Miaka 10 ya Uhuru wa Sudani Kusini: ' Ilibaki kidogo tu nimle rafiki yangu aliyefariki ili kujiokoa kufa njaa’

Lost Boys of Sudan

Chanzo cha picha, Wendy Stone/Getty images

Sudan Kusini ilipata uhuru miaka 10 iliyopita baada ya zaidi ya miaka 20 ya mapigano.Vita hivyo vilianza mwaka wa 1983 wakati maasi yalipozuka kusini mwa Sudan hadi mwaka wa 2005 wakati mkataba wa amani ulipotiwa saini kumaliza vita na kuwapa watu wa kusini mwa Sudan uhuru wa kuamua hatima ya nchi yao.Katika msururu wa makala zetu ya maadhimisho ya miaka 10 ya uhuru wa nchi hiyo tunakupakualia kumbukumbu za harakati za kujitawala,matukio muhimu na watu mashuhuri waliohusika na harakati hizo.Katika sehemu hii ya tatutunaangazia simulizi ya watoto waliokimbia vita na kutembea maelfu ya kilomita kwenda Ethiopia mpaka Kenya ili kuwa salama.

John Garang'

Chanzo cha picha, Getty Images

Katika vita ya kupigania uhuru wa Sudani Kusini, watoto walikuwa ni moja ya makundi yaliyoathirika zaidi na mgogoro huo wa miaka 23.

Maelfu ya watoto wa kiume, kuanzia umri mdogo wa miaka saba waliingizwa jeshini na kutumika kama wapiganaji wa mstari wa mbele. Mamia walifariki vitani, mamia wengine walifariki kwa njaa, ukame na maradhi. Lakini kuna maelfu ambao walichukua mkondo ambao baadae uliishangaza dunia.

Zaidi ya watoto 20,000 wa Sudani Kusini walitembea kwa miguu maelfu ya kilomita kupitia Ethiopia mpaka Kenya kukimbia makali ya vita. Wengi kati ya hawa walikuwa wameachwa yatima ama kupoteana na wazazi wao kutokana na vita hii.

Watoto hao walipewa jina ambalo sasa ni maarufu sana la 'The Lost Boys of Sudan' (Wavulana wa Sudani waliopotea). Jina hilo walipewa nawatoa huduma za misaada ya kibinaadamu waliowapokea katika makambi ya wakimbizi ya Ethiopia na Kenya. Si wote waliofika Ethiopia ama Kenya, mamia walipoteza maisha njiani ama kupotea kabisa.

Kwa waliofanikiwa kufika katika kambi za wakimbizi, baadhi yao wameenda nchi za ng'ambo hususani Marekani, wengine wamerejea Sudani Kusini.

Moja ya watoto hao ambao waliathirika moja kwa moja na vita hivyo ni mwimbaji maarufu Emmanuel Jal. Hii ni simulizi ya wavulana hao kupitia masaibu ya Jal kama alivyozungumza na BBC.

'Niliingizwa vitani nikiwa na miaka 7'

Lost Boys of Sudan

Chanzo cha picha, Wendy Stone/Getty Images

Vita vya pili vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan vilianza mwaka 1983 na kumalizika mwaka 2005. Wavulana wengi walijikuta wakikatiza masomo ama kuchukuliwa kutoka kwa wazazi wao wakiwa bado wadogo na kupelekwa mstari wa mbele.

Jal, alikuwa ni miongoni mwao. Vita ilianza akiwa na miaka mitatu, alipotimu miaka saba alichukuliwa na waasi na kupelekwa mafunzoni. Lakini hakujua kama anaenda kuwa askari mtoto.

"Mimi sikuamua niwe mwanajeshi. Tuliambiwa tunakwenda shuleni huko Ethiopia. Baba yangu akanitoa (niende). Tukatembea kwa mguu mpaka Ethiopia. Kufika huko ndipo tukafunzwa kuwa majeshi...Tulikuwa watoto wa miaka saba mpaka 13...Haikuwa rahisi, tunafundishwa kuua watu, kutumia bunduki," anaeleza Jal.

