IPCC: Ripoti ya mabadiliko ya tabia nchi kuonya athari za ongezeko la joto duniani

Chanzo cha picha, Getty Images
Ripoti mpya kuhusu athari za mabadiliko ya tabia nchi inaweza kuwa tathmini inayotia wasiwasi zaidi ya jinsi kupanda kwa joto kunavyoathiri kila kitu kilicho hai.
Hii itakuwa ni ripoti ya pili kati ya tatu kuu kutoka kwa Jopo la Serikali mbalimbali kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa (IPCC) na ya kwanza tangu mkutano wa kilele wa COP26 wa mwezi Novemba mwaka uliopita.
Wanasayansi na maafisa watachapisha hitimisho lao tarehe 28 Februari mwaka huu.
Utafiti huo utajikita zaidi katika athari za kikanda pamoja na miji na jamii za pwani.
IPCC hufanya ukaguzi kwa utafiti wa hivi punde kuhusu ongezeko la joto kila baada ya miaka sita au saba kwa niaba ya serikali.
Watafiti wameundwa katika vikundi vitatu ambavyo vinaangalia sayansi ya kimsingi, ukubwa wa athari na njia za kushughulikia matatizo.
Kwa miji mingi mikubwa na nchi zinazoendelea, ripoti itaangazia kwamba kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa haihusu kupunguza uzalishaji na kufikia sufuri, bali ni juu ya kukabiliana na vitisho zaidi vya muda mfupi.
"Kwa hivyo ikiwa itabidi kushughulikii wimbi kubwa la wahamiaji, au tukio kubwa la mafuriko, hapo ndipo lengo litakapowekwa," alisema Mark Watts, mkurugenzi mtendaji wa kundi la C40, mtandao wa karibu miji mikuu 100 ambayo inashirikiana kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Chini ya mwavuli wa IPCC, wanasayansi wanaoshughulikia ripoti, ambao wote wanajitolea kwa kazi hii, wanapitia na kuandika maelfu ya nakala ili kufanya muhtasari wa matokeo ya hivi punde.
Kisha wanakutana na maafisa wa serikali ili kupitia matokeo yao mstari kwa mstari na, baada ya kufikia muafaka, muhtasari mfupi wa matokeo yao utachapishwa.
Utafiti huo pia utatoa vidokezo muhimu ambavyo vina uwezekano wa kupitishwa wakati ulimwengu unapozidi kukumbwa na ongezeko la joto, na madhara yakiwemo kuyeyuka kwa barafu ya Greenland.
Ripoti hiyo pia itaangalia baadhi ya suluhu za kiteknolojia kwa mabadiliko ya hali ya hewa.
Kwa ujumla itakuwa na mwelekeo mpana zaidi kuliko tu ya sayansi ya kile tunaweza kufanya kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ukiwa nyumbani kwa wakazi milioni 24, mji wa Lagos nchini Nigeria ndio wenye watu wengi zaidi barani Afrika - lakini ambao uko katika hatari kubwa ya mafuriko na kupanda kwa kina cha bahari. Kufanya hali kuwa mbaya zaidi ni tatizo la taka zinazokusanyika katika mito. Kukabiliana na suala hili kunaweza kuwa njia ya kusaidia jiji kukabiliana na mabadiliko yanayoletwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
"Moja ya mambo ambayo yanahitaji kubadilika huko Lagos ili kupunguza athari ya mafuriko ni kupata udhibiti wa mfumo wa usimamizi wa taka," kulingana na Mark Watts kutoka C40.
"Ripoti itazungumzia haki ya kijamii zaidi na maendeleo endelevu. "Hii ni kuhusu athari kwa watu, hatari wanazokabiliana nazo na mipaka ya kukabiliana na hali hiyo pia."

Chanzo cha picha, Getty Images
Mzozo juu ya maneno
Lakini wakati wanasayansi na maafisa wanakutana ili kufafanua maelezo ya mwisho, mzozo umeibuka juu ya matumizi ya kifungu cha maneno muhimu katika maandishi.
Kwa miaka mingi, nchi zinazoendelea zimekuwa zikijaribu kupata ulimwengu tajiri zaidi kujibu ndani ya mazungumzo ya hali ya hewa ya Umoja wa Mataifa kuhusu suala la "hasara na uharibifu".
Wanafafanua neno hili kumaanisha athari za mabadiliko ya hali ya hewa ambayo nchi haziwezi kukabiliana nayo, ikiwa ni pamoja na hali ya hewa kali kama vile dhoruba kuu lakini pia matukio ya kuanza polepole kama vile kupanda kwa kina cha bahari au jangwa.
Nchi tajiri kwa muda mrefu zimepinga dhana hiyo, zikiogopa kuwa zinaweza kuwajibika kisheria na kifedha kwa karne nyingi kwa usumbufu unaosababishwa na utoaji wa miaka mingini wa kaboni . Matokeo yake suala hili limekubwa na mgawanyiko mkubwa wa kisiasa ndani ya mazungumzo ya hali ya hewa duniani.
Katika ripoti hii mpya, wanasayansi wa IPCC wanatafuta kutumia toleo la neno lililorekebishwa kidogo, wakizungumzia "hasara na uharibifu," ambayo wanasema ina maana tofauti, isiyo ya kisiasa.
Lakini maafisa kutoka serikali kadhaa tajiri zaidi wanaohudhuria kikao cha kuidhinishwa wamepinga, wakihofia kwamba iwapo wazo hilo litaonekana katika ripoti muhimu, litatoa uungaji mkono kwa nchi hizo zinazotaka "hasara na uharibifu" kuwa kipaumbele cha mazungumzo ya kimataifa.
Kisha ripoti hii itasisitiza kwamba ikiwa hatua za haraka zitachukuliwa kapunguza gesi chafuzi na matumizi ya kusaidia watu kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa yakiongezeka, basi hatari mbaya zaidi zinaweza kuepukwa.
Lakini matumaini haya yanapaswa kupimwa dhidi ya ukweli wa siasa, kulingana na mwenyekiti mwenza Prof Hans-Otto Pörtner.
"Ujumbe mmoja muhimu umetoka katika ripoti za awali - msukumo wa kisiasa, katika suala la hatua za hali ya hewa, ni kikwazo kwa mustakabali endelevu."















