Miaka 10 ya Uhuru wa Sudani Kusini: Vita mbili kuu na harakati za miongo sita ya kutafuta kujitawala

Uhuru wa sudani kusini

Chanzo cha picha, Getty Images

Sudan Kusini ilipata uhuru miaka 10 iliyopita siku kama ya leo baada ya zaidi ya miaka 20 ya mapigano.Vita hivyo vilianza mwaka wa 1983 wakati maasi yalipozuka kusini mwa Sudan hadi mwaka wa 2005 wakati mkataba wa amani ulipotiwa saini kumaliza vita na kuwapa watu wa kusini mwa Sudan uhuru wa kuamua hatima ya nchi yao.Katika msururu wa makala zetu ya maadhimisho ya miaka 10 ya uhuru wa nchi hiyo tunakupakualia kumbukumbu za harakati za kujitawala,matukio muhimu na watu mashuhuri waliohusika na harakati hizo.Katika sehemu hii ya nne na ya mwisho, tunaangazia mwanzo wa mapambano hayo na vita mbili ndefu zilizozaa uhuru wa taifa hilo.

Short presentational grey line

Siku kama ya leo miaka 10 iliyopita, bendera ya rangi sita na nyota katikati yake ilipandishwa. Taifa jipya lenye matumaini tele lilizaliwa. Mpaka sasa hilo ndilo taifa changa zaidi duniani. Ni taifa la Sudani Kusini.

Julai 9, 2011 ilikuwa ni siku ya uhuru ambao mamilioni ya Wasudani Kusini waliutafuta kwa hamu na ghamu. Hamu yake ilikuwa ni ya mustakabali wa kuanza upya na kujitawala wenyewe bila kupangiwa cha kufanya na utawala wa Khartoum.

Siku hiyo pia ilibeba kumbukumbu za ghamu na chonda. Uhuru wa nchi hiyo haukupatikana kwa wepesi, njia ya kuufikia ilijaa madhila ya huzuni, taabu, mabaa ya njaa, vifo na vita.

Harakati za kutaka kupatikana kwa taifa huru la Sudani Kusini zilianza toka miaka ya 1950. Hivyo, wakati uhuru unapatikana 2011, nyuma yake kulikuwa na safari ya miongo sita ya mapambano.

Mwanzo wa harakati, Anyanya

Mwaka 1955 Sudan ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza na Misri. Sudan ikiwa ni miongoni mwa mataifa makubwa ya bara la Afrika (kabla ya kujitenga kwa Sudani Kusini) ilikuwa imegawanyika katika pande mbili, Kaskazini ambapo maendeleo yalikuwa makubwa na kusini ambapo maendeleo yalikuwa finyu.

Waasi wa Anyanya walisaidiwa kimafunzo na silaha na Israeli

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Waasi wa Anyanya walisaidiwa kimafunzo na silaha na Israeli

Tofauti kubwa nyengine ilikuwa ni kaskazini ni eneo ambalo uislamu umetapakaa wakati kusini wengi wakiwa wakristo ama wafuasi wa dini za jadi.

Watu wa kaskazini walikuwa wameshika nafasi nyingi nyeti na za maamuzi ya mustakabali wa nchi baada ya uhuru. Watu wa kusini waliona wanabaguliwa katika nyanja zote katika taifa hilo jipya. Taratibu harakati za kisiasa za kutaka usawa kwa watu wa kusini zikaanza.

Awali harakati zilianza kama mlizamu punde tu baada ya uhuru, zikiambatana na mashambulio madogo, ya kuvizia na kushtukiza. Mambo yalibadilika ilipofikia mwaka 1963 ambapo makundi ya waasi wa kusini yalijiunga na kutengeneza kundi la Anyanya (lenye maana ya sumu ya nyoka), mlizamu ukageuka kuwa mto mkubwa wenye maporomoko na maji yaendayo kasi. Vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya Sudani ikazaliwa.

