Mwai Kibaki: Rais aliyebadili uchumi wa Kenya kwa kiwango kikubwa

Rais mstaafu Mwai Kibaki
Maelezo ya picha, Rais mstaafu Mwai Kibaki

Mwai Kibaki alikuwa rais wa tatu wa Kenya ambaye aliiletea nchi hiyo mabadiliko makubwa ya maendeleo na udhabiti wa kitaifa.

Aliingia siasa mapema wakati Kenya ilipojipatia uhuru wake na alifanya kazi katika nyadhfa mbalimbali serikalini .

Baada ya kuhudumu kama makamu wa rais alijipatia uzoefu na maarifa ya kisiasa na uongozi - uzoefu ambao ulimpatia uwezo wa kuongoza kenya katika mwelekeo wa kidemokrasia.

Kenya ilikuwa imetawaliwa na chama tawala cha KANU tangu ilipojipatia uhuru wake 1963.

Rais Mwai Kibaki alianzisha chama chake cha Democratic Pary DP baada ya kutofautiana kisiasa na aliyekuwa rais Daniel Toroitich Arap Moi kabla ya kuanza safari yake ya kutaka kuwa rais wa Kenya.

Baada ya kuchukua madaraka wakati muhimu wa taifa hilo ambapo ilionekana kama mabadiliko mapya nchini humo, akiwa kiongozi aliyechaguliwa kidemokrasia akiungwa mkono kitaifa na kimataifa.

Huku utawala wake ukizongwa na masuala ya ufisadi, Kibaki alianzisha mabadiliko ya kikatiba , kuleta elimu ya msingi ya bila malipo na kufanya juhudi kuinua sekta ya afya iliyozorota .

th

Chanzo cha picha, Getty Images

Maisha yake ya utotoni

Akizaliwa tarehe 15 mwezi Novemba 1931, Mwai Kibaki alikuwa kitinda mimba cha familia ya watoto wanane kutoka kwa mkulima kwa jina Kibaki Githinji na mkewe Teresia Wanjiku.

Akiwa mzaliwa kutoka kabila kubwa la Wakikuyu , aliishi katika kijiji kwa jina Gatuyaini katika kaunti ya Nyeri.

Alionyesha uwezo wa kipekee wa kusoma wakati wa miaka ya shule ya msingi na alitumwa kujiunga na Shule ya Upili ya Man'gu, moja ya shule bora za upili nchini Kenya.

Kibaki alisomea katika shule hiyo kati ya mwaka 1947 na 1950.

Matokeo mazuri yalimsaidia kupata ufadhili wa masomo ambapo alijiunga na chuo kikuu cha Makerere nchini Uganda ambapo alisomea Uchumi, sayansi ya kisiasa na historia.

Uongozi wake ulionekana alipokuwa mwenyekiti wa muungano wa wanafunzi katika chuo kikuu cha Makerere kabla ya kuhitimu na shahada 1955.

Baada ya kuhudumu kama naibu meneja wa kampuni ya mafuta ya Shell nchini Uganda, Mwai Kibaki alipata ufadhili wa kusoma katika chuo cha uchumi cha London.

Alihitimu na shahada ya Uchumi na ufadhili wa umma{ Public Finance}, na alitarajiwa kutumia maarifa yake nchini mwake aliporudi 1958.

Safari yake ya kisiasa

Mwai Kibaki alikubali wadhfa wa mhadhiri msaidizi katika somo la uchumi katika chuo kikuu cha Makerere.

Mwaka 1960, alijiuzulu wadhfa wake na kujiunga na chama cha KANU {Kenyan African National Union} chama tawala nchini Kenya wakati huo.

TH

Mabadiliko kadhaa miaka michache iliofuata yaliisaidia Kenya kujipatia Uhuru wake kutoka kwa Uingereza na miaka mitatu baadaye Mwai Kibaki alikumbatia dunia ya uanasiasa.

Mwaka 1963, alichaguliwa katika bunge la Kenya na kuendelea kuhudumu katika nyadhfa tofauti hadi alipoteuliwa kuwa waziri wa fedha na mipango ya kiuchumi na mwanzilishi wa taifa la Kenya marehemu mzee Jomo Kenyatta mwaka 1969.

Baada ya kujipatia uzoefu na kujiwekea sifa nzuri katika miaka yake ya kwanza katika siasa na serikali, Mwai Kibaki aliteuliwa kama Makamu wa Rais chini ya uongozi wa rais

Daniel arap Moi mnamo 1978, aliyechukua madaraka baada ya mzee Jomo Kenyatta kufariki.

