha nje ya nchi, na pia kulazimisha kampuni zinazouza bidhaa kubadilisha 80% ya mapato yao ya ngambo kuwa sarafu ya Urusi.

Nchi pia imeweza kuepuka kushindwa kulipa madeni yake ya nje.

Rais Putin amesisitiza kuwa nchi za Magharibi zimeshindwa katika kuikabili kwenye ''vita ya kiuchumi''.

Lakini Elina Ribakova, naibu mwanauchumi mkuu katika Taasisi ya Fedha ya Kimataifa, anasema ''viashiria'' hivi vya juu ''havina maana kubwa kwa maisha halisi''.

Watengenezaji chuma wa Urusi, watengenezaji kemikali na kampuni za magari tayari wanahisi mzigo mkubwa wa vikwazo vinavyolenga kulemaza juhudi za vita za Rais Putin.

Uchunguzi wa hivi majuzi wa biashara zaidi ya 13,000 uliofanywa na benki kuu ya Urusi ulionyesha kwamba wengi wanakabili matatizo ya kuleta bidhaa kama vile chipu ndogo, vipuri vya magari, vifungashio, au hata vifungo.

Uhaba wa malighafi au vipuri unalazimisha baadhi ya makampuni kufunga viwanda kwa muda au kutafuta mahali pengine.

Kampuni ya kutengeneza magari ya Japani Toyota, kwa mfano, ilisimamisha uagizaji wa magari nchini Urusi na kusimamisha shughuli zake katika kiwanda chake huko St Petersburg mwezi Machi, ikitoa mfano wa ''kuvurugika kwa mlolongo wa ugavi'' unaohusishwa na mzozo huo.

Chart tracking inflation across G7 countries, Russia and China since 2015

Mchumi ambaye pia ni msimamizi wa kampuni ya BlueBay Timothy Ash, anasema kuwa vikwazo kwa ujumla vimekuwa vikali zaidi kuliko wengi walivyotarajia.

''Nadhani athari za muda mrefu zitakuwa mbaya,'' anaiambia BBC, akiongeza kuwa ''Urusi ikiondolewa kwenye usambazaji kwa nchi za Magharibi kwa sababu ya kuwa mshirika asiyetegemewa '' kuifanya nchi hiyo kuingia kwenye mdororo wa kiuchumi.

Hata Benki Kuu ya Urusi imekiri kwamba makampuni yanapotafuta wasambazaji tofauti, kushughulikia kususia kwa makampuni ya meli au kushindwa kupata teknolojia wanayohitaji, nchi itakabiliwa na kipindi kigumu kiviwanda.

''Ukweli ni kwamba, Urusi itakuwa na uwezo mdogo wa kufikia masoko ya fedha, ukuaji mdogo, viwango vya chini vya maisha na gharama ya juu ya kukopa,'' Bw Ash anaongeza.

Bila shaka, athari hiyo ipo.

Warusi wengi wa kawaida, Bi Ribakova anasema, ''wanaishi katika kipindi ambapo ni hawajui kitakachofuata'', hasa linapokuja suala la usalama wa kazi.

Watu wengi hawajui kitakachotokea... Wanaweza kuwa bado wanaenda kwenye migahawa, wanaenda kazini na hawaoni mabadiliko mengi bado kwa sababu makampuni wanayofanyia kazi hayako wazi kuhusu mipango yao.''

line

TV, iliyojaa propaganda rasmi, bado ina nguvu zaidi kuliko friji tupu - jinsi Warusi wa kawaida wanavyokabiliana na hali hii

Shopper in Moscow

Chanzo cha picha, Getty Images

Na Anastasiia Stognei, ripota wa biashara, BBC Kirusi

Olga, 30, ni mfanyakazi wa benki ya Moscow.

Anajaribu kuendeleza viwango vyake vya maisha kabla ya vita lakini inazidi kuwa ngumu.

Kama Warusi wengi, inambidi amuulize rafiki yake anayeishi Ulaya amlipie Netflix na Spotify, baada ya Visa na Mastercard kuondolewa kimatumizi nchini Urusi.

Mapema mwezi huu, alitafuta nafasi ya ndege kwenda likizo Uturuki - mojawapo ya maeneo machache sana ya kigeni ambayo bado yapo wazi kwa Warusi.

Kabla ya vita tikiti ya ndege ingemgharimu rubles 15,000 (£170).

Lakini sasa amelazimika kulipa rubles 55,000 (£640).

Olga anaomba iwezekane kusasisha simu yake ya mkononi ya iPhone na MacBook akiwa nje ya Urusi - kampuni ya Apple pia imesitisha shughuli zake nchini humo.

Kwa Lyudmila mwenye umri wa miaka 79 kutoka Voronezh, jiji lililo kilomita 500 kusini mwa Moscow, mahitaji ya kimsingi yamekuwa ghali zaidi.

''Ninaenda sokoni mara moja kwa wiki. Kila wakati mambo yanazidi kuwa ghali. Mara ya mwisho maziwa yalipanda kwa robo tano, nyanya kwa mara 10.''

Dmitry, 33, ni mfanyabiashara wa masaji kutoka mji mdogo wa Siberia wa Rubtsovsk.

Kabla ya vita alikuwa na maisha mazuri, akitumia takriban 300 rubles (£3.50) kwa siku.

''Soseji, mkate, kwende kujivinjari katika eneo la maji moto mara moja kwa wiki na marafiki.''

