Uber: Kwanini imesitisha huduma zake Tanzania?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mapema leo kampuni maarufu ya Uber inayotoa huduma za usafiri kwa njia ya mtandao ilitoa taarifa ya kusitisha huduma zake nchini Tanzania.
Katika taarifa yake Uber inasema kuwa kanuni za sasa za usafirishaji nchini Tanzania zimesababisha ugumu katika uendeshaji wa biashara hiyo
'' Kanuni za sasa za usimamizi wa sekta hii zimejenga mazingira ambayo si rafiki na zimekuwa changamoto kubwa katika uendeshaji wa biashara yetu, hadi pale muafaka utakapopatikana, hatutaendelea kutoa huduma za usafiri wa UberX, UberX Saver na UberXL nchini Tanzania'' ilisema taarifa hiyo ambayo ilitumwa kwa watumiaji wa huduma za Uber.
Mapema mwezi uliopita Bodi ya mamlaka ya usafiri wa ardhini nchini Tanzania (LATRA) ilitoa kanuni za uendeshaji wa tax za mtandaoni kutokana na mabadiliko ya sheria.
Mabadiliko hayo yalihusisha uthibiti wa tozo za nauli kwenye makampuni ya tax za mtandao kama Uber na makampuni mengine.
Bodi hiyo ilitoa kiwango elekezi cha mgao wa fedha kutoka kwa madereva kwenda kwenye kampuni za tax za mtandaoni, ni kiwango kilichowekwa haitakiwi kuzidi asilimia 15%.
Lakini pia iliweka kiwango cha nauli kwa safari, kiwango cha chini ikiwa ni shilingi 5000 za Tanzania na kwa kilomita moja shilingi 900.
''Sheria inatekelezwa kwakua na kanuni, sasa kuna kanuni za mwaka 2020 na zinaeleza jinsi tutakavyoweza kudhibiti tax, na sheria ya LATRA inasema ni lazima tudhibiti nauli na tozo na tunaanza na hili'' alisema Mkurugenzi wa LATRA Gilliard Wenge.
LATRA iliongeza kuwa kumekua na malalamiko mengi hususani kutoka kwa madereva wa tax za mtandaoni na viwango vya chini vya nauli.

Katika taarifa ya Uber inaeleza kuwa viwango hivi vipya pamoja na kanuni vinasababisha uendeshaji wa biashara yao nchini Tanzania kuwa mgumu.
Lakini hata hivyo wameeleza kuwa ikiwa kutakua na mazungumzo baina yao na serikali ya Tanzania basi wako tayari kutoa ushirikiano.
''Tuko tayari kushirikiana na mamlaka husika na kuwa na mazungumzo yatakayoleta tija na kujenga mazingira wezeshi.'' Ilisema taarifa hiyo.
Uber ilianza kufanya biashara nchi Tanzania mwaka 2016.
Kesi za Uber katika nchi nyingine
Madereva wa Uber kwa sasa wanachukuliwa kama watu waliojiajiri, ikimaanisha kuwa kisheria wanapewa ulinzi mdogo tu, hali ambayo kampuni hiyo yenye makao yake Silicon Valley ilitafuta kudumisha mzozo wa kisheria wa muda mrefu.
Kampuni hiyo inakabiliwa na hatua za kisheria katika miji kadhaa duniani kote na imekosolewa kuwa magari yake yanaongeza msongamano na kuzipokonya biashara teksi za kawaida.
Hapa kuna baadhi mifano ya makabiliano ya kisheria yanayohusu kampuni hiyo kote ulimwenguni:
UINGEREZA
Mnamo 2017, Usafiri wa London uliondoa leseni ya Uber katika mji mkuu, ikitaja mapungufu katika mbinu yake ya kuripoti makosa makubwa ya jinai na ukaguzi wa historia ya madereva.
Mnamo 2018, ilipewa leseni ya miezi 15 huko London baada ya kufanya mabadiliko ili kuboresha uhusiano na wakuu wa jiji.
Mnamo Septemba 2019, ilipokea leseni ya miezi miwili tu, ambayo muda wake uliisha muda mfupi baadaye
Kampuni hiyo ilinyang'anywa leseni yake ya kufanya kazi London mnamo Novemba 2019 kwa mara ya pili katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili kwani mdhibiti wa jiji alisema programu ya teksi iliweka usalama wa abiria hatarini.

Chanzo cha picha, EPA
MAREKANI
Mnamo Novemba 2019, mahakama ya New York ilitupilia mbali kesi ya Uber iliyopinga sheria ya jiji inayoweka kikomo cha idadi ya leseni za huduma .
Uber ilitaka mnamo Septemba 2019 kubatilishwa sheria mpya inayoweka kikomo cha muda ambao madereva wanaweza kutumia katika barabara za mitaa yenye shughuli nyingi za Manhattan bila abiria.
Huku wabunge wa Marekani wakitishia udhibiti mkali, Uber na Lyft Inc zilikwepa kikao cha bunge la Marekani mnamo Septemba 2019 kuhusu usalama, kazi na msongamano wa sekta hiyo.
Mnamo Septemba 2019 dereva wa Uber alishtaki kampuni hiyo kwa kuainisha vibaya madereva wake kama wakandarasi huru.
Mnamo Machi 2019 kampuni hiyo ililipa dola milioni 20 kusuluhisha kesi ya muda mrefu iliyoletwa na madereva wakidai kuwa walikuwa wafanyikazi na wana haki ya kulindwa hasa katikasuala la malipo.
AUSTRALIA
Mnamo Mei 2019, kampuni ya sheria iliwasilisha kesi ya pamoja kwa niaba ya maelfu ya madereva wa teksi na waliokodishwa, ikishutumu kampuni hiyo kwa kufanya kazi kinyume cha sheria na kuwadhuru kifedha.
UJERUMANI
Mahakama ya juu zaidi ya Ujerumani iliamua mnamo Desemba 2018 kwamba huduma ya magari ya 'limousine' ambayo haikutumika iliyotolewa na Uber lakini ikaondolewa kwenye huduma mwaka wa 2014 ilikuwa kinyume cha sheria, jambo lililorudisha nyuma kampuni hiyo katika uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya.
UHOLANZI
Mnamo Machi 2019, Uber ililipa takriban euro milioni 2.3 ($ 2.79 milioni) kutatua kesi ambayo iligundua kuwa ilikuwa imetoa huduma za teksi zisizo na leseni mnamo 2014-2015.
Wadhibiti wa Uingereza na Uholanzi mwaka jana waliitoza Uber faini kwa kushindwa kulinda taarifa za kibinafsi za wateja wakati wa shambulio la mtandaoni la 2016 lililohusisha mamilioni ya watumiaji.
INDIA
Mnamo Novemba 2018, nchi iliamua kuwa kampuni za teksi za kidijitali kama Uber na Ola hazikukiuka sheria za upangaji bei kufuatia malalamiko kuhusu mkakati wao wa kupanga bei.
AUSTRIA
Uber ilisimamishwa kwa siku mbili mnamo 2018 kwa sababu ya kesi ya kampuni ya teksi ya eneo hilo, lakini ilianza shughuli zake baada ya kufanya makubaliano.














