China imesema mabaki ya Roketi yake imeangukia bahari ya Hindi

Chanzo cha picha, Getty Images
Mabaki ya roketi ya Kichina ambayo ilikuwa ikirudi nyuma kuelekea Dunia imeanguka katika Bahari ya Hindi, shirika la anga za mbali la nchi hiyo linasema.
Sehemu kubwa ya roketi iliharibiwa ilipoingia tena kwenye anga, lakini vyombo vya habari vya serikali viliripoti kwamba mabaki ya roketi yaliangukia magharibi mwa visiwa vya Maldives siku ya Jumapili.
Kumekuwa na siku za kubashiri juu ya roketi inaweza kutua wapi, na maafisa wa Marekani na wataalam wengine walionya kuhusu kuanguka kwake na uwezekano wa kutokea majeruhi.
Lakini China ilisisitiza kuwa hatari ilikuwa ndogo.
Idara ya anga za mbali ya Marekani , wakati huo huo, ilisema tu kwamba roketi "ilikuwa imeingia tena juu ya Rasi ya Arabia". Haikuthibitisha sehemu ya kutua iliyoripotiwa na vyombo vya habari vya China, ikisema badala yake kwamba "haijulikani ikiwa mabaki hayo yameathiri ardhi au maji''.
Huduma ya ufuatiliaji Space-Track, ambayo hutumia data ya jeshi la Marekani , ilisema roketi hiyo ilirekodiwa juu ya anga la Saudi Arabia kabla haijaangukia Bahari ya Hindi karibu na Maldives.
Marekani ilisema nini?
Roketi hiyo kwa jina Long March 5B ilizinduliwa mwishoni mwa Aprili kubeba chombo cha kwanza cha China kitakachokuwa kuwa kituo cha anga za mbali siku za usoni kwenda kwenye mzingo wa dunia.
Kufikia Alhamisi, Marekani ilikuwa imesema inafuatilia njia ambayo chombo hicho inapitia lakini haina mpango wa kuidungua.
"Ni matumaini yetu kuwa itaangukia sehemu salama bila kumdhuru yeyote," amesema Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin. "Matumaini yetu ni kwamba itaanguka baharini, au sehemu nyingine kama hiyo."
Pia imeikosoa China ingawa sio moja kwa moja, na kusema "ni muhimu kuhakikisha tunazingatia mambo hayo wakati tunapanga kufanya operesheni".
Chombo cha habari cha China kinachomilikiwa na serikali siku za nyuma kilipuuzilia mbali hofu ya kuwa chombo hicho kinaweza kulipuka kwenye makazi na kusema kuwa kitaangukia sehemu nyingine ya maji ya kimataifa.
Gazeti la Global Times ilimnukuu mtaalam Song Zhongping ambaye aliongeza kuwa mtandao wa China wa kufuatilia anga la mbali atakuwa anafuatilia kwa karibu tukio hilo na kuchukua hatua stahili iwapo kutatokea uharibifu wowote.












