Ni wakati wa waarabu kutawala soka duniani?

d

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mohammed bin Salman, mwenyekiti wa PIF, wamiliki wapya wa Newcastle United

Leo Newcastle United ya England ni moja ya vilabu tajiri kabisa duniani. Imenunuliwa wiki iliyopita na Saudi Arabia kupitia mfuko wake wa "Public Investment Fund (PIF) kwa thamani ya £300m na kuhitimisha miaka 14 ya umiliki wa Mike Ashley.

Ununuzi huo wa waarabu hao wenye utajiri wa zaidi ya £320 billion umezua gumzo na makelele, wengi wakiuona haujakaa sawa, kufuatia rekodi ya masuala ya haki za binadamu huko Saudi Arabia.

Inadaiwa vilabu kadhaa vya ligi kuu England vilijaribu kuzuia ununuzi huo huku Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International likataka kukutana na vilabu vya England kuhusu ununuzi huo. Lakini hilo halizuii kuona dhamira ya waarabu hao kwenye soka. Sasa Newcastle inaungana na vilabu kadhaa duniani vinavyomilikiwa na mabilionea wa kiarabu na kuibua swali kubwa, Je ni wakati wa waarabu kulitawala soka la dunia?

1: Kununua vilabu vikubwa vya soka Ulaya 169025

Mpira ni pesa, vilabu vingi sasa vinawekeza fedha nyingi katika miundo mbinu yake, utawala na kwa wachezaji. Ili kufanikisha hayo unahitaji wamiliki wenye uwezo mkubwa. Haishangazaji kuona leo Klabu kama Chelsea, PSG, Manchester City, zikifanya vizuri kuliko klabu kama Arsenal ama Nottigham Forest ambazo zilikuwa moto wa kuotea mbali wakati wa utawala wao kwenye soka la England.

Kinachowasumbua kuwa wababe leo ni fedha, sasa kumekuwa na vilabu vingi vyenye wamiliki wenye fedha, wengi wao ni waarabu walioamua kununua vilabu na kuvimiliki.

Klabu ya Paris Saint-Germain (PSG), iliyokuwa inamilikiwa awali na mbunifu wa mavazi wa Ufaransa, Daniel Hechter, kwa sasa inamilikiwa na Qatar Sports Investments.

a

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Nasser Al-Khelaifi wa Qatari, Mmiliki wa PSG alifanikisha kumsajili Messi katika dirisha la usajili msimu huu

PSG ilikua haifanyi vizuri, kuingia kwa Qatar Sports Investments mwaka 2011 chini ya mwenyekiti wake Nasser Al-Khelaifi wa Qatari, leo PSG ni tishio, ikisajili nyota wakubwa kama Zlatan Ibrahimovic, Thiago Silva, Cavani, na David Luiz! Kwa sasa ina Lionel Messi, Kylian Mbappe, Neymar na nyota wengine wakubwa.

Bilionea Farhad Moshiri, mwarabu kutoka Iran anaimiliki Everton tangu mwaka 2016, ingawa bado haijawa tishio sana, lakini ni miongoni mwa timu zinazoleta ushindani katika ligi kuu England.

Manchester City inamilikiwa na waarabu wa Abu Dhabi United Group toka 2008 hakuna mwenye mashaka kuhusu kiwango cha Man City na utawala wake kwa sasa kwenye soka la England. Ni miongoni mwa klabu zinazopigiwa chapuo kwenye ligi ya mabingwa Ulaya.

Vilabu kama Malaga CF inamilikiwa na mwarabu Sheikh Abdullah Al Thani kutoka familia ya kifalme huko Qatari, Hull City iko chini ya mwarabu wa Misri Assem Allam ni miongoni mwa vilabu vinavyoonyesha dhamira ya waarabu kuwa sehemu kubwa ya soka la dunia.

2: Ligi za Uarabuni ni kivutio sasa kwa wachezaji wenye majina makubwa Ulaya

a

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, James Rodriguez amehamia klabu ya Al Rayyan Club mwezi uliopita akitokea Everton

Kwa sasa ligi za Uarabuni zimekuwa zikivutia wachezaji wengi wakubwa kutoka timu kubwa za Ulaya. Haishangazi wachezaji kama Éver Banega (Al-Shabab), Christian Atsu (Al-Raed), Sebastian Giovinco, aliyeshinda mataji mawili ya ligi kuu akiwa na Al-Hilal, Wilfried Bony (Al-Ittihad - 2019-20), Odion Ighalo (Al-Shabab - 2020), Ahmed Musa (Al-Nassr - 2018-21) na M'Baye Niang (Al-Ahli - 2020-21), ni miongoni mwa wachezaji wachache wenye majina kucheza uarabuni.

Mchezaji mwingine mkubwa kuhamia uarabuni kwenye ligi ya Qatari ni James Rodriguez anayeichezea klabu ya Al Rayyan Club. Ukiacha hao wapo pia makocha wenye majina majina makubwa kwenye soka la Ulaya kama nahodha wa zamani wa Barcelona, Xavier Hernández Creus aliyewika sana na timu ya taifa ya Hispania. Kwa sasa Xavier kocha wa mabingwa wa ligi ya Qatar Stars League, klabu ya Al Sadd.

3: Kombe la dunia 2022 kufanyika Uarabuni ni mkakati?

Mwaka 2010 Shirikisho la soka duniani FIFA, iliitangaza Qatar kuwa mwenyeji wa fainali za kombe la dunia kwa mwaka 2022. Na kuwa nchi ya kwanza kutoka uarabuni kuandaa kombe la dunia.

Qatari ilizishinda nchi za Japan/Korea zilizotaka kuandaa pamoja, Marekani na Australia iliyokuwa inapewa kipaumbele. Serikali, familia za kifalme na mabilionea wa taifa hilo kwa miaka 10 wameshirikiana kuhakikisha nchi hiyo inaanda vizuri mashindano hayo makubwa kabisa ya soka duniani.

d

Chanzo cha picha, Qatar

Maelezo ya picha, Uwanja wa Lusail, Qatar

Uwepo wa mashidano hayo umeleta hamasa kubwa katika nchi za kiarabu, ukiacha viwanja vya kisasa vilivyojengwa kama Lusail, utakaochezewa fainali na wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 80,000... kumekuwa na hamasa kubwa ya soka kwa vijana.... na tayari wachezaji wengi vijana wameanza kwenda Ulaya kucheza timu za watoto.

Wafuatiliaji wa soka wanasema huu ni mkakati utakaolipa kwa waarabu.

Huenda miaka 10 ijayo utawala wa waarabu kwenye soika la dunia utajidhihirisha kama wataendelea kumiliki timu, kuboresha ligi yao na kuvutia wachezjai wakubwa na na kuandaa matukio makubw aya kisoka kama mashindano ya kombe la dunia.