Haile Gebrselassie wa Ethiopia na Feyisa Lilesa wako tayari kujiunga na vita vya Tigray

Chanzo cha picha, Getty Images
Mashujaa wa Olimpiki wa Ethiopia Haile Gebrselassie na Feyisa Lilesa wanasema wako tayari kwenda mstari wa mbele katika vita dhidi ya vikosi vya waasi.
Tangazo lao linakuja baada ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kusema atakuwa mstari wa mbele kuongoza vita.
Waasi wa Tigray wanasema wanaelekea mji mkuu wa Addis Ababa.
Ujerumani na Ufaransa ni nchi za hivi punde kuwashauri raia wao kuondoka Ethiopia, huku taharuki ya kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe ikipanda.
Siku ya Jumanne mjimbe wa Marekani katika eneo hilo Jeffrey Feltman alionya kuwa maendeleo ya muda ya kidiplomasia kuelekea kumaliza mzozo huo yanahatarishwa na matukio ya kutisha mashinani.
Waasi hao mapema wiki hii walisema wamechukua udhibiti wa Shewa Robit, mji ulioko umbali wa kilomita 225 kaskazini mashariki mwa Addis Ababa.
Madai hayo hayajathibitishwa.
Huku Bw Abiy akienda kuongoza juhudi za vita, naibu wake, Demeke Mekonnen Hasse, alikuwa amechukua jukumu la shughuli za kawaida za serikali, msemaji alinukuliwa na vyombo vya habari vinavyohusishwa na serikali akisema.
Tangazo la Bw Abiy limeimarisha usajili jeshini, huku mamia ya wanajeshi wapya wakihudhuria sherehe, iliyoadhimishwa kwa nyimbo za kizalendo, mjini Addis Ababa siku ya Jumatano.
Hapo awali, Gebrselassie, 48, alinukuliwa na televisheni ya taifa akisema kuwa uamuzi wa Bw Abiy kwenda vitani "unatarajiwa kutoka kwa kiongozi anayeipenda nchi yake".
"Nipo tayari kufanya lolote linalotakiwa kwangu ikiwa ni pamoja na kwenda vitani," alisema.
Gebrselassie anachukuliwa kuwa shujaa nchini Ethiopia, na maoni yake yalionekana kama jaribio la kukusanya uungwaji mkono wa umma nyuma ya juhudi za vita.
Wakati wa maisha yake ya miaka 25 kama mwanariadha, alishinda medali mbili za dhahabu za Olimpiki, ushindi nane wa Ubingwa wa Dunia na kuweka rekodi 27 za ulimwengu.
Alitangaza kustaafu riadha mnamo 2015.
Akielezea kuunga mkono vita hivyo, Feyisa, 31, alinukuliwa na tovuti ya shirika la habari la Fana inayoshirikiana na serikali akisema kuwa Bw Abiy amefanya "uamuzi sahihi" kwa kusema atakwenda vitani kukabiliana na waasi.
Aliongeza kuwa yeye pia alikuwa tayari kupata msukumo kutoka kwa "ushujaa wa mababu zangu" na kwenda mstari wa mbele "kuokoa nchi yangu".
Mwanariadha huyo alishinda medali ya fedha katika mbio za marathon katika michezo ya Olompiki ya Rio mwaka 2016.

Chanzo cha picha, AFP
Alipata umaarufu kwa kuinua mikono yake ikiwa imepishana kana kwamba imefungwa pingu ili kuvutia tahadhari ya kimataifa kuhusu ukandamizaji dhidi ya waandamanaji wanaodai mageuzi ya kisiasa nchini Ethiopia.
Tigray People's Liberation Front (TPLF) kilikuwa chama kikuu serikalini wakati huo.Kufuatia maandamano hayo, Bw Abiy alikua waziri mkuu na TPLF ikapoteza udhibiti wa nchi iliyokuwa imeshikilia kwa miaka 27.
Baadaye ilirejea kwenye ngome yake ya Tigray, ambako ilianzisha uasi Novemba mwaka jana baada ya mzozo mkubwa na Bw Abiy kuhusu mageuzi yake.
Vita hivyo vimezua mzozo mkubwa wa kibinadamu, na kusababisha maelfu ya watu kupoteza maisha, mamilioni kutoka makwao, na laki kadhaa katika hali kama ya njaa wakati mashirika ya misaada yanapambana kufikisha chakula katika maeneo yaliyoathiriwa na vita.
Uchambuzi
Matarajio ya baadhi ya wanamichezo wanaoheshimika zaidi wa Ethiopia wanaoelekea kwenye mstari wa mbele kupigana kunaashiria kitu kikubwa na cha nguvu kuhusu hali ya Addis Ababa na kwingineko.
Wakati wa mzozo mkali, Waethiopia wengi wanasiamama na waziri mkuu, na wana nia ya kutekeleza jukumu lao katika kukuza uungaji mkono wa umma kwa kampeni ya kijeshi ambayo imekumbwa na vikwazo visivyoweza kupingwa katika miezi ya hivi karibuni, ingawa mengi hayajafichuliwa kuhusu takwimu ya majeruhi na kasi ya uwanja wa vita.
Ni wazi watu wengi wanaona tishio la kijeshi linaloletwa na tplf na washirika wao kama hali halisi kwa Ethiopia.
Zaidi ya hayo ni chuki kubwa ya TPLF yenyewe, ambayo inatokana na miongo yake ya kuongoza serikali ya kitaifa ya kimabavu. Lakini kuna zaidi ya hilo.
Waziri Mkuu ametaka kuionyesha nchi yake kama mwathirika, sio tu wa uvamizi wa Tigray, lakini njama kubwa ya kimataifa iliyopangwa kudhoofisha Ethiopia na kuiadhibu kwa madai, kupinga maslahi ya ukoloni wa Magharibi katika bara.
Vyombo vya habari vya Magharibi vinaonyeshwa kama waungaji mkono kwa shauku wa nadharia hiyo ya njama - moja ambayo inaonekana kupata uaminifu mkubwa katika nchi inayojitahidi kuelezea jinsi kundi la waasi lingeweza kupiga hatua ya kushangaza.

Umoja wa Afrika unaongoza juhudi za kupata mwisho wa upatanishi katika mzozo huo, lakini hakuna upande ambao umejitolea kushuriki katika mazungumzo.
Siku ya Jumanne, wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani ilisema raia wake wanapaswa kuondoka kwa safari za kwanza za ndege za kibiashara, huku Ufaransa ikiwataka raia wake kuondoka nchini humo "bila kuchelewa".
Wakati huo huo hati ya ndani ya usalama ya Umoja wa Mataifa ilisema "wanafamilia wanaostahiki wa wafanyikazi walioajiriwa kimataifa" wanapaswa kuondolewa ifikapo tarehe 25 Novemba.
Hapo awali Marekani na Uingereza zilitangaza kuwa wanawaondoa wafanyakazi wa kidiplomasia wasio wa muhimu, na kuwaambia raia wengine kuondoka.
TPLF wanasonga mbele kuelekea Addis Ababa kwenye barabara kuu ya A2 hasa kusini zaidi kuliko Kemise.

Pia uanweza kusoma:













