Virusi vya Corona: Fahamu dhana nne potofu dhidi ya chanjo za corona Tanzania

Workers in Dar es Salaam prepare face shields

Chanzo cha picha, Reuters

Chanjo za corona kwa ajili ya raia wa Tanzania zinaanza kutolewa leo kwa watu wa makundi maalumu wakiongozwa na Rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan.

Hii ni hatua muhimu katika mapambano dhidi ya virusi hivyo ambavyo kama ilivyo katika nchi nyengine vimeathiri maisha ya watu kwa kiwango kikubwa.

Kama ilivyo katika maeneo mengine duniani, mwanzo wa mchakato wa chanjo Tanzania umekumwa na taarifa nyingi za upotoshaji. Toka siku ya Jumamosi ya Julai 24 ambapo chanjo hizo ziliingia Tanzania kutoka Marekanikupitia mpango wa Covax, taarifa potofu zimekuwa zikishika kasi mitandaoni kama moto wa nyika.

Maelezo ya video, Watanzania wana maoni yapi kuhusu kupokea chanjo ya Corona?

Wananchi wengi wamekuwa wakitoa maoni mitandaoni kulingana na taarifa za kipotoshaji zilizotapakaa. Baadhi wanakariri maneno ya rais aliyepita wa nchi hiyo hayati John Magufulia ambaye msimamowake wa mashaka juu ya chanjo hizo aliuweka wazi kabla ya kifo chake mapema mwaka huu.

Hizi ni dhana nne potofu ambazo zimekuwa zikiorodheshwa kwa wingi zaidi:

'Chanjo za corona zimewahishwa, tunatumika kwa majaribio'

Watu wengi wamekuwa wakisema kuwa chanjo za corona si za kawaida na hivyo wanamashaka na ufanisi wake kwa kuwa zimewahi kuingizwa katika matumizi bila kufuata utaratibu wa kawaida wa kisayansi.

TZ

Chanzo cha picha, Getty Images

Utaratibu unaokusudiwa hapa ni ule uliozoeleka ambao huchukua miaka ya majaribio kuanzia kwa Wanyama na binadamu na kisha ubora na ufanisi wake kuchunguzwa kwa kina.

Kwa utaratibu huo wa kawaida, huchukua baina ya miaka mitano mpaka 10.

Lakini hoja hii kwa mujjibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) haina mashiko. Shirika hilo ndilo lenye dhamana ya kusimamia masuala yote ya kiafya duniani ikiwemo kupasisha ufanisi wad awa na chanjo.

Wataalamu wa WHO wanasema kwamba chanjjo zote zilizopitishwa za corona kufikia sasa ni salama kwa matumizi ya binadamu na zimefanyiwa utafiti na uchunguzi wa kutosha wa kisayansi.

"Ushirikiano wa kisayansi wa hali ya juu ambao haukuwahi kushuhudiwa hapo kabla umewezesha utafiti, utengenezwaji na upitishwaji wa chanjjo katika kipindi kifupi Zaidi kilichovunja rekodi - yote hayo yalifanyika kwa kasi ili kukidhi mahitaji makubwa na ya haraka ya ulimwengu huku hatua zote za usalama na ubora zikifuatwa," inaeleza taarifa ya WHO kuhusu hoja ya uharakishwaji wa chanjo.

WHO pamoja na vyombo vingine vya kikanda na baadhi ya mataifa wanaendelea kusimamia na kuchunguza matumizi ya chanjo hizo na kutatua changamoto zote zinazojitokeza ili kuhakikisha usalama wa watumiaji unalindwa.

'Siumwi, sichanjwi'

Baadhi ya watu mitandaoni n ahata waliohojiwa na BBC wanadai kuwa hawaumwi ama hawajawahi kupata corona hivyo hawana haja ya kuchanja.

Jambo la kwanza muhimu hapa kuelewa ni kuwa, si kila anayepata corona huonesha dalili, ama hupata madhara makubwa ambayo yanaweza kusabishwa kulazwa. Lakini, hata ikiwa hautaonesha dalili ama kupata madhara makubwa bado unaweza kumuambukiza mtu mwengine ambaye anaweza kudhurika na virusi hivyo na hata kupoteza maisha.

Wazziri wa Afya Tanzania Dorothy Gwajima kushoto

Chanzo cha picha, State Department/Twitter

Maelezo ya picha, Wazziri wa Afya Tanzania Dorothy Gwajima kushoto

Hivyo, ni muhimu kwa watu kuchanjwa kwa wingi ili kujilinda na kuwalinda wengine na maambukizi.

