Vita vya Ukraine: Urusi yaharibu miundombinu ya reli kuzuia silaha za kigeni kuingia Ukraine

Chanzo cha picha, Getty Images
Urusi iligonga miundombinu ya reli kote Ukraine siku ya Jumatatu kwa lengo la kuzuia usambazaji wa silaha za kigeni, huku Marekani ikitangaza kuwa itatoa silaha zaidi licha ya pingamizi la Moscow.
Takriban watu watano waliuawa na 18 kujeruhiwa katika mashambulizi ya Urusi katika eneo la Vinnytsia, kwa mujibu wa maafisa wa Ukraine.
Njia za reli pia hutumiwa na raia wanaopita kati ya miji au kujaribu kukimbia maeneo yenye migogoro. Mapema mwezi huu karibu raia 50 - wengi wao wakijaribu kuhamia maeneo salama - waliuawa na shambulio la roketi la Urusi kwenye kituo cha reli huko Kramatorsk.
Kwingineko siku ya Jumatatu, mipango ya njia za kibinadamu kuwaruhusu raia kuondoka kwenye kiwanda cha vyuma huko Mariupol ilishindwa.
Moscow ilisema kutakuwa na usitishwaji wa mapigano karibu na kiwanda hicho mapema alasiri lakini naibu waziri mkuu wa Ukraine alisema hakuna makubaliano yaliyofikiwa na kwamba Urusi inafanya kazi bila maafikiao ya pamoja.
Marekani inataka Urusi 'idhoofishwe'

Chanzo cha picha, EPA
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin alisema Marekani ilitaka kuona Urusi "ikidhoofika" ili isiwe tishio tena kwa mataifa mengine.
Alikuwa akizungumza nchini Poland siku moja baada ya yeye na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kukutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky mjini Kyiv.
Marekani ilitangaza nyongeza ya $713m (£559m) ya msaada wa kijeshi kwa serikali ya Ukraine na serikali nyingine 15 washirika wa Ulaya.
Mwandishi wa BBC wa masuala ya ulinzi Jonathan Beale anasema maneno ya Bw Austin yanaangazia ushiriki wa Marekani katika vita vya Ukraine.
Balozi wa Urusi mjini Washington alisema Moscow ilituma barua ya kidiplomasia kutaka kusitishwa kwa usambazaji wa silaha za Marekani kwa Ukraine.

Kutoroka kambi ya kizuizi ya Urusi

Chanzo cha picha, BBC/Jonny Dunstan
Mji wa Mariupol sasa uko karibu chini ya udhibiti kamili wa Urusi, na raia ambao wanataka kutoroka mara nyingi hujikuta katika "kambi ", ambapo hubaki kabla ya kuhamishwa.
BBC imesikia hadithi za kutisha za hali ndani ya kambi hizo, na kile kinachotokea kwa watu wanaoshukiwa na mamlaka ya Urusi kuwa na uhusiano na jeshi au serikali ya Ukraine.
"Ilikuwa kama kambi ya mateso ," Oleksandr mwenye umri wa miaka 49 alisema. Alikuwa akizungumza na BBC baada ya kutoroka eneo linalodhibitiwa na Urusi na kusafiri hadi Lviv magharibi mwa Ukraine.

Kushikilia mstari wa mbele huko Donbas - kwa miaka minane

Vikosi vya Ukraine vimekuwa vikidhibiti watu wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi huko Donbas tangu 2014 lakini mapigano ya hapa na pale sasa yamegeuka kuwa vita kamili.
"Imekuwa ngumu zaidi," Luteni Denys Gordeev alimwambia mwandishi wa BBC Jonathan Beale. "Tuna mashambulizi ya mabomu, mashambulizi ya roketi kila siku, wakati wote, kila saa."
Baada ya kuondoka Kyiv wiki tatu zilizopita, Urusi imeelekeza nguvu zake za kijeshi Mashariki mwa Ukraine kwa lengo la kuchukua eneo lote la Donbas.
Vikwazo vya michezo vinafaya kazi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Wiki iliyopita michuano ya tenisi ya Wimbledon ilitangaza kuwa wachezaji wa Urusi na Belarus watazuiwa kushiriki michuano hiyo.
Ndiyo hatua ya hivi punde zaidi katika orodha ndefu ya matukio ya michezo na mabaraza tawala kuweka vizuizi kwa timu za Urusi au watu binafsi, bila kujali kama wana uhusiano na serikali ya Urusi au la.
Lakini kuna uwezekano gani kwamba vikwazo kama hivi vinaweza kushawishi Urusi kukomesha uvamizi wake kwa Ukraine?
Katika nakala hii, ripota wa BBC World Service na mwanahistoria wa kriketi Mo Allie anazingatia historia ya vikwazo vya michezo, hasa jinsi vilisaidia kukomesha ubaguzi wa rangi katika nchi yake ya Afrika Kusini.
Unaweza pia kusoma
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
- SILAHA:Mzozo wa Ukraine:Makombora ya stinger na silaha nyingine kali zinazotumiwa Ukraine














