SpaceX: Je nyama inaweza kukuzwa kwenye anga la mbali?

A stock image of an astronaut eating a hamburger

Chanzo cha picha, Getty Images

Jaribio la kujua ukweli limekamilika hivi punde kwenye Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu.

Jeff Bezos na Elon Musk wote wanataka kutawala katika anga za mbali.

Nasa pia inajaribu kuweka watu kwenye uso wa vumbi wa Mirihi yaani Mars.

Lakini ikiwa wanadamu wanataka kuanzisha jamii kwenye mwezi au sayari, je watakula nini?

Majaribio mengi yamefanywa ili kuona kama mimea inaweza kustawi kwenye anga la mbali.

Na kufikia wiki iliyopita, jaribio jipya lilikuwa limeanza kufanyika kuona ikiwa seli za nyama zinaweza kukua.

Ilikuwa ni hatua ndogo ya majaribio ya kujaribu chanzo cha virutubishi kinachowezekana, hatua moja kubwa - angalau wanaojaribio wanamatumaini - kwa safari za siku zijazo za anga la mbali.

Majaribio hayo yalikuwa ndoto ya Aleph Farms, kampuni ya Israeli ambayo inajishughulisha na ukuzaji wa nyama kutoka kwa seli na inafanywa na timu ya kwanza ya wanaanga ya kibinafsi kutembelea Kituo cha Kimataifa cha Anga za Mbali.

Wakosoaji ingawa wanasema mbinu hiyo si dhabiti kwa wanaanga kutegemea - na kwamba kukuza nyama kwenye anga la mbalo haitakuwa rahisi ikilinganishwa na duniani.

Jinsi ya kukuza nyama

Jinsi ya kukuza nyama kutoka kwa seli - haswa kwa kiwango fulani - hata duniani sio rahisi.

Aleph Farms ni mojawapo ya makampuni kadhaa yanayojaribu kuzalisha ''nyama kwa njia ya kitamaduni'' lakini ndiyo ya kwanza kufanya jaribio hilo katika anga la mbali.

Kampuni hiyo haipendi kutumia neno ''nyama iliyokuzwa katika maabara'' - lakini kwa kweli mchakato huu hauonekani kama tuliozoea shambani.

Seli kutoka kwa ngombe (ingawa inaweza kuwa mnyama yeyote) zinalishwa vitu vinavyohitaji kukua, kama vile asidi ya amino na wanga.

Seli huongezeka hadi tishu za misuli zitengenezwe, na hatimaye inakuwa nyama ambayo unaweza kula.

Utaratibu huu unaitwa ''cultivation'' au ''proliferation'' kwa kiingereza.

Nyama hiyo hukuzwa katika matangi ambayo yanafanana zaidi na kile unachoweza kupata kwenye kiwanda cha pombe kuliko shambani.

Mzunguko wa maisha ya mnyama aliyelelewa kwa ajili ya nyama - yaani kuzaliwa, kuishi na kuchinjwa - umepitwa kabisa.

A steak grown by Aleph Farms

Chanzo cha picha, Aleph Farms

Maelezo ya picha, Mnofu wa nyama iliyokuzwa na kampuni ya Aleph Farms

Wenye shauku wanasema mchakato huo una uwezekano wa athari chanya kwa mazingira, na kupunguza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa methane kwa mfano.

Kwa nini nyama ikuzwe katika anga la mbali?

Zvika Tamari, ambaye anaongoza programu ya anga yay a mbali ya Aleph Farms, anasema wanasayansi hawajui kama hii inaweza kuigwa katika kiasi kidogo sana cha nguvu za uvutano.

''Tunajua kutokana na tafiti nyingi za awali za kisayansi kwamba fiziolojia na baiolojia hutenda kwa njia tofauti sana katika mazingira ya mvuto mdogo... Kwa hivyo, kwa kweli hatujui, hakuna anayejua, ikiwa michakato hii ya ukuzaji wa nyama inaweza kutokea katika anga za mbali.''

Kwa hivyo, mnamo tarehe 8 Aprili wanaume wanne walipoelekea kwenye anga la mbali kwa roketi ya SpaceX, kwenye misheni ya kwanza ya kibinafsi kwenye Kituo cha Kimataifa cha Anga zaa Mbali, walikwenda na kama kisanduku kidogo cha viatu lililobeba ndani yake seli za wanyama - na kila kitu wanachohitaji kuikuza.

Larry Connor, Eytan Stibbe, na Mark Pathy walizindua mradi huo kutoka kituo cha anga za mbali cha Kennedy huko Florida, wakiandamana na mwanaanga wa zamani Michael Lopez-Alegria.

Walitakiwa kurejea kwenye anga la mbali siku ya Jumapili tarehe 24 Aprili, ambapo seli hizo zitachambuliwa kwa karibu.

Lakini je, thamani ya mradi huu ikoje?

Hata kama jaribio limefaulu na imethibitishwa kuwa nyama inaweza kukuzwa katika anga la mbali, haimaanishi kuwa ni wazo zuri.