Waasi wa Anyanya walipata msaada mkubwa wa vifaa silaha na mafunzo kutoka kwa Israeli ambayo ilikuwa katika operesheni maalumu ya kuihujumu Sudani ili isiungane na mataifa mengine ya kiarabu katika harakati za kijeshi dhidi yake.

Vita vilirindima mpaka mwaka 1972 ambapo makubaliano ya amani ya Addis Ababa yalisainiwa baina ya kiongozi wa Anyanya Joseph Lagu na utawala wa Khartoum kumaliza miaka 17 ya mapigano. Viongozi wa Sudan waliahidi kutatua tofauti zao kusini, ikiwa ni pamoja na kulipa eneo hilo uwezo wa kujiendesha kwa kiasi ndani ya nchi moja ya Sudani.

SPLM na vita ya pili ya 'ukombozi'

Vita ya pili ya ukombozi iliongozwa na John Garang

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Vita ya pili ya ukombozi iliongozwa na John Garang

Makubaliano ya Addis hata hivyo hayakutekelezwa kama ilivyotakiwa katika macho ya wanaharakati wengi wa kusini. Miaka 10 baada ya makubaliano ya Addis, uasi wa pili ukazaliwa.

Uasi huu uliongozwa na chama cha ukombozi cha SPLM kutoka mwaka 1983. Chama hicho kiliasisiwa na kuongozwa na Kanali John Garang ambaye pamoja na wafuasi wake ambao walikuwa ni wanajeshi wa Sudani waliasi kutoka katika safu za jeshi ambalo lilikuwa chini ya utawala wa Khartoum.

Wakati Garang na wafuasi wake wakiasi, walikutana na wapiganaji wa kundi la Anyanya II, hawa ni wanamgambo ambao waliendeleza mapambano ya chini kwa chini hata baada ya makubaliano ya Addis.

Awali makundi hayo mawili yaliungana kwa kuwa yalikuwa na lengo moja, lakini muda mfupi tu baadae mgogoro mkubwa ukatokea juu ya uongozi wa harakati zao na kusababisha vita ya miaka mitatu iliyomalizika kwa uongozi wa Anyanya II kupigwa na Garang na hatimaye wapiganaji wote wa kusini kuwa chini ya amri yake.

Lost Boys of Sudan

Chanzo cha picha, Wendy Stone/Getty images

Maelezo ya picha, Zaidi ya watoto wa kiume 20,000 pia walikimbia kusini mwa Sudani kwa kutembea kwa miguu maelfu ya kilomita mpaka Ethiopia na Kenya kukimbia makali ya vita.

Safari hii, vita baina ya Khartoum wa kusini ilichukua muda mrefu zaidi mpaka kumalizika. Mapambano yalidumu kwa miaka 22 mpaka mwaka 2005. Inakadiriwa zaidi ya watu milioni moja walipoteza maisha kusini mwa Sudani katika vita hivyo kutokana na mapigano pamoja na mabaa ya njaa na ukame.

Zaidi ya watoto wa kiume 20,000 pia walikimbia kusini mwa Sudani kwa kutembea kwa miguu maelfu ya kilomita mpaka Ethiopia na Kenya.

Mkataba wa amani na kufariki kwa Garang

Juhudi mbalimbali za kimataifa na kikanda zilifanyika ili kuleta amani ya kudumu katika nchi ya Sudani. Makubaliano kadhaa yalifikiwa lakini utekelezaji wake ukawa na changamoto na hatimaye makubaliano kuvunjika.

John Garang (kulia) akipeana mkono na aliyekuwa rais wa Sudani Omar al-Basir baada ya kusaini makubaliano ya amani ya Januari 2005 nchini Kenya.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, John Garang (kulia) akipeana mkono na aliyekuwa rais wa Sudani Omar al-Basir baada ya kusaini makubaliano ya amani ya Januari 2005 nchini Kenya.