Mafunzo yalikuwa magumu, Jal anaeleza kuwa siku za mwanzoni walikuwa wanapigwa fimbo na wakufunzi wao bila hata ya kufanya makosa. Walikuwa wanaamshwa mapema na kuanza kukimbia.

"Tuliona watoto waliouawa kutokana na kutokufuata maelekezo, na hakuna mtu aliyeshtuka ama kujali...Hilo lilitufanya wote tunyooke...Mimi nilikuwa mtu wa kucheka cheka lakini niliingia kwenye mstari."

Jal alistahmili ukali wa mafunzo ili ajifunze kutumia bunduki na kwenda kulipiza kisasi kwa waliowauwa ndugu na jamaa zake. Mama yake aliuawa katika vita hivyo kabla ya yeye kuchukuliwa na waasi.

'Nilikunywa mkojo ili kujinusuru na kifo'

Emmanuel Jal

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Emmanuel Jal kwa sasa ni mwimbaji na anaishi Canada

Akiwa na miaka 13, Jal alikuwa sehemu ya vikosi vya waasi ambavyo vilihasimiana karibu na mji wa Juba. Askari wengi watoto waliondoka kwenye vikosi vyao kwa lengo la kwenda kuzilinda familia na jamaa zao wasikumbwe na mkasa huo.

Akiwa na wenzake takriban 200, wakaazimia kutorejea tena na kushika njia iliyochukuliwa na wavulana wengine kama wao kuelekea Ethiopia kukimbia makali ya vita.

Safari ya miezi nyikani haikuwa rahisi, wavulana hao walikuwa wakisafiri kwa mguu maelfu ya kilomita kutafuta kambi za wakimbizi, hawakuongozana na watu wazima na walikuwa wakipambana na adha chungu tele njiani.

Bila ya chakula na maji safari hiyo ilikuwa ni kama jaribio la kifo: " Watu walikufa njiani, hatukuwa na chakula. Hatukuwa na maji, ulikuwa unakunywa mkojo wako. Mtu akifa tulikuwa tunasubiria tai waje tunawaua na kula ndege hao."

Jal anasema kuwa baadhi yao walifikia hatua ya kula nyama za wenzao waliofariki, naye ilibaki kidogo ale nyama ya binadau: "Hata mimi mwenyewe nilitaka kula binadamu lakini Mungu alifanya maajabu, ndege alitokea akauawa tukamla.La sivyo ningemla rafiki yangu."

Wakati maelfu wakitembea kwa mguu mpaka kambi ya wakimbizi ya Kakuma Kenya, Jal alipata bahati ya mtende kwa kusafirishwa kimagendo kwa ndege mpaka Nairobi. Katika kundi lake la watoto zaidi ya 200, ni 16 tu ndio waliofika kwenye kambi ya wakimbizi.

Miaka 10 ya Uhuru imekuwaje kwao?

Uhuru ulipatikana miaka 10 iliyopita ambapo kundi hilo lilolokuwa wavulana wakiwa tayari ni vijana ama watu wazima ambao wamepiga hatua fulani maishani. Jal alipotoka Kenya akahamia Canada.

Wengi wao waliazimia kurejea nyumbani na kutoa mchango wao katika maendeleo ya taifa lao changa. Baadhi ya waliokuwa wakiishi ng'ambo kama Jal walirejea kwa shauku. Na hata baadhi ya waliokuwa wapo kwenye kambi za wakimbizi katika maeneo mbali mbali ya Kenya na Uganda walirejea.

Hata hivyo, miaka mingi ya kuwa nje yawezekana iliwafanya wawe wageni zaidi baada ya kurejea. Kulipuka kwa vita ya 2013 kukawafanya wale waliotangulia kurudi warejee ng'ambo na ambao hawakurudi kuachana na mipango hiyo.

Jal, alirejea Canada baada ya kushambuliwa lakini anapanga kurejea tena Kenya.