Miaka 10 ya Sudani Kusini: Viongozi wa kisiasa waliopigiwa magoti na Papa kuacha vita

Salva Kiir na Machar

Chanzo cha picha, Getty Images

Sudan Kusini ilipata uhuru miaka 10 iliyopita baada ya zaidi ya miaka 20 ya mapigano.Vita hivyo vilianza mwaka wa 1983 wakati maasi yalipozuka kusini mwa Sudan hadi mwaka wa 2005 wakati mkataba wa amani ulipotiwa saini kumaliza vita na kuwapa watu wa kusini mwa Sudan uhuru wa kuamua hatima ya nchi yao.Katika msururu wa makala zetu ya maadhimisho ya miaka 10 ya uhuru wa nchi hiyo tunakupakualia kumbukumbu za harakati za kujitawala,matukio muhimu na watu mashuhuri waliohusika na harakati hizo.Katika sehemu hii ya pili tunaangazia vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimechukua zaidi ya miaka sita kati ya 10 ya Sudani Kusini huru.

Short presentational grey line

Julai 9, 2011 nchi ya Sudani Kusini ilipata uhuru wake kutoka kwa Sudan. Siku hiyo ilipokewa kwa mikono miwili kutoka kwa wapenda amani na maendeleo wote barani Afrika na jumuiya ya kimataifa.

Kwa wengi, imani waliokuwa nayo kipindi hicho ilikuwa, sasa nchi hiyo mpya ambayo historia yake imejaa makovu ya vita ilikuwa inafungua ukurasa mpya wa amani, usalama na maendeleo.

Chini ya miaka mitatu, matumaini hayo yakageuka kuwa ndoto ya mchana, vikosi vya Sudani Kusini vilianza kushambuliana baada ya tofauti za kisiasa baina ya viongozi wakuu wawili wa nchi hiyo kutoka chama kimoja SPLM kufikia kiwango cha juu kabisa.

Mapigano hayo yalilipuka katika mji mkuu Juba baada ya Rais wa nchi hiyo, Salva Kiir kumtuhumu Makamu wake wa Kwanza wa Rais, Riek Machar Pamoja na viongozi wengine 10 kula njama za kutaka kumpindua madarakani.

Machar akautoroka mji huo na kwenda mafichoni na kuongoza uasi kupitia kundi la SPLM/IO. Na huo ukawa mwanzo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe katika taifa hilo changa zaidi barani Afrika ambayo iliendelea kwa miaka sita na kusababisha maelfu ya watu kupoteza maisha.

SPLM na historia ya mapambano ya wenyewe kwa wenyewe

Garang and Machar

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, John Garang na Riek Machar (kushoto) walihasimiana kwa miaka 11 kabla ya kuafikiana tena mwaka 2002.

Kulipuka kwa vita hivyo kuliwavunja moyo watu wengi ambao walikuwa wanalipigia upatu taifa hilo kushika njia ya maendeleo na kujikwamua kutoka lindi la dhiki.

Hata hivyo, kwa wafuatiliaji makini wa siasa na harakati za SPLM huo ulikuwa ni mwendelezo tu wa siasa za mapambano baina ya makamanda wa kundi hilo.

SPLM iliundwa mwaka 1983 na John Garang na wafuasi wake ambao walikuwa ni wanajeshi walioasi kutoka vikosi vya Sudani. Mwaka 2013 chama hicho kilitimiza miaka 30 kwa mapambano mapya baina ya Kiir na Machar.

Lakini hata kuzaliwa kwa SPLM kwenyewe kunahusishwa na mapambano ya kutokuelewana kwa makamanda wakuu.

Wakati Garang na wafuasi wake wakiasi kutoka katika safu za jeshi la utawala wa Khartoum, walikutana na wapiganaji wa kundi la Anyanya II ambao walikuwa ni mwamvuli wa makabila zaidi ya 60 ya kusini mwa nchi hiyo ambao walikuwa hawautambui utawala wa Sudan.

Awali makundi hayo mawili yaliungana kwa kuwa yalikuwa na lengo moja, lakini muda mfupi tu baadae mgogoro mkubwa ukatokea juu ya uongozi wa harakati zao na kusababisha vita ya miaka mitatu iliyomalizika kwa uongozi wa Anyanya II kupigwa na Garang na hatimaye wapiganajji wote wa kusini kuwa chini ya amri yake.

Riek Machar kabla ya kukosana na Kiir baada ya uhuru alishawahi kuwa na uhasama na Garang kabla ya uhuru. Wakati Garang akiamini katika kupigania usawa na kuthaminiwa kwa watu wa kusini ndani ya nchi ya Sudani, Machar alitaka mapambano yajikite katika kutafuta uhuru wa kuunda taifa la jipya la watu wa kusini.