Kuna sababu maduka makubwa ya kufanya manunuzi hayajajazwa nyama iliyokuzwa kutokana na seli.

Kwa hakika, ingawa mamia ya mamilioni ya dola yameelekezwa kwenye sekta hii (Leonardo DiCaprio ni mwekezaji katika Aleph Farms) hiki ni chakula ambacho ni vigumu kukizalisha kwa kiwango kikubwa.

Aleph Farms pia bado inangoja idhini ya udhibiti nchini Israeli kabla ya kuanza kuiuz kwenye mikahawa.

Hiki ni chakula ambacho bado hakijajiimarisha duniani, licha ya anga za mbali.

Kuna shida zingine za kinadharia zaidi linapokuja suala la kukuza nyama kwenye anga la mbali.

La kwanza ni suala la utasa.

''Seli za wanyama hukua polepole,'' anasema David Humbird, mhandisi wa kemikali huko Berkeley.

''Kama bakteria au kuvu wangeingia kwenye tamaduni hiyo ingekua haraka sana kutoka kwa seli za wanyama na ingeshika kasi yenyewe ili usitengeneze seli za wanyama tena. Unatengeneza bakteria. Na lazima uitupe,'' anasema Bw Humbird.

Kampuni ya Farms inasema inaamini kuwa tatizo la utasa linaweza kushughulikiwa, hasa katika pale ambapo kiasi kidogo cha nyama kingehitajika kuzalishwa.

Lakini uchafuzi unaweza kuwa mbaya kwa jamii kwenye Mirihi - iko ni sawa na kushindwa kwa mazao.

Aleph Farms rendering of what a farm on Mars could look like

Chanzo cha picha, Aleph Farms

Maelezo ya picha, Kampuni ya Aleph Farms ikionyesha vile shamba linavyoweza kuwa katika anga la mbali.

Aleph Farms pia inahoji kuwa kusafirisha chakula kwenye anga la mbali ni gharama kubwa sana.

Takwimu zinatofautiana sana, hata hivyo makadirio ya Nasa kutoka 2008 yanaweka gharama kuwa $10,000 (£7,800) ili tu kupata pauni moja ya malipo kwenye mzunguko wa Dunia.

Ingegharimu mara nyingi zaidi kuleta ratili ya chakula kwa Mirihi.

''Mars iko umbali wa mamilioni na mamilioni ya kilomita. Na hivyo kuweza kuzalisha chakula chako ndani kwa ndani, kwenye tovuti ni faida kubwa, anasema Bw Tamari.

Bw Humbird hakubaliani kuhusu manufaa haya yanayoweza kutokea, hata hivyo.

''Seli hizo ambazo zenyewe hupandwa kwa nyenzo zinazoweza kuliwa zitakuwa sukari, asidi ya amino na maji. Na thamani ya kalori ya seli unazotengeneza daima itakuwa chini ya hiyo,'' anasema.

''Katika njia zuri zaidi unaweza kupata 25% ya kalori na kuzila kama chakula. Kwa hivyo swali ni, kwa nini ubebe kalori hizo zote kwenye anga la mbali ili kutumia tu 75% yazo?''

Lakini kuna mambo mengine ya kuzingatia wakati wa kupanga misheni za anga za mbali- kama vile afya ya akili ya wanaanga.

Karen Nyberg ni mwanaanga wa zamani wa Nasa ambaye alitumia miezi mitano na nusu kwenye Kituo cha Kimataifa cha Anga za Mbali, na sasa yuko kwenye bodi ya ushauri ya Aleph Farms.

Anasema chakula kina jukumu muhimu katika ustawi wa kisaikolojia wa wafanyakazi.

Chakula kinakuja kwenye mifuko hii mieupe ambayo inatubidi tu kutia maji, kama maziwa ya unga na kitu kama hicho ... nilikuwa nikitamani harufu ya vitunguu saumu na mafuta ya mizeituni, na ni kitu ambacho hatuna. Na kwa hivyo chochote tunaweza kurudisha nyumbani nadhani itakuwa nzuri.''

Kwa Bi Nyberg, chakula na mboga mboga ni muhimu ikiwa wanadamu wanatarajiwa kuwa mbali na dunia kwa miaka mingi.

Kwa hakika ikiwa ubinadamu una nia ya dhati ya kuwaweka watu kwenye Mirihi, jinsi ya kuwalisha wanaanga kwa vyakula vyenye virutubishi vingi ambavyo haviharibiki - na ladha nzuri - ni kitendawili muhimu na kigumu.

Ni jambo moja kuthibitisha nyama inaweza kupandwa katika anga la mbali - na ni jambo jingine kuthibitisha ni jambo la kuaminika kwamba kitakuwa cha kutosha, au mbadala wa chakula kicholetwa kutoka duniani.

Na Kampuni ya Aleph Farms ina matarajio makubwa, lakini kuonyesha kwamba nyama kweli inaweza kuzalishwa kwa kiwango kikubwa duniani ni swali muhimu zaidi kwa kampuni hiyo.