Vita vya Ukraine : Nini kilicho nyuma ya maneno ya Lloyd Austin wamba Marekani inataka kudhoofisha uwezo wa kijeshi wa Urusi

Chanzo cha picha, EPA
Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin alielezea matumaini kwamba kupoteza katika Ukraine kungezuwia utawala wa Urusi kurudia vitendo vyao.
Aliongeza kuwa Ukraine inaweza bado kushinda vita iwapo itapata usaidizi inaouhitaji, na kusifu juhudi za jeshi lake.
"Tunataka Urusi kudhoofishwa kufikia kiwango ambacho haiwezi kufanya kile ilichofanya wakati wa uvamizi wa Ukraine. Tayari wamepoteza uwezo wa kijeshi na tunataka wasiwe na uwezo wa kurudia hili haraka sana'', mkuu wa Pentagon alisema.
Siku moja kabla, Austin alikutana na Rais Volodymyr Zelensky katika Kyiv. Mkutano ulidumu kwa zaidi ya saa tatu.
Austin na Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken, ambaye aliwasili pamoja naye katika mji wa mkuu Kyiv, ni maafisa wa ngazi ya juu zaidi wa Marekani kutembelea Ukraine tangu kuanza kwa vita.
Mwandishi wa BBC wa masuala ya kidiplomasia James Landale alibaini kuwa kauli za Austin zinazotoa wito wa kudhoofisha urusi zilikuwa za ukali usio wa kawaida kutolewa na Waziri wa ulinzi wa Marekani.
Kulingana naye, ni suala moja kuisaidia Ukraine kukabiliana na uchokozi wa Warusi, na mazungumzo mengine kuhusu udhoofishaji wa uwezo wa kijeshi wa ni suala jingine.
Kauli ya kushangaza ya Waziri wa ulinzi
James Landale , Mwandishi wa BBC wa masuala ya Kidiplomasia
Ziara ya Anthony Blinken na Lloyd Austin nchini Ukraine ilitimiza kikamilifu matarajio.
Kuonyesha uungaji mkono wa wazi unaoonekana. Tangazo la kurejea kwa wanadiplomasia wa Marekani nchini Ukraine. Ahadi ya usaidizi zaidi wa kijeshi.
Lakini ilikuwa ni kauli ya Austin kuhusu kuidhoofisha Urusi ambayo ilivuta usikivu zaidi.
Hii ni kauli ya ajabu kwa Waziri wa ulinzi wa Marekani.
Huenda anaweza kuwa anamaanisha vikwazo vikwazo vya Magharibi vitadhoofisha viwanda vya jeshi la Urusi.
Au je Waziri alimaanisha malengo mapya ya kijeshi kwa ajili ya nchi za Magharibi? Je inawezekana kuelewa maneneo yake katika njia ambayo inamaanisha kwamba kurefushwa kwa vita vya Ukraine kunaweza kuwa jambo la maana?
Hapana sio washirika wote wa magharibi watakubaliana na msimamo wa Lloyd Austin au uwazi wake.
Baada ya ziara yake mjini Kyiv, Waziri wa ulinzi wa Marekani aliwaambia wandishi wa habari katika mkutano nchini Poland kwamba maafisa mjini Washington bado wanaamini kwamba Ukraine inaweza kushinda mzozo iwapo ina silaha zinazofaa na usaidizi unaofaa.

Chanzo cha picha, EPA
Jumla ya msaada wa kijeshi wa Marekani uliotolewa kwa Ukraine tangu mwanzoni mwa uvamizi utafikia zaidi ya dola bilioni 3.7.
Kwa wiki mbili Rais Zelensky amekuwa akiwaomba viongozi wa Magharibi kuongeza uletwaji wa vifaa vya kijeshi, akiahidi kuwa vikosi vyake vitalishinda jeshi la Urusi iwapo watapokea ndege za mapigano na zana nyingine za kijeshi.
Katika kujibu, Urusi ilituma barua kwa Umoja wa Mataifa ikitaka usitishe upelekaji wa silaha nchini Ukraine. Hii ilitangazwa na balozi wa Urusi nchini Marekani Anatoly Antonov.
"Dola milioni 800 - hiki ni kiasi cha pesa ambacho Marekani inakitoa kwa ajili ya silaha zinazokwenda Kyiv. Hiki ni kiasi kikubwa sana cha fedha, hazichangii katika kutafuta suluhu la hali," alisema.
Kulingana na Antonov, kutumwa kwa silaha nchini Ukraine kwa Marekai ni jaribio la kuendelea uhasama hata zaidi, inasababisha hali kuwa mbaya hata zaidi, kuona vifo zaidi.
Anthony Blinken alitangaza kuwa sehemu ya wafanyakazi wa ubalozi wa Marekani wataanza kurejea Ukraine kuanzia wiki ijayo. Wanatarajiwa kuwa na makao yao katika Kyiv kwanza, huku kukiwa na mipango ya kufungua tena ubalozi wa Marekani wa kudumu mjini Kyiv.
Mapema, Ikulu ya White house ilitangaza kwamba Rais Joe Bidenatamteua mwanadiplomasia Bridget Brink kama balozi wa Marekani nchini Ukraine. Kazi hii imekuwa wazi kwa zaidi ya miaka miwili.
Blinken pia akiungwa mkono na msimamo wa kidiplomasia wa Marekani, akisema kuwa kwa njia hii Washington ninaweka shinikizo kwa utawala wa Rais Vladimir Putin.
"Mkakati ambao tumeutengeneza, uungaji mkono mkubwa kwa Ukraine, shinikizo kubwa kwa Urusi, mshikamano na zaidi yan chi 30 zinazoshiriki katika juhudi hii, vinazaa matokeo halisi ," Blinken alisema. " Na tunaona kwamba inapokuja katika kazi za kijeshi , Urusi inashinda, lakini Ukraine inafanikiwa ."
"Hatujui ni kwa muda gani vita hii itachukua, lakini tunajua uhuru wa Ukraine utadumu kwa muda mrefu kuliko Vladimir Putin. Na msaada wetu kwa Ukraine utaendelea hadi tutakapoona mafanikio kamili," alisema Blinken.
Akizungumza baada ya mkutano, Rais Zelensky alisema serikali yake inashukuru usaidizi "ambao haukutarajiwa" kutoka kwa Marekani na kuongeza "angependa kumshukuru Rais Biden binafsi na kwa niaba ya watu wote wa Ukraine kwa uongozi wake katika kuisaidia Ukraine."
Katika siku za hivi karibuni, Urusi imebadisha mkakati wake wa mashambulio dhidi ya jimbo la mashariki mwa Ukraine la Donbass, na vyanzo vya marekani vinaamini kuwa Urusi imepeleka zaidi ya batalioni 76, zenye mikakati maalumu nchini Ukraine.
Unaweza pia kusoma
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
- SILAHA:Mzozo wa Ukraine:Makombora ya stinger na silaha nyingine kali zinazotumiwa Ukraine












