Meli ya kivita ya Urusi Moskva imezama -Wizara ya Ulinzi ya Urusi

Chanzo cha picha, Getty Images
Meli ya kivita ya Urusi ambayo iliharibiwa na mlipuko siku ya Jumatano imezama, wizara ya ulinzi ya Urusi imesema.
Moskva, Meli muhimu ya Urusi katika ya Bahari Nyeusi, ilikuwa ikivutwa hadi bandarini wakati "bahari yenye dhoruba" iliposababisha kuzama, kulingana na ujumbe wa wizara.
Meli hiyo ya kubeba makombora na wafanyakazi 510 ilikuwa ishara ya nguvu za kijeshi za Urusi, ikiongoza mashambulizi yake ya majini dhidi ya Ukraine.
Kyiv inasema makombora yake yaligonga meli hiyo ya kivita. Moscow haijaripoti shambulio lolote. Inasema chombo kilizama baada ya moto.
Moto huo ulisababisha mlipuko wa risasi za meli hiyo ya kivita, Urusi inasema, na kuongeza kuwa wafanyakazi wote baadaye walihamishwa hadi kwenye meli za karibu za Urusi katika Bahari Nyeusi. Haikutoa maelezo zaidi.
Baada ya kusema awali meli ya kivita ilikuwa inaelea, Alhamisi jioni vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vilitangaza habari kwamba Moskva ilikuwa imepotea.

Chanzo cha picha, MAX DELANY/AFP
"Wakati wakivutwa... kuelekea bandari iliyokusudiwa, meli hiyo ilipoteza usawa wake kutokana na uharibifu uliokuwa ndani ya meli wakati moto ulipozuka baada ya risasi kulipuka. Kutokana na hali ya bahari iliyochafuka, meli hiyo ilizama," shirika la habari la serikali Tass lilinukuu Wizara ya Ulinzi ya Urusi.
Maafisa wa kijeshi wa Ukraine walisema waliipiga Moskva kwa makombora ya Neptune yaliyotengenezwa na Ukraine - silaha iliyoundwa baada ya Urusi kutwaa eneo la Crimea mwaka 2014, na tishio la majini kwa Ukraine katika Bahari Nyeusi liliongezeka.
Afisa mkuu wa Ukraine alisema kuwa wafanyakazi 510 wangeweza kuwa ndani ya Moskva.
Katika siku ya kwanza ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine tarehe 24 Februari, Moskva ilipata sifa mbaya baada ya kukitaka kikosi kidogo cha askari wa mpaka wa Kiukreni wanaotetea Kisiwa cha Snake katika Bahari Nyeusi kujisalimisha - ambapo kwa kumbukumbu walitangaza ujumbe wa kukataa.
Meli hiyo ilijengwa katika enzi ya Soviet, Moskva iliingia huduma mapema miaka ya 1980. Meli hiyo iliwekwa chini katika mji wa kusini mwa Ukraine wa Mykolaiv, ambao umeshambuliwa kwa bomu na Urusi katika siku za hivi karibuni.
Meli hiyo ya kusafirisha makombora hapo awali ilitumiwa na Moscow katika mzozo wa Syria ambapo ilivipa vikosi vya Urusi nchini humo ulinzi wa majini.
Inaripotiwa kuwa ilikuwa na makombora 16 ya kuzuia meli ya Vulkan na safu ya silaha za kupambana na manowari pamoja na topedo.
Ikiwa shambulio la Ukraine litathibitishwa, Moskva yenye tani 12,490 itakuwa meli kubwa zaidi ya kivita kuzamishwa na hatua ya adui tangu Vita vya Pili vya Dunia.
Ni meli ya pili kubwa ambayo Urusi imepoteza tangu kuanza kwa uvamizi wake. Mnamo Machi, meli ya kutua ya Saratov iliharibiwa na shambulio la Ukraine katika bandari ya Berdyansk, Bahari ya Azov ya Kiukreni ilitekwa na Urusi.
Vita vya Ukraine: Taarifa zaidi:
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
- SILAHA:Mzozo wa Ukraine:Makombora ya stinger na silaha nyingine kali zinazotumiwa Ukraine