Jambo la pili ni kuwa, kwa mujibu wa mwongozo wa WHO watu wanaotakiwa kuchanjwa ni wale ambao ni wazima wa afya na si wagonjwa.

Hivyo, endapo utabainika kuwa na maambukizi ya corona itakupasa usubiri mpaka pale dalili za ugonjwa huo ziondoke ama kupungua kabisa.

"Madaktari ndiyo wanaweza kushauri endapo mtu hatakiwi kupewa aina Fulani ya chanjo endapo ana historia ya mzio mkali (severe allergy) kutokana na viambata vilivyotumika kutengeneza chanjo husika," inaelekeza WHO.

'Waliochanjwa nje ya nchi wamepata madhara'

Dhana nyengine potofu dhidi ya chanjo inayozungumwa nchini Tanzania na sehemu nyengine ulimwenguni ni kuwa chanjo za corona zina madhara makubwa kwa watumiaji wake.

Kuna wanaosema kuwa zinasababisha vifo, zinavuruga hedhi, zinaharibu nguvu za uzazi kwa wanaume na wanawake na zina shambulia mfumo wa vinasaba na hivyo zinawafanya watu kuwa 'mazombi'.

Hizo zote ni dhana potofu zilizosambazwa na wakataa chanjo duniani, kwa mujibu wa taarifa za WHO na watafiti wengine wa kisayansi ni kuwa madhara makubwa ambayo yanaweza kumpata mtu ni endapo atatumia chanjo ambayo ana mzio (allergy) nayo. Hivyo WHO inashauri madaktari kuwapa taarifa sahihi watu kabla ya kuchoma chanjo ikiwemo kuwakataza kama zinaweza kuwadhuru, kama ilivyoelezwa hapo juu.

Madhara mengine ambayo yameripotiwa japo kwa uchache sana ni ya watu kuganda dam una kupoteza Maisha baada ya kupatiwa chanjo. Kutokana na madhara hayo, chanjo kama AstraZeneca na Johnson & Johnson zilizuiliwa kwa muda katika baadhi ya sehemu duniani lakini baada ya muda zikaruhusiwa kuendelea kutumika.

Kufikia juma la kwanza la mwezi Aprili mwaka huu, watu takriban milioni 25 barani Ulaya walikuwa wameshachomwa chanjo ya Johnson & Johnson (ambayo ndiyo iliyoingia Tanzania) na kati yao ni 83 tu ndio waliopatwa na tatizo la kuganda kwa damu.

Kutokana na takwimu hizo, mamlaka ya ukaguzi wad awa ya Umoja wa Ulaya EMA ikatoa msimamo wake kuwa chanjo hizo ni salama na tatizo la kuganda damu ni la nadra sana.

'Hata ukichanjwa bado unapata corona'

Ndiyo, ni kweli kuwa kuna uwezekano wa kupata maambukizi ya corona hata ukishapata chanjo.

Hili ni suala ambalo linatumika kama hoja kubwa ya upotoshaji katika nchi za magharibi na sasa baadhi ya watu Afrika na hata Tanzania wanaitumia kuogopesha wengine ama kupinga kabisa chanjo za corona wakisema hazina ufanisi.

Lakini kuna uhalisia wa tofauti kabisa juu ya jambo hili. WHO inaeleza kuwa japo ufanisi wa chanjo zilizopo unatofautiana, hakuna ambayo inatoa kinga kwa asilimia 100.

Hospital en India

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Kirusi cha Delta kiligunduliwa mwishoni mwa mwaka jana kilisababisha mlipuko mkubwa wa corona mwanzoni mwa mwaka huu nchini humo.

"Kutokana na uhalisia huo, kutakuwa na asilimia ndogo ya watu ambao wamechanjwa lakini watapata maambukizi ya corona," inaeleza WHO.

Hata hivyo, tofuati na wale wasiochanjwa, wanaopata corona baada ya kuchanjwa hupata dalili za wastani zisizo na madhara makubwa ya kusababishwa kulazwa ama kupoteza maisha.

Hivi karibuni mganga mkuu wa Marekani, Vivek Murthy, alibainisha kwamba asilimia 99.5 ya vifo vitokanavyo na corona nchini humo ni vya watu ambao hawajachanjwa.

Hivyo, kupinga chanjo kwa hojja hii ama yoyote ile ni kuhatarisha maisha na kufanya harakati za kulidhibiti janga la corona kuendelea kuchelewa.