Tangu Februari 24, wakati vita vilianza, gharama zake zimeongezeka kwa 50%.

Licha ya shida za kiuchumi, Dmitry anaunga mkono vita.

Anasema baadhi ya marafiki zake wanalalamika kuhusu bei hizo na pia kwamba haiwezekani tena kutazama wasanii wa filamu wa Magharibi katika kumbi za sinema.

Licha ya kila kitu, Warusi wengi bado wanaunga mkono vita hivi.

TV, iliyojaa propaganda rasmi, bado ina nguvu zaidi kuliko friji tupu.

line

Kampuni za Magharibi maarufu kama vile McDonald na Levi, zinaendelea kulipa maelfu ya wafanyikazi wa Urusi, licha ya kusimamisha shughuli nchini humo.

Lakini kuna hofu kwamba upotezaji wa kazi utaanza kuongezeka huku matumaini yakififia kuwa vita hivyo vitafikia kikomo hivi karibuni.

Meya wa Moscow Sergey Sobyanin alionya mwezi Aprili kwamba kazi zipatazo 200,000 ziko hatarini katika jiji hilo pekee, huku wachumi wakitabiri kwamba kiwango cha ukosefu wa ajira kote Urusi kinaweza kuongezeka hadi 7% ifikapo 2024.

Mashirika kadhaa ya ushauri yamewaondoa wafanyakazi nchini humo, huku ripoti za tovuti huru ya habari ya Urusi yenye makao yake Latvia Meduza zikipendekeza hadi wafanyakazi 5,000 wa Yandex waliondoka Urusi, huku baadhi wakitaja wasiwasi juu ya udhibiti wa kampuni hiyo kubwa ya kiteknolojia ya maudhui yanayohusiana na vita.

Kwa wale waliosalia, kupata riziki imekuwa vigumu mno.

Kuna wazo kwamba Warusi ni wapambanaji haswa lakini wameishi miaka 20 ya ustawi,'' Bw Ash alisema.

''Wamejua maisha mazuri.''

Shoppers walk by a shuttered Levi's store in Moscow

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Baadhi ya kampuni za Magharibi kama vile Levis na McDonald zinaendelea kuwalipa wafanyikazi wa Urusi licha ya kusimamisha shughuli zake nchini humo.

Baadhi ya kampuni za Magharibi kama vile Levi na McDonald zinaendelea kuwalipa wafanyikazi wa Urusi licha ya kusimamisha shughuli nchini humo ingawa kulikuwa na ripoti za uhaba wa vitu kama vile mafuta ya kupikia karibu na kuzuka kwa vita, rafu za maduka makubwa zinaripotiwa kujaa vizuri kwa sasa - lakini bidhaa ni za bei ya juu sana.

Nchi nyingi zinakabiliwa na kupanda kwa bei kutokana na janga hili.

Lakini katika uso wa uchumi unaodorora na kuvurugika kwa usambazaji wa bidhaa, wanauchumi wanatarajia kwamba mfumuko wa bei, ambao unafuatilia jinsi gharama ya maisha inavyobadilika kwa wakati, inaweza kugonga angalau 20% nchini Urusi mnamo 2022.

Chart showing unemployment rates in Russia

Bw Ash na Bi Ribakova wanakumbuka marafiki waliokuwa wakihangaika kupata dawa ya moyo au tezi dume, lakini wanasema ni Warusi maskini zaidi ambao watahisi zaidi gharama inayoongezeka na kufanya maisha kuwa magumu sana.

Rais Putin ameahidi kwamba mafao ya uzeeni na ukosefu wa ajira kwa wale wanaotatizika yataongezeka sambamba na mfumuko wa bei.

Na serikali ya Urusi ina njia yake ya kifedha, hata ikiwa na viwango vya juu vya vikwazo vilivyowekwa.

Bado ina uwezo wa kuuza mafuta na gesi nyingi - nguzo muhimu ya uchumi wake.

Kulingana na takwimu kutoka benki kuu ya Urusi, ilisafirisha bidhaa na huduma zenye thamani ya $58.2bn (£47.2bn) zaidi ya thamani ya uagizaji wake katika miezi mitatu ya kwanza ya 2022 - huku idadi hiyo ikiongezeka kutokana na bei ya juu ya nishati.

Ingawa Marekani imetangaza kupiga marufuku uagizaji wa nishati kutoka Urusi, Ulaya bado imegawanyika juu ya jinsi ya kumaliza utegemezi wa usambazaji wa Urusi.

Ulaya inapata takriban 40% ya gesi yake asilia kutoka Urusi, ambayo pia ni muuzaji mkuu wa mafuta wa umoja huo, lakini baadhi ya nchi zinategemea zaidi mafuta ya Kirusi kuliko nyingine, hivyo kupunguzwa kwa ghafla kwa usambazaji kunaweza kuwa na athari kubwa za kiuchumi.

Ingawa Urusi inaweza kuwa na fedha za kutosha kutoa ruzuku kwa maskini zaidi katika muda mfupi, na pia kulinda rouble, Bw Ash anasema mtazamo wa muda mrefu hauna uhakika zaidi.

Lakini anaongeza: ''Chochote kitakachotokea, iwe marufuku ya mafuta itaanzishwa ndani ya miezi sita au mwaka ... itakuwa pigo kubwa'', kwa uchumi uliotengwa na Magharibi.

Unaweza pia kusoma