Kufikia mwanzoni wa miaka ya 2000, kwa kiasi mwelekeo wa mazungumzo ukaanza kuonekana kuleta matumaini. Utawala wa Khartoum awali ulikuwa hautaki kukubali mapendekezo yoyote ya kuliachia eneo hilo moja kwa moja na badala yake kutaka kulipa kiasi cha uhuru wa kujiendeshea mambo yake ndani ya Sudani.

Msimamo huo wa Khartoum mwanzoni ndio ulikuwa pia msimamo wa John Garang, lakini ulisababisha kuhasimiana na baadhi ya makamanda wake wakuu kama Riek Machar, ambaye walikubali kukaa meza moja baada ya miaka 11 mwaka 2002.

Januari 2005 SPLM pamoja na serikali ya Khartoum ziliingia makubaliano ya amani ambayo yaliridhia raia wa eneo la kusini kupiga kura ya maoni ya kuamua kama wanataka kujitenga ama kubaki kama jimbo lenye mamlaka ndani ya Sudani.

Baada ya makubaliano hayo, SPLM ikaingia ndani ya seikali ya umoja wa kitaifa huku Garang akiwa makamu wa kwanza wa rais. Hata hivyo, umauti ulimfika Novemba ya mwaka huo baada ya helikopta ya jeshi la Uganda aliyokuwa amepanda kuanguka akiwa safarini kurejea SUdani akitokea kwenye mkutano na rafiki yake rais Yoweri Museveni wa Uganda.

Uhuru...sio mwisho wa vita

Kifo cha Garang kiliitikisa SPLM, lakini haukuwa mwisho wa safari yao ya ukombozi. Kama ilivyoainishwa kwenye makubaliano ya 2005, kura ya maoni ilipigwa mapema Januari 2011. Asilimia 98 ya watu milioni 3.7 waliopiga kura walikubali eneo hilo kujitenga na kuunda taifa jipya.

Rais Salva Kiir (kulia) na Makamu wake Riek Machar

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais Salva Kiir (kulia) na Makamu wake Riek Machar walizama katika mgogoro wa miaka sita ulionza miaka mitatu tu baada ya uhuru.

Uhuru rasmi ukatangazwa Julai 9, 2011 huku Jenerali Salva Kiir akiapishwa kuwa rais wa taifa hilo.

Ilikuwa ni siku ya fanaka kwa watu wa Sudani Kusini waliokuwa nyumbani na ng'ambo. Jumuiya ya kimataifa pia ilishusa pumzi kwa kuona moja ya maeneo ambayo yaliathirika na vita vya muda mrefu ikipata nafasi ya kuanza upya safari ya kuboresha maisha kwa watu wake.

Chini ya miaka mitatu, matumaini hayo yakageuka kuwa ndoto ya mchana, vikosi vya Sudani Kusini vilianza kushambuliana baada ya tofauti za kisiasa baina ya viongozi wakuu wawili wa nchi hiyo kutoka chama kimoja SPLM kufikia kiwango cha juu kabisa.

Mapigano hayo yalilipuka katika mji mkuu Juba baada ya Rais wa nchi hiyo, Salva Kiir kumtuhumu Makamu wake wa Kwanza wa Rais, Riek Machar Pamoja na viongozi wengine 10 kula njama za kutaka kumpindua madarakani.

Machar akautoroka mji huo na kwenda mafichoni na kuongoza uasi kupitia kundi la SPLM/IO. Vita vikarindima mpaka Januari 2020 ambapo Machar alirejea serikalini katika nafasi yake ya awali ya Makamu wa Kwanza wa Rais.

Wakati leo Sudani Kusini ikitimiza miaka 10 ya Uhuru, matumaini ya amani na maendeleo yamereja, hata hivyo kugeuza matumaini hayo kuwa uhalisia ndio mtihani mkubwa unaowakabili viongozi na wananchi wa taifa hilo changa zaidi ulimwenguni.