Kofi la Emmanuel Macron: Kitabu cha Hitler na silaha zapatikana kwa washukiwa

Chanzo cha picha, UGC
Wachunguzi wameripotiwa kupata silaha na nakala ya kitabu cha Hitler- Mein Kampf, nyumbani kwa mmoja wa washukiwa wawili wanaozuiliwa baada ya Rais Emmanuel Macron kuzabwa kofi la usoni akiwa katika ziara rasmi.
Wanaume hao, walio na umri wa miaka 28, walikamatwa nje ya shule ya hoteli kusini mashariki mwa Ufaransa.
Nyumba zao zilipekuliwa baada ya shambulio la Tain-l'Hermitage.
Kitabu na silaha ziliripotiwa kupatikana katika nyumba ya mwanamume ambaye anashukiwa kurekodi video inayomuonesha Bw. Macron akizabwa kofi.
Baadhi ya silaha zilizopatikana ni pamoja na upanga mrefu, kisu na bunduki ambayo mshukiwa alimiliki kinyume cha sheria. Haijabainika ikiwa silaha hizo zilipangwa jinsi zitakavyotumika.
Rais wa Ufaransa alizabwa kofi la usoni alipokimbilia mkusanyiko wa watu waliokuwa wamesimama kando ya bara bara wakiwa wametenganishwa na vizuizi vya chuma, akiwa na walinzi wake.
Msemaji wa Bwana Macron amekanusha madai kwamba alikuwa ameonywa na maafisa wake wa usalama kutowafikia watu hao.
"Bila shaka rais ataendelea kutangamana na raia wa Ufaransa, sawa na wengine wote serikalini," alisema Gabriel Attal.

Chanzo cha picha, EPA
Saa chache baada ya tukio hilo, Bw Macron alisema kisa hicho kilikuwa "cha kipekee" na "watu wenye vurugu"ambao hawapaswi kuruhusiwa kuteka mjadala wa umma.
Washukiwa ni kina nani?
Mtu wa kwanza, anayeshukiwa kumzaba kofi rais, inaaminika alikuwa anavutiwa na viongozi wa mrengo wa kulia na watawala wa kifalme, na pia historia ya zamani ya Ufaransa.
Katika ukurasa wake wa Instagram anajieleza kuwa sehemu ya shirikisho la kitaifa la sanaa ya kijeshi ya kihistoria ya Ulaya, pamoja na picha zake akiwa amevalia mavazi ya kale na akiwa amebeba upanga mrefu.
Lakini kulingana na mmoja wa marafiki zake, Loïc Dauriac, haegemei "mrengo wa kisiasa" na kwamba alikosea kumpiga kofi rais. Tovuti ya Le Parisien ilinukuu chanzo katika uchunguzi huo kama muhtasari wa siasa zake kama "kitendo cha kiitikadi
Mshukiwa pia alisikika akipiga mayowe akisema "Montjoie et Saint-Denis! Down with Macronism". Ingawa alitumia kilio cha vita vya enzi za kati, wafafanuzi wa Kifaransa pia wanaamini kuwa huenda alikuwa anaiga mhusika wa vichekesho kutoka kwa filamu maarufu ya 1993 Les Visiteurs (Wageni).

Chanzo cha picha, Getty Images
Muda mfupi kabla ya kisa hicho, alisimama karibu na wanaume wengine wawili wakati wa mahojiano ya Televisheni, ambapo mmoja wao anasema, "Kuna vitu ungelitaka kumwambia [Bw Macron] lakini kwa bahati mbaya huwezi... kushuka kwa Ufaransa."
Nyumba za washukiwa wote zilipekuliwa katika kijiji cha kaskazini cha Tain-l'Hermitage baada ya tukio la Jumanne. Mshukiwa wa pili anaripotiwa kuwa shabiki wa mapigano ya medieval.