Katika baraza la mawaziri la rais Moi, Kibaki alikabidhiwa wadhfa wa Fedha.

th

Chanzo cha picha, Getty Images

Kama waziri wa fedha Kibaki alianzisha mikakati na mabadiliko ambayo yaliiletea Kenya maendeleo.

Mwaka 1982 alikabidhiwa wadhfa wa waziri wa Masuala ya ndani. Mfumo wa Moi wa Kuongoza uliendelea kuwa ule wa ukandamizaji na alibadilisha kifungu cha katiba na kukifanya chama tawala cha KANU kuwa chama pekee cha kisiasa.

Moi alichukua madaraka yote, na kumuondoa Kibaki kama makamu wa rais kabla ya kumpeleka katika wadhfa wa waziri wa Afya 1988 hatua ilioonekana na wengi kama kumshusha madaraka.

Tofauti ya kimawazo kati ya Moi na Kibaki ilipelekea msomi huyo wa chuo kikuu cha Makerere kujiuzulu kutoka KANU 1991.

Wakati huo raia walianza kulalamika kuhusu ukandamizaji uliokuwepo hatua iliozaa upinzani mkali dhidi ya rais Moi na kumfanya kubadili kifungu cha sheria ambayo ilikuwa imekihalalisha chama cha KANU kama chama cha pekee.

Kibaki alijiuzulu na kuunda chama chake cha Democratic Party DP .

Hatahivyo utawala wa Moi uliendelea kuwa thabiti licha ya taifa kuonekana kutoa upinzani mkali dhidi ya uongozi wake.

Alidaiwa kutumia mbinu za kikabila na ghasia kusalia madarakani katika chaguzi mbili zilizofuata.

Huku Wakenya wakitafuta mtu ambaye angewaunganisha ili kumuondoa Moi madarakani , Kibaki alijiunga na viongozi wengine waliokuwa upinzani kama vile Raila Odinga, Michael Kijana Wamalwa na Charity Ngilu ili kuunda muungano wa upinzani kwa jina National Rainbow Coalition NARC.

Kibaki alichaguliwa kuwa mgombea wa urais wa Muungano huo na mwaka 2002, alishinda uchaguzi wa urais baada ya viongozi kadhaa kuondoka KANU na kuhamia katika chama hicho cha upinzani.

Ushindi wake ulikaribishwa kwa nderemo na vigelegele na matumaini makubwa ya kuboreka kwa maisha ya usoni yalionekana.

Alifanya mabadiliko muhimu ya kiuchumi wakati wa muhula wake wa kwanza kama rais.

Hatahivyo jinamizi la ufisadi ambalo Kibaki alikuwa ameahidi kukabiliana nalo wakati wa kampeni zake za uchaguzi lilisalia kumwinda.

Baadhi ya viongozi wa upinzani ambao waliungana naye walidai kwamba Kibaki alienda kinyume na makubaliano yao.

Wakiongozwa na Raila Odinga viongozi hao walibadilika na kuwa mwiba katika serikali ya Kibaki na kumfanya rais huyo kuwafuta kazi.

Hatua yake ilipelekea kuundwa kwa upinzani ambao ulimtoa kijasho katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2007 uliokumbwa na utata na ghasia za baada ya uchaguzi.

Takriban raia 1000 walidaiwa kuuawa katika ghasia za baada ya uchaguzi huo ambao upinzani ukiongozwa na Raila Odinga uliandamana kupinga matokeo yake.

Na kufuatia ghasia hizo jamii ya kimataifa ikiongozwa na mpatanishi mkuu Koffi Annan aliyeshirikiana na waliokuwa marais wa Tanzania Marehemu Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete waliingilia kati na hatimaye wakabuni serikali ya muungano ambapo huku rais Kibaki akisalia kuwa kiongozi wa taifa, Raila Odingwa alipatiwa wadhfa wa waziri mkuu.

Na baada ya muhula wake kukamilika 2013 alimpatia madaraka mrithi wake Uhuru Kenyatta aliyeibuka mshindi wa uchaguzi mkuu wa urais mwaka huo.

Mwai Kibaki amewaacha watoto wanne,Judy Wanjiku, Jimmy Kibaki, David Kagai na Tony Githinji.