Kutofautiana kwa mtazamo baina ya wawili hao kulimsukuma Machar kujiondoa SPLM mwaka 1991 na kukabiliana na vikosi vya Garang mpaka walipokubaliana kuweka tofauti zao na Machar kurejea SPLM miaka 11 baadae mnamo mwaka 2002.

Maelfu ya wananchi wapoteza maisha na umasikini kushamiri

vita na umasikini

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Umasikini uliendelea kukithiri katika muda wote wa mapigano

Vita ya wenyewe kwa wenyewe ya wafuasi wa Kiir na Machar japo ilianza kwa kutofautiana kisiasa lakini ilitumbukia katika tofauti za kikabila na kufanya athari zake kuwa mbaya zaidi.

Kiir anatokea katika kabila kubwa zaidi nchini humo la Dinka wakati Machar akitokea kabila la Nuer ambalo ni la pili kwa ukubwa.

Vita hivyo pia vilifumua kidonda kingine cha zamani cha nchi hiyo ambacho ni matumizi ya ya watoto kama wapiganaji ambapo mashirika ya misaada ya kimataifa yanakisia kuwa zaidi ya watoto 17,000 waliingizwa kwenye mapigano.

Miaka sita ya vita hivyo vilivyokoma Februari 2020 imeshuhudia zaidi ya watu 400,000 kupoteza maisha. Zaidi ya watu milioni nne wameyakimbia makazi yao, kati ya hao watu milioni 1.8 wakiwa wakimbizi wa ndani na zaidi ya watu milioni 2.5 wakikimbilia nchi jirani.

Vita hii pia imefanya janga la umasikini nchini humo kuongezeka ambapo mfumuko wa bei umeshuhudiwa ukipanda mpaka asilimia 300.

Katika miaka sita ya mapigano wananchi walikumbwa na mabaa ya njaa mara kwa mara. Mapambano yalihusisha maeneo ambayo yanategemewa kwa kilimo hali ambayo iliwazuia raia kutolima kwa ufanisi ama kuyakimbia makazi yao kabisa.

Majanga mengine ya njaa yalikuwa ni ya kutengeneza, serikali ya Marekani pamoja na mashirika ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu yaliituhumu serikali ya Kiir kuzuia misaada ya chakula kutofika katika maeneo ambayo waasi wanaungwa mkono.

Papa Francis awapigia magoti Kiir na Machar

Kikwete na viongozi wa Sudani Kusini

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Juhudi mbalimbali zikiwemo za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zilifanyika ili kusitisha vita hivyo.

Katika miaka sita ya vita hivyo, juhudi kadhaa za kikanda zikiongozwa na mataifa ya IGAD, EAC pamoja na nchi jirani kama Kenya, Ethiopia, Uganda, Sudan na hata Tanzania na Afrika Kusini zilifanyika ili kusitisha mapambano hayo.

Makubaliano kadhaa yaliingiwa ya kusitisha mapigano lakini hayakufua dafu. Makubaliano ya kwanza kabisa yakifanyika Januari ya 2014 lakini hayakuheshimiwa na mapambano yakaendelea.

Septemba mwaka 2018 Kiir na Machar waliingia makubaliano lakini makubaliano hayo ya kusitisha mapambano ya miaka mitano kwa wakati yalichukua muda kufanikishwa na yalikutana na vigingi kadhaa ikiwemo mgawanyo wa madaraka pamoja na kuwajumuisha makundi mengine madogo ya waasi katika serikali ya pamoja.

Kutokana na sababu za kiusalama Machar ambaye alikuwa nje ya nchi hiyo aliomba kupewa miezi sita zaidi ili kurejea nyumbani ombi ambalo Kiir alilikubali.

Mwezi Aprili mwaka 2019, viongozi hao wawili walikutana na Papa Francis huko Vatican na katika hali iliyostaajabisha wengi Papa aliwapigia magoti wote wawili na kubusu miguu yao kama ishara ya kuwaomba wasirejee katika mapigano.

"Ninawaomba kama ndugu yenu mbaki katika amani. Ninawaomba kwa moyo wangu wote, tusonge mbele. Kutakuwa na vikwazo vingi lakini visituangushe. Tatueni shida zenu," Papa Francis aliwanasihi wawili hao.

Hatimaye Februari mwaka 2020 Machar alirejea serikalini kwa kuapishwa tena kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na kumaliza kabisa mgogoro huo mbaya zaidi wa kisiasa na kibinaadamu nchini